Upweke sasa basi. Si kwamba nimepata mpenzi mpya, hapana. Kile kibaridi cha Dar es Salaam na maeneo mengine nchini kimeanza kupungua.
Kuna joto fulani limeanza kuja taratibu. Joto linaondoa upweke hasa kwa sisi ‘mabachela’. Watu ambao tumegoma kuuza uhuru wetu kwa watu wengine.
Hata hivyo, hili si joto la jua ama moto wa kuni. Ni joto la soka. Hili tunalielewa kwa wale tunaopenda kabumbu tu. Ule muda mwingi wa wikiendi ambao tulikua tunakaa bila kuwa na cha kufanya ulitushawishi sana kuwa mbali na Mungu. Shetani alikua kazini kwelikweli.
Anafahamu kabisa kuwa saa nyingi za wikiendi huwa tunayatumia kutazama burudani ya soka. Sasa haikuwepo. Akaongeza idadi ya dhambi na vishawishi . Hata hivyo, tumevishinda vyote. Mungu ni mwema.
Kwa Tanzania ilianzia pale Tanga wiki iliyopita. Ilikuwa ni Ngao ya Jamii. Kwa mara ya kwanza ilichezwa kwa mfumo wa shindano. Ni mabadiliko mazuri. Zilichezwa mechi nne kali pale Tanga kutoka kwa wababe wanne wa soka hapa nchini kwa sasa. Na mwisho wa siku Simba ikabeba ngao na kusepa nayo.
Wanatamba huko mitaani. Wamebeba ngao mbele ya mtani wao, Yanga ambaye kwa miaka miwili aliwatesa pale kwa Mkapa. Simba ikasema sasa unyonge basi. Mechi za Tanga zilifanya tuone namna wababe hawa walivyjiandaa na mechi za kimataifa pamoja na Ligi Kuu Bara.
Kuna baadhi ya watu wanasema ingekuwa aibu sana kwa Simba iliyokuwa Ulaya kufungwa na Yanga iliyoweka kambi Kigamboni kwenye mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii. Ulaya ingekuwa na maana gani sasa?
Lakini soka ni zaidi ya hapo. Unaweza kujiandaa ukiwa popote na ukashinda chochote. Mengine ni mbwembwe tu. Kwenye maandalizi unahitaji vifaa, uwanja mzuri wa mazoezi, makocha wazuri na wachezaji mahiri.
Hivi vitu unaweza kuwa navyo ukiwa Kigamboni, Manungu, Tabora au Tanga. Unahitaji nini zaidi? Hakuna.
Mwisho wa yote hata ukienda kufanya maandalizi Ulaya au Marekani, bado ligi unakuja kucheza Tanzania. Utakwenda sehemu ngumu kama Sokoine Mbeya, Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Lake Tanganyika, Kigoma na nyinginezo.
Hii ndio sababu Simba haikucheza kwa kiwango bora Mkwakwani, Tanga. Mechi zote mbili haikuwa katika ubora wake.
Hawakuwa wazuri kwenye kupiga pasi. Hawakuwa vizuri kwenye kupokonya mipira. Hawakuwa vizuri kwenye kutengeneza nafasi. Ndio sababu mechi zote mbili za ngao hawakufunga bao lolote.
Hii ndiyo tofauti ya Ulaya na Bongo. Iliwahi kuikuta pia Yanga msimu wa 2013/14. Nao waliweka kambi Uturuki. Waliporudi tu Bongo mechi yao ya kwanza ikawa pale Mkwakwani dhidi ya Coastal Union. Wakacheza ovyo. Wakapata suluhu mbele ya Wagosi wa Kaya Waliokuwepo hapohapo Tanga wakijiandaa. Watu wakaicheka sana Yanga.
Kambi ya Uturuki haikuwasaidia chochote cha maana. Msimu ulimalizika kwa Azam FC iliyoweka kambi yake Chamazi ikatwaa ubingwa.
Tuachane na mambo ya kambi kwanza. Nilitaka kuzungumza kuhusu usajili wa Simba na Yanga mpaka sasa. Timu zote mbili zimefanya usajili kwa umakini. Simba baada ya kukosa mataji kwa misimu miwili mfululizo, imefanya usajili kabambe.
Kuna wachezaji wameingia moja kwa moja kwenye mfumo wa timu taratibu. Lakini mpaka sasa Che Fondoh Marlone ndiye usajili bora zaidi.
Achana na makosa aliyofanya pale Manungu juzi, ukweli ni kwamba jamaa ni kitasa kweli. kuumia kwa Henok Inonga kumemfanya awe na mzigo mkubwa sana.
Yule Leandre Onana ni mchezaji mahiri pia. Japo anapata shida kuzoea viwanja vigumu. Ila kwa mechi za Mkapa atasumbua sana. Fabrice Ngoma hana mjadala.
Luis Miquissone hajawa fiti vya kutosha lakini ametuonyesha pale Manungu kuwa ana uwezo wa kufanya nini. Ile pasi yake kwa Clatous Chama haipigwi na kila mchezaji. Ni mafundi tu.
Kwa kifupi Simba imetatua tatizo lake la msingi la msimu uliopita. Ilikosa upana wa kikosi. Walioanza walikuwa bora, lakini waliokaa nje walikua ovyo. Msimu huu wanaanza na watu wa maana na nje kunabaki na silaha haswa.
Hebu fikiria ameanza Kibu Denis, nje yupo Miquissone. Ameanza Onana nje yupo Aubin Kramo na Saido Ntibazonkiza. Ameanza Baleke nje wapo Bocco na Phiri. Hapo sijamtaja Shaban Chilunda. Kwa upande wa Yanga wamefanya usajili muhimu.
Ameondoka Djuma Shaban, wamemleta Yao Kouassi. Yupo fiti, anashambulia na kukaba kama ametiwa ndimu. Wamemwongeza pia Gift Fred kwenye ulinzi. Katikati ameondoka Yannick Bangala wamemleta Pacome Zouzoua. Fundi haswa. Vipi kuhusu Maxi Nzingeli? Winga wa kisasa. Anafanya vitu ambayo Bernard Morrison na Tuisila Kisinda walishindwa. Ni roho ya Yanga.
Wasiwasi ni pale alipoondoka Fiston Mayele. Sidhani kama Hafiz Konkon ataweza kuvaa viatu vyake.