Wakati zikibaki mechi nne huku kila timu ikipiga hesabu kuweza kubaki salama ligi kuu, presha imeonekana kuwa kali kwa timu za taasisi za jeshi na zile zinazomilikiwa na Halmashauri kutokana na matokeo zilizonazo.
Katika ligi kuu timu tatu zinamilikiwa na jeshi ikiwa ni Tanzania Prisons (Magereza), Ruvu Shooting na Polisi Tanzania, huku Halmashauri zikiwa nazo nne ambazo ni Geita Gold, Mbeya City, Dodoma Jiji na KMC.
Hadi sasa timu zilizopo kwenye sehemu salama ni Geita Gold ya Halmashauri ya Mji wa Geita ambayo ipo nafasi ya tano kwa pointi 37, huku Tanzania Prisons ikiwa anagalau inapumua kwa pointi 28 nafasi ya 10.
Dodoma Jiji (Dodoma), hawapo salama sana wakiwa nafasi ya 11 kwa pointi 28, huku Mbeya City (Mbeya) ikiwa nafasi ya 13 kwa alama 27, huku Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zikinyukana nafasi mbili za mkiani.
Timu zote hizo zimebakiza mechi nne, ambapo Aprili 21, Prisons itanyukana na Geita Gold, huku City ikipepetana na Kagera Sugar, KMC ikinyooshana na Singida BS.
Vibonde Polisi Tanzania waliopo mkiani kwa pointi 19 watakuwa na kibarua mbele ya Ihefu huku Ruvu Shooting wakikipiga na Azam.
Timu zitakazomaliza nafasi mbili za mwisho zitashuka moja kwa moja daraja kucheza championship msimu ujao.
Zile zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitacheza ligi yao mkondo wa kwanza kubaki ligi kuu na itakayopoteza itacheza na zile za Championship kujitetea kwenye play off.