Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nilishawahi kuwafunga Al Ahly, kesho sitopaki basi - Gamondi

Gamondi Msondaz Nilishawahi kuwafunga Al Ahly, kesho sitopaki basi - Gamondi

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Miguel Gamondi na Kennedy Musonda, leo wamezungumza mbele ya waandishi wa habari nchini Misri kuelekea mchezo wa kesho Ijumaa dhidi ya Al Ahly.

Mchezo huo wa kuhitimisha Kundi D la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utachezwa Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri kuanzia saa 1:00 kwa saa za Afrika Mashariki.

Gamondi amesema katika mchezo huo, hatacheza kwa kuzuia sana kwani yeye ni kocha anayeamini mpira wa miguu ni shoo, hivyo burudani itakuwepo, huku akibainisha kwamba, anahitaji ushindi.

“Kiukweli tunakwenda kukabiliana na mchezo mgumu sana na muhimu kwetu na hata Al Ahly, tunafahamu ni aina gani ya timu tunacheza nayo, tutajaribu kucheza aina ya soka letu ambalo watu wanafahamu Young Africans inachezaje.

“Tunatarajia kuwa na mchezo wa mbinu zaidi, ninaiheshimu Al Ahly, hatuogopi kucheza na timu kubwa Afrika, tunataka kuonesha uimara wetu, tumekuja hapa kujaribu kushinda.

“Mimi sio kocha wa kupaki basi, binafsi ninaamini mpira wa miguu ni shoo, ukiangalia historia yangu nilipokuwa Zamalek au Hassania Ghadir tulikuwa tunacheza zaidi soka la kushambulia.

“Siwezi kubadilisha mbinu, hivyo simuogopi mpinzani ninayekutana naye, ninamuheshimu. Ninawaamini wachezaji wangu, falsafa ya mpira wa miguu, utaona kesho uwanjani namna tutakavyocheza, tusubiri hilo.

“Siku zote ninapoiandaa timu ninaiandaa kushinda, tuna matatizo kadhaa ya wachezaji wetu ambao ni majeruhi.

“Napenda kurudia kwamba, ninawaheshimu sana wapinzani, nimeshawahi kucheza na Al Ahly nikiwa Platinum Stars, kama unakumbuka tuliwafunga Al Ahly nikiwa Afrika Kusini na kuweka rekodi ya timu ya kwanza kuifunga Al Ahly nchini Afrika Kusini, tukaja hapa tukacheza vizuri lakini tukapoteza kwa magoli 2-0, Al Ahly wakafuzu. Kwangu hii ni mtihani mkubwa.

“Ama hakika kesho, kwa maoni yangu na kutokana na uzoefu wangu, itakuwa mechi nzuri kwa sababu Young Africans ni timu nzuri, lakini katika michuano ya kimataifa haina uzoefu mkubwa ingawa msimu uliopita ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho.

“Malengo yalikuwa ni kufuzu, timu haikufuzu kwa miaka 25, tumepambana imewezekana. Kwa kesho tupo tayari na wachezaji wapo tayari kushindana na kuifunga Al Ahly, tutafanya kila tuwezalo, tupo tayari.

“Pacome aliumia, tutaangalia kama tumchezeshe hivyo hivyo au lah, tutaona kesho itakavyokuwa,” alisema Gamondi.

Kwa niaba ya wachezaji, Musonda alisema: “Tunashukuru kwa kutukaribisha, sisi kama wachezaji tunajisikia vizuri kucheza na timu kubwa Afrika hasa katika mechi za kimashindano, hiyo itasaidia kuonesha ukubwa wetu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: