Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nini Luis? Jangwani inaleta jembe hili!

90040 Luis+pic Nini Luis? Jangwani inaleta jembe hili!

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

INAWEZEKANA mashabiki wa Simba kwa sasa wanachekea chini chini baada ya mabosi wao kuwakata stimu wenzao wa Yanga kwa winga na nahodha wa UD Songo, Luis Jose Miquissone, lakini wala wasibweteke kwani watani wao hao wanaleta mashine nyingine matata.

Ndio! Mabosi wa Yanga wanadili na kusaka wachezaji kwa ajili ya usajili wa dirisha dogo baada ya kubaini ni vigumu kumpata winga huyo wa klabu huyo ya Msumbiji wameamua kumlia ‘taimingi’ mkali mwingine anayekipiga Afrika Kusini, Orebotse ‘Bobo’ Mongae ili atue Jangwani.

Winga huyo kwa sasa anakipiga Baroka FC aliyokuwa akiichezea Abdi Banda na tayari mikakati imeanza kimyakimya kwa mabosi wa Yanga baada ya kubaini watani wao ni kama kivuruge tu kwenye usajili wa Jangwani baada ya kumdandia juu kwa juu Luis waliyempotezea awali.

Ipo hivi. Mabosi kutoka Kamati ya Ufundi ya Yanga wamebaini uwezo mkubwa alionao winga huyo anayemudu kucheza kushoto na kulia na hata kati na uwezo wa kutupia kambani na kulipelekea jina lake fasta kwa bilionea wa klabu hiyo, GSM ili amshushe kabla dirisha halijafungwa Januari 15. Mongae ni winga mwenye kasi na mbunifu wa kutengeneza nafasi na kufunga kama ilivyokuwa kwa Luis aliyekuwa akihitajiwa Jangwani kuziba jumla pengo la Saimon Msuva anayekipiga Difaa el Jadida ya Morocco kwani, tangu alipotimka klabu hiyo hajapatikana wa kuiziba kikamilifu.

Habari kutoka kwa mmoja wa viongozi wanaodili na usajili, alilitonya Mwanaspoti tayari kuna watu ambao walipewa kazi ya kumfuatilia staa huyo ambapo wamejiridhisha kuwa anaweza akaziba pengo la Msuva.

Kigogo huyo alisema wanatambua Simba nao imeanza kuleta chokochoko za kumrubuni mchezaji huyo, lakini wanajiamini watamfanikisha kutokana na mazungumzo yao yalipofikia.

“Kuna maskauti waliotumwa kumfuatilia Mongae na pia tumeangalia baadhi ya video za kazi zake, ana kasi, mnyumbulifu na mbunifu kama alivyokuwa Msuva aliyekuwa anafunga mpaka kuchukua kiatu cha dhahabu,” kilisema chanzo hicho. Yanga imeshawanasa Ditram Nchimbi, Tariq Seif, Adeyum Saleh na Haruna Niyonzima, hivyo kama dili la mchezaji huyo aliyezaliwa Julai 31, 1993 atatua Jangwani itaongeza udambwidambwi kabla ya mechi ya watani, Januari 4.

Awali ilionekana Yanga ingekuwa na kibarua cha kumng’oa Mongae ndani ya Baroka kwa vile alikuwa na mkataba na klabu hiyo hadi 2021, kwani alijiunga nayo Julai 1, 2018 akitokea Jwaneng Galaxy ya Botswana, lakini wamerahisishiwa kazi baada ya klabu hiyo iliyo kwenye hali mbaya katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), kutangaza kumsitishia yeye na wenzake watatu.

Inaelezwa uongozi wa klabu hiyo umesitisha mkataba wa Mongae sambamba na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Mduduzi Mdantsane, Thato Madigoe na Matome Mabeba - uamuzi unaoelezwa umewashtua mashabiki wa klabu hiyo kwani umekuja saa chache baada ya Kocha wao Wedson Nyirenda kujiuzulu nafasi yake kutokana na timu kufanya vibaya katika PSL.

Kabla ya kujiunga na Jwaneng 2014, Mongae alianza kung’ara timu ya Chuo Kikuu cha North-West na akiwa Botswana Jwaneng ilimtoa kwa mkopo Miscellaneous SC Serowe pia ya Botswana hadi Juni 30 mwaka jana aliporejea Jwaneng iliyoamua kumuuza Baroka ambako amekuwa akifanya mambo kama winga na wakati mwingine kama mshambuliaji.

“Kama mambo yataenda tunavyotaka jamaa anaweza kutua mapema ili kumalizana naye, lakini ni kati ya wachezaji watakaotufungia dirisha letu la usajili baada ya kina Tariq,” chanco hicho kilisisitiza.

Chanzo: mwananchi.co.tz