Aliyekuwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' amesema kwa sasa anajifua mwenyewe ili kuweka kiwango chake sawa kabla hajajiunga na timu yoyote.
Ninja msimu uliopita alikuwa na wakati mgumu kupata namba ndani ya kikosi cha Kocha Nassredine Nabi akiwa Yanga hadi kupelekwa kwa mkopo Dodoma Jiji na aliporudi hakuwa na nafasi.
Akizungumza na Mwanaspoti Ninja alisema, hana papara kwa sasa ndio maana ameamua kutulia ili kufanya maamuzi sahihi.
"Kwa sasa nipo tu nyumbani nafanya mazoezi yangu kuhakikisha nakuwa sawa muda wote ili nikipata timu niweze kuhimili ushindani nitakaoukuta," alisema Ninja. Ninja alisema kuna timu nyingi zinahitaji huduma yake na yeye hataki kukurupuka, anacholiangalia ni masilahi na sio ilimradi kupata timu.
"Dirisha bado halijafungwa, naamini kwa uwezo wa Mungu nitapata timu ya kucheza, siwezi kukosa muda mwingi upo," alisema Ninja.
Kuhusu ushindani anakiri upo katika kila timu hivyo zinahitajika juhudi binafsi ili kocha aweze kumwamini mchezaji na kumpa nafasi.