Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni zamu ya Aziz Ki

Aziz KI National Team Aziz Ki

Tue, 16 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni zamu ya Stephane Aziz KI. Chama lake la Burkina Faso litarusha kete yake ya kwanza kwenye Afcon 2023 leo Jumanne kwa kukipiga na Mauritania katika mechi inayotazamiwa kuwa na ushindani mkali mjini Bouake.

Rekodi zinaonyesha Burkina Faso na Mauritania zimewahi kukutana mara nne, mara mbili kwenye mechi za kirafiki na mbili nyingine kwenye kufuzu michuano ya Afcon, Kundi I mwaka 2019.

Katika mechi hizo, Burkina Faso imeshinda mbili, sare moja na Mauritania ikishinda moja. Hivyo, moto utawaka wakati watakapochuana kwenye mechi zao za kwanza za hatua ya makundi kwenye Afcon 2023 huko Ivory Coast.

Wakati mchakamchaka wa Afcon 2023 ukiingia kwenye siku yake ya nne, mechi nyingine itakayopigwa leo, Tunisia watakuwa na kazi nzito mbele ya Namibia uwanjani Amadou Gon Coulibaly.

Rekodi zinaonyesha Tunisia na Namibia zimekutana mara moja tu, kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika 2007 na miamba ya Tunisia iliibuka na ushindi wa mabao 2-0. Itakuwaje safari hii? Ngoja tuone. Kila timu imejiandaa vyema kwa mechi hiyo na tayari kuwapa uhondo wa kutosha mashabiki wao.

Kivumbi na jasho kitakuwa kwenye mchezo wa usiku, wakati Mali itakapokuwa na kibarua kigumu mbele ya Afrika Kusini. Mara tatu za mwisho Mali na Afrika Kusini zilipokutana, vijana wa Bafana Bafana wameshinda mara mbili na kutoka sare moja.

Lakini, kwenye Afcon mambo yamekuwa tofauti na matamu zaidi. Kingine kinachovutia ni kikosi cha sasa cha Mali kusheheheni mastaa wenye uwezo mkubwa ambao inaaminika wataiweka Afrika Kusini kwenye majaribu makubwa muda wote wa mchezo.

Hii ni mara ya tatu kwa Mali na Afrika Kusini kukutana kwenye mikikimikiki ya Afcon na mara mbili, Mali imetamba mbele ya wapinzani wao hao na mara zote zilikuwa mechi za mtoano.

Kingine kinachoitisha Afrika Kusini katika mchezo huo ni Mali haijawahi kupoteza mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi kwenye Afcon, imeshinda saba na kutoka sare mbili.

Hata hivyo, wana rekodi mbaya hawajawahi kushinda mfululizo kwenye michuano ya aina moja tangu mwaka 2004. Kwenye mechi za kufuzu, Mali ilifunga mabao 15 na ilizidiwa na Nigeria pekee, mabao 22.

Hata hivyo, mabao yao tisa ya mwisho kwenye michuano ya Afrika imefunga kwa mikwaju ya penalty na tatu zilifungwa na Ibrahima Kone kwenye Afcon 2021.

Fowadi ya Afrika Kusini kwenye Afcon imekuwa si tishio sana, haijawahi kushinda zaidi ya bao moja katika mechi tisa zilizopita za michuano hiyo ya ubingwa wa Afrika. Mara ya mwisho kufunga bao zaidi ya moja, ilikuwa kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Morocco, kwenye hatua ya makundi ya Afcon 2013.

Wakati Afrika Kusini ikiwa na wakati mgumu kwenye kufunga mabao, imekuwa na rekodi mbaya pia ya kuruhusu nyavu zake kuguswa kirahisi. Je, usiku wa leo wataweza kuwazuia Mali wasifanye jambo lao? Patachimbika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live