Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nicolas Pepe afunguka maisha ya Arsenal

Nikolasa Pepe Pepe na Mikel Arteta

Mon, 3 Jul 2023 Chanzo: Dar24

Kiungo Mshambuliaji kutoka Ivory Coast Nicolas Pepe, amekiri uhusiano wake na Kocha Mkuu wa Arsenal Mikel Arteta, haukuwa mzuri, lakini alimsifu bosi huyo kwa kujitolea kwake kumsaidia kuwa mchezaji bora.

Pepe alijiunga na Arsenal msimu wa majira ya joto mwaka 2019 kwa ada ya rekodi ya klabu ya Euro milioni 72 rekodi ambayo inatazamiwa kuvunjwa na uhamisho wa Declan Rice wa Pauni milioni 105 kwenda Emirates lakini alishindwa kuonesha kiwango kilichotarajiwa.

Kiungo huyo ana mabao 27 na asisti 21 katika mechi 112 alizoichezea Arsenal, lakini mechi 50 kati ya hizo alikuja kama mchezaji wa akiba huku Pepe akihangaika kupata nafasi ya kuanza.

Hapo awali alisajiliwa chini ya kocha Unai Emery, lakini Pepe ametumia muda mwingi wa maisha yake ya uchezaji Arsenal chini ya Arteta, ambaye alijiunga na ‘Washika Bunduki’ hao miezi minne baada ya kuwasili na ripoti zimekuwa zikieleza kwamba wawili hao walikuwa hawaivi kabisa.

Ingawa Pepe amekiri kuwa hakubaliani na maamuzi ya Arteta, lakini alimsifu Kocha huyo kutoka Hispania kwa dhamira yake ya kuleta kilicho bora zaidi kutoka kwake.

“Watu wanasema kwamba alinitambua kama mchezaji ambaye hakuwa katika kiwango cha timu yake, katika falsafa yake. Ni uongo kabisa,” amesema Pepe kwenye mahojiano na Mail.

“Alipofika, alikuwa na falsafa ya Manchester City. Alikuwa na kikosi kilichojaa ubora katika kila nafasi. Alipozungumza nami, alisema ananitegemea, alitaka nifanye hili au lile.

“Msimu wa kwanza ulipoisha, alizungumza na mimi na kuniambia nifanye hiki au kile, msimu wa pili unakuja, nilikuwa mbadala, nilikuwa nikichanganyikiwa, ningewezaje kuwa mbadala wakati alisema ananihesabia.

“Kila kitu kinazunguka kichwani mwako. Nilikuwa mbadala wa mechi 10. Ilikuwa ni wakati wa kumsajili Willian. Yeye ni namba 10 au winga, lakini anacheza kwenye winga kama namba 11.

“Lakini hilo liliimarika kwa maana ya kwamba alinipa nafasi, nilifunga dhidi ya Sheffield United pale Emirates. Kujiamini kulianza kurejea. Nilianza kuzungumza vizuri.

“Alinisaidia kwa kila hali, kwa kiwango cha mbinu, katika akili ya mchezo kwa sababu falsafa yake inahitaji akili nyingi. Alijua uchezaji wangu si kusubiri kumiliki mpira.”

Kwa kuwa Pepe sasa amerejea Arsenal, itabidi uamuzi ufanywe kuhusu mustakabali wake. Winga huyo amebakiza miezi 12 tu kwenye mkataba wake na alikiri kuwa bado hana uhakika wa kuhama kwake.

“Nitarejea Arsenal. Nilitolewa kwa mkopo bila chaguo la kuninunua hivyo lazima nirudi Arsenal.”

Chanzo: Dar24