Jana tumeona wachezaji wa Ligi Kuu ya NBC wakiziwakilisha timu zao za taifa kwenye michuano ya AFCON 2023 na kuzisaidia kushinda na kupata alama tatu kwenye hatua ya makundi.
Mchezo wa mapema tulimshuhudia Stephane Aziz Ki akiiwakilisha Burkina Faso dhidi ya Mauritania kwa dakika takribani 85 na timu yake ikashinda lakini baade Djigui Diarra alikuwa kwenye goli la Mali wakati wakicheza dhidi ya Afrika Kusini na akaiwezesha Mali kupata ushindi.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukisubiri timu za Ligi yetu kuwa na wachezaji wa aina hii, wachezaji wa kigeni ambao wanapata nafasi ya kucheza kwenye timu zao za taifa. Ni fahari kubwa kabisa!
Zamani ilikuwa ni ngumu kumshawishi mchezaji wa Afrika Magharibi kuja kucheza Ligi ya Tanzania, labda kwa mchezaji ambaye yupo nyakati za mwisho za kumalizia soka lake lakini haikuwa kwa mchezaji ambaye anacheza timu ya taifa.
Kwa sasa klabu zetu zina uwezo wa kuchukua mchezaji ambaye anaanza kwenye kikosi cha kwanza cha timu timu ya taifa kutoka ukanda wa Afrika Magharibi.
Leo tunaweza kuona wachezaji wengine wa Ligi ya Tanzania wakicheza kwenye timu zao za taifa, ukiacha wale wa Taifa Stars DR Congo yupo Henock Inonga na Zambia kuna Kennedy Musonda na Clatous Chama ambao kama watapata nafasi wataiwakilisha Ligi Kuu ya Tanzania.