Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nini Morocco? watu tuliona Cameroon buana 1990

Camerron 1990 wachezaji wa Cameroon walioshiriki Kombe la Dunia 1990

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jana ilikuwa ni Fainali ya Kombe la Dunia. Mechi ya fainali ilizikutanisha Argentina na Ufaransa. Kwa mara nyingine Afrika inakosa nafasi ya kutinga mchezo wa mwisho wa fainali.

Timu ya Taifa ya Morocco iliyobeba matumaini ya Waafrika wengi ilipotea na kutolewa kinyonge na Ufaransa baada ya kufungwa mabao 2-0.

Sitaki kuingia katika vita vya Uafrika wa taifa hilo, binafsi sina budi kuipongeza Morocco kuwa timu ya kwanza Afrika kutinga nusu fainali, lakini naamini rekodi hiyo ilipaswa kuandikwa mwaka 1990 na Timu ya Taifa ya Cameroon.

UBABE WA CAMEROON

Uliwaona Morocco walivyokuwa wakikaba? Basi wachezaji wa Cameroon walikuwa kama mbwa mwitu waliokuwa na njaa ya mafanikio.

Cameroon wachezaji wengi wakiwa na miili iliyoshiba na kuwa fiti, ilicheza soka la vipaji halisi vya Kiafrika kwa kuuchezea mpira na kuzisumbua timu ngumu za barani Ulaya.

Walikuwa wanaupiga mwingi ni timu ambayo ilitegemewa kubeba taji lililokuja kubebwa na Ujerumani. Mwaka 1990 Cameroon ilipaswa kuandika historia kubwa duniani. Iliishangaza dunia kwa hatua ilivyofikia. Ilitabiriwa kufanya makubwa zaidi lakini bahati mbaya wachezaji hawa walipoondoka wakaondoka na kizazi cha dhahabu cha nchi hiyo.

Baadaye Senegal (2022) na Ghana (2010) zilifikia rekodi ya kufika robo fainali. Laiti penalti ya Asamoh Gyan isingeota mbawa Ghana ingeanza kuandika historia ya kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza kwa timu za Afrika.

Cameroon ilianza hatua ya makundi kibabe Juni 8, 1990 ikiwa Kundi B iliwachapa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Argentina bao 1-0 katika dakika 67, bao la Francious Omam - Biyik

Kabla ya mchezo huo kuanza, nahodha wa Argentina, Diego Maradona alikuwa akipiga danadana na kuuchezea mpira kwa kutumia viungo vyake wakati huohuo kamera zikamvuta beki na nahodha wa Cameroon, Emmanuel Kunde akikaza kamba za viatu vyake kuashiria kulikuwa na kazi nzito.

KUNDE ZAIDI YA BEKI

Katika fainali hizo, beki huyo mbali ya kuwa nahodha alikuwa akicheza kutokana na ukali wa timu pinzani. Kama mchezaji wa timu pinzani mkali alikuwa anatokea pembeni, basi na yeye angecheza upande huo. Kama mtu hatari alikuwa katikati naye alikuwa akisimama kama beki wa kati.

Cameroon ilikuwa na wachezaji nguli kwelikweli ambao walikuwa watu waliotumwa kazi. Katika mchezo huo wa kwanza wachezaji wawili walitolewa kwa kadi nyekundu Andre Kana Biyik dakika ya 61 na Benjamin Massing dakika 89.

Kikosi cha Cameroon kilikuwa na Thomas Nkono, Bertin Ebwele, Victor Ndip, Emmanuel Kunde, Benjamin Massing na Steven Tawtaw.

Wengine ni Andre Kana Biyik, Cyrille Makanack (Roger Milla), Emile Mbou, Fronsoir Omam Biyik na Thomas Libiih (Loius Paul Mfede).

Kumbuka Argentina ilikuwa bingwa mtetezi ikitoka kuchukua ubingwa Mexico 1986 ambapo Maradona aling’ara vya kutosha. Mbali na kusakata kabumbu Cameroon walikuwa wametawala kwa ubabe na waathirika wakubwa wa faulo za wababe hao walikuwa ni Maradona na Claudio Cannigia.

Maradano peke yake alichezewa faulo 11 za hatari. Mechi ya pili, Cameroon ilicheza na Romania na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Roger Milla alifunga mabao yote mawili katika dakika 77 na 87 hapa ndipo alipoibuka na staili ya kushangilia kwenye kibendera cha kona kwa kukata viuno.

Romania ilipata bao la kufutia machozi dakika 89 kupitia Garvil Balint. Kumbuka Romania ilikuwa kiungo mshambuliaji, Gheorghe Hagi. Mechi ya tatu, Cameroon ilicheza dhidi ya Colombia ya kipa mwenye mbwembwe, Rene Higuita. Wababe hao wa Afrika walishinda 2-1 mabao ya Cameroon yakifungwa na Milla tena.

Baada ya mchezo kwenda sare hadi dakika za nyongeza baada ya kutoka sare tasa katika dakika 90. Milla alifunga bao la kwanza katika dakika 106 na lingine ambalo alimnyang’anya mpira Higuita aliyekuwa akifanya mbwembwe na kufunga katika dakika 109. Colombia ilipata bao dakika ya 116 lililofungwa na Bernardo Redin.

MECHI ILIYOFUTA NDOTO

Katika kutaka kutimiza ndoto za kwenda kucheza fainali na hata kuchukua taji hilo mwaka huo, Cameroon iliangukia mikononi mwa England.

Gemu ilikuwa ngumu kwelikweli. David Platt aliiongoza England katika dakika 26. Kipindi cha pili Milla aliingia na kuchezewa faulo wakati akiwa anakwenda kumuona kipa wa England, Peter Shilton. Kunde alifunga kwa penalti.

Katika dakika 65, Eugune Ekeke aliindikia bao Cameroon, hapo kila mtu aliamini timu hiyo ilikuwa inakwenda nusu fainali.

Ndoto za Afrika za kuitaka Cameroon itinge nusu fainali zilikatishwa kwa penalti mbili ambazo zilifungwa na Gary Lineker katika dakika za 83 na 105.

Hata hivyo, Tim ya Taifa ya England haikuwa ya kitoto, ilikuwa na watu wa kazi. Ilikuwa ya moto kwelikweli ikiwa na mastaa kama kina Paul Gascoigne ‘Gaza’, Paul Parker, Chris Waddle, Stuart Pearce, John Barnes, Mark Wright na Terry Butcher. Wengine ni Gary Lineker, Peter Beardsley, Chris Woods na wengine wengi.

MILLA MKONGWE ZAIDI

Staa huyo wa Cameroon anashikiria nafasi ya tatu kwa wachezaji wenye umri mkubwa zaidi kushiriki Kombe la Dunia.

Milla aliacha kucheza fainali hizo akiwa na umri wa miaka 42 na siku 39.

Mbele ya Milla wapo Mcolombia, Faryd Mondragon (miaka 43 na siku 3) na anayeshika namba moja ni raia wa Misri, Essam El-Hadary(miaka 45 na siku161)

Pia, Milla ni mmoja kati ya wafungaji wakongwe mwaka1990 alikuwa na umri wa miaka 38 kwa sasa ana miaka 70.

Mastaa wengine wa Cameroon 1990 hawa hapa, Joseph Antonio Bell, Jules Denis Onana, Bertin Ebwele, Alphonce Yombi, Jean Claude Pagal, Boneventure Djonkep, Rogae Feutmba, Emmanuel Maboang, Jaques Sango.

Chanzo: Mwanaspoti