Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni weka, tuweke Simba SC

Kanoute Pic Data Wachezaji wanaohusishwa na Simba SC

Sun, 8 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Baada ya kukamilisha usajili Peter Banda kutoka Malawi, mabosi wa Simba hawajamaliza kazi kwani, wanajiandaa kumshusha kiungo fundi wa mpira anayekaba na kushambulia, Saido Kanoute kutoka Mali ili kuja kuwa pacha na Mganda, Taddeo Lwanga.

Kiungo aliyeng’ara kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji waliopo ardhi ya Afrika (CHAN 2020), ni pendekezo la Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes aliyewaagiza mabosi hao kumtafutia kiungo mwenye sifa ya kukaba na kushambulia (box to box), ile aje kucheza pamoja na Lwanga.

Awali Gomes aliwaambia mabosi wake hao kuna viungo watatu wenye sifa hizo anazohitaji na wote ni raia wa Mali na ndipo wakaanza kuwafuatilia na kuridhika kabla ya kukubaliana wamchukue Kanoute anayeichezea Al-Ahli Benghazi ya Libya.

Taarifa hiyo kutoka ndani ya Simba inaelezwa rasmi viongozi wao hawakuridhika na viungo wengine wawili ambao majina yao yamekuwa siri na kuvutiwa na uwezo wa Kanoute (24) ili aje kuliamsha na nyota wengine wa mabingwa hao wa Ligi Kuu na Kombe la ASFC.

Hata hivyo, Simba italazimika kubomoa benki ili kumpata Kanoute kwa vile mkataba wake ndio kwanza mpya kwani alisajiliwa Mei mwaka huu na utadumu hadi mwaka 2024, japo bilionea wa klabu hiyo, Mohamed ‘Mo’ Dewji alikaririwa hivi karibuni akitamba kuwa wakimtaka mchezaji yeyote lazima wambebe ili kutimiza malengo.

Simba iliyofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili ndani ya miaka mitatu, imepania kutwaa ubingwa wa Afrika, hivyo imekuwa ikisaka wachezaji wenye uwezo wa kutimiza hilo na hasa ikizingatiwa inatarajia kuvuta Pesa ya maana kwa kumuuza Luis Miquissone kwa Al Ahly ya Misri.

“Kuna mazungumzo yameanza kufanyika kati yetu Simba na Al-Ahli Benghazi ili kuona namna gani tunaweza kumpata Kanoute aliyetumikia mkataba wake kwa msimu mmoja tu katika kikosi hicho,” alisema Mjumbe mmoja wa Bodi ya Simba, bila kutaka kutajwa jina.

“Ndio kwanza tumeanza mchakato wa kumpata Kanoute na shida kubwa mchezaji huyo alisaini mkataba wa miaka mitatu kwa timu anayoitumikia na uzuri ni tangu amefika Benghazi ameonekana kutokuwa na furaha na hiyo ni sababu kubwa kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara jambo ambalo kama watakubali kumuachia kwetu tutamtumia zaidi kuliko huko.”

Kanoute alijiunga na Benghazi Mei 3, 2021 kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Stade Malien iliyopo Ligi Kuu ya Mali na mkataba wake utamalizika Desemba 31, 2024.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz