Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni usiku wa maajabu Ulaya!

Man City Refa Ni usiku wa maajabu Ulaya!

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni kuombeana dua mbaya mwanzo mwisho. Hilo ndilo linalokwenda kutokea usiku wa leo, Jumanne huko kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hasa kwa wababe wa Kundi A la michuano hiyo.

Kwenye kundi hilo, Bayern Munich pekee ndiyo walioweka kibindoni tiketi ya kucheza hatua ya mtoano ya 16 bora, huku vigogo watatu Copenhagen, Galatasaray na Manchester United zote zikiwa na nafasi za kusonga mbele kwa kuzingatia matokeo ya mechi zao za mwisho zitakazopigwa usiku huu wa leo. Ni balaa hilo.

Man United itakuwa Old Trafford kuwakabili Bayern, ambao wataingia uwanjani bila ya kuwa na presha yoyote, huku shughuli nzito itakuwa huko uwanjani Parken, ambako Copenhagen na Galatarasay zitaulizana maswali zenyewe juu ya nani apenye.

Huko Old Trafford wao wanachoomba ni sare tu ipatikane huko Parken, huku wao wakiomba wapate ushindi wowote ule dhidi ya Bayern. Wataweza? Kuna maajabu?

Ngoja tuone kile kinachokwenda kutokea. Galatasaray wanaamini bahati yao juu ya uwanja wa Parken itaendelea, ambapo wanakumbuka mwaka 2000 waliichapa Arsenal kwenye fainali ya Kombe la UEFA na kunyakua ubingwa. Itakuwaje leo?

Msimamo wa kundi hilo unavyosoma, Bayern ina pointi 13, huku Copenhagen na Galatasaray kila moja ikiwa na pointi tano na Man United ina pointi nne.

Kundi B hakuna shughuli, sare yoyote kwenye mchezo wa PSV na Arsenal utaiwezesha timu hiyo ya Uholanzi iungane na The Guanners kwenye hatua ya mtoano, huku majaliwa ya Lens kuvuka ni wao kushinda nyumbani dhidi ya Sevilla, huku wakiomba chama ma Mikel Arteta lipate ushindi mkubwa huko Uholanzi. Arsenal wao wameshaweka mfukoni tiketi yao ya mtoano. Kwenye Kundi C, Real Madrid imeshavuka na bila ya shaka itaungana na Napoli kwenye hatua hiyo endapo kama watashinda au kutoa sare na Braga, ambao ndio wanaowatishia amani.

Mechi za mwisho za usiku wa leo zitakuwa za Kundi D, ambapo Inter Milan itakumbana na Real Madrid, ambazo zenyewe zimeshavuka, kila moja ikiwa na pointi 11, huku vita yao itakuwa ya kuongoza kundi. Timu nyingine kwenye kundi hilo, RB Salzburg na Benfica zenyewe zitakamilisha ratiba tu.

Kesho, Jumatano shughuli itakuwa kwenye Kundi F, ambako ukiwaweka kando Borussia Dortmund ambao tayari wameshafuzu hatua ya mtoano, kazi ipo kwa Paris Saint-Germain, Newcastle United na AC Milan zinazogombania nafasi moja iliyobaki.

Ni yaleyale tu ya kuombeana dua mbaya tu. PSG ili kufuzu itahitaji kushinda ugenini dhidi ya Dortmund, huku Newcastle na Milan, timu yoyote itakayoshinda kwenye mechi hiyo na endapo PSG itachapwa, basi watafuzu mtoano.

Kwenye kundi hilo, Dortmund ina pointi 10, PSG saba na Newcastle na Milan kila moja ikiwa na pointi tano, jambo linalofanya mechi zao za mwisho kuwa na upinzani mkali.

Kundi E hakuna shughuli, Atletico Madrid na Lazio zenyewe zimeshafuzu na vita yao itakuwa ya kuwania kuongoza kundi, huku Celtic na Fayenoord zitakamilisha ratiba.

Kwenye Kundi G, Manchester City na RB Leipzig zenyewe zimeshafuzu kwenye hatua ya mtoano, hivyo zitaingia uwanjani kucheza mechi zao za mwisho bila ya presha, zikimalizana na Crvena zvezda na Young Boys mtawalia.

Kazi ipo kwenye Kundi H, ukiwatoa Barcelona, ambao tayari wameshafuzu hatua ya mtoano, kasheshe limebaki kwa FC Porto na Shakhtar Donetsk. Barca imeshakusanya pointi 12, lakini Porto na Shakhtar kila moja ina pointi tisa na zitamenyana zenyewe usiku wa kesho huko Ulaya.

Sare yoyote itawabeba FC Porto kutokana na kuwa na mtaji mzuri wa mabao, hivyo Shakhtar wanahitaji ushindi tu wasonge mbele. Barca wao watamaliza na vibonde wa kundi, Antwerp.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live