Timu ya taifa ya Nigeria imekamilisha tathmini iliyosababisha kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wa fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Guinea ya Ikweta na sasa wanajiwinda kwa mchezo unaotazamiwa kuwa wa kuvutia dhidi ya wenyeji Ivory Coast baadae leo Alhamis (Januari 18).
Ivory Coast inayoongoza kundi wakiwa mabingwa mara mbili wa michuano hiyo, watataka kukata tiketi ya mapema kuingia hatua ya mtoano kwa kuwafunga Nigeria Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara ulio kwenye mji wa Ebimpe.
Nigeria, mabingwa mara tatu wa mashindano hayo na wakiwa nafasi ya pili wakifungana na Guinea ya Ikweta kwa pointi kwenye Kundi A wamedhamiria kuibuka na ushindi kuweka hai matumaini yao kuingia hatua ya mtoano.
Beki wa timu hiyo, William Ekong aliyeiongoza timu hiyo kwenye mhezo wa Jumapili (Januari 14) amewaomba mashabiki wa soka wa Nigeria kuiunga mkono timu hiyo wakati huu wakisaka pointi tatu dhidi ya wenyeji Ivory Coast baadae leo Alhamis (Januari 18).
“Tulingia kwa dhamira ya kuchukua pointi tatu dhidi ya Guinea ya lkweta, lakini haikuwezekana. Tunaishi tupigane siku inayofuata Kwa upande wetu, tunawaomba mashabiki wa Nigeria duniani kote kuendelea kutuunga mkono na kuamini timu yao. Malengo yetu, kwanza kufika hatua ya mtoano na kuanzia hapo tutapambana kusonga mbele zaidi.”
Nigeria walitengeneza nafasi za kutosha dhidi ya Guinea ya lkweta, lakini umaliziaji mbaya ulifanya watoke sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopigwa Jumapili (Januari 14).
Kocha Jose Peseiro amepata matumaini baada ya kurejea kwa washambuliaji wake Kelechi Iheanacho na Terem Moffi na kambi ya timu hiyo inaamini safu yao ya ushambuliaji iliyofunga mabao 22 kwenye michezo ya kufuzu wangeweza kufunga zaidi kwenye mchezo wa Jumapili (Januari 14).
“Tunatarajia mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Ivory Coast ni wenyeji na wanaongoza kundi letu. Lakini tuna malengo yetu pia na tunajiamini” amesema beki wa timu hiyo, Kenneth Omeruo.