Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni muda wa lala salama EPL

Arsenal Ghs Ni muda wa lala salama EPL

Sun, 7 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pointi moja tu imezitofautisha Manchester City na Arsenal kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu. Vijana wa Pep Guardiola, Man City wapo kileleni na pointi zao 79, wakati jeshi la Mikel Arteta lipo namba mbili na pointi 78.

Man City imecheza mechi 33, Arsenal imecheza 34. Leo hii, Jumamosi Man City itasawazisha kiporo chake ili kuwa idadi sawa ya mechi na Arsenal, wakati itakaposhuka uwanjani Etihad kukipiga na Leeds United.

Dakika 90 za mchezo huo, zinaweza kuwa na hadithi mbaya au nzuri kwa Arsenal. Kama Man City itashinda, basi pengo la pointi litapanga na kuwa nne, hapo hata Arsenal washinda mchezo wao wa kesho, Jumapili, hawataweza kurudi tena kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo. Na hii itakuwa imemaliza zama zao za kutesa kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo, ambapo walikaa kwa muda mrefu msimu huu. Itakuwaje?

Rekodi za Man City na Leeds United kwenye mechi zao za Ligi Kuu England hakuna mnyonge. Mara 19 walizokutana, kila moja imeshinda saba huku mechi tano zilimalizika kwa sare. Man City imeshinda tatu nyumbani na nne ugenini, wakati Leeds yenyewe imeshinda tano nyumbani na mbili ugenini. Lakini, mechi tano za mwisho, Man City imeshinda nne.

Arsenal wao msala wao wa kesho watakuwa ugenini kukipiga na Newcastle United. Mara 55 ambazo wamekutana kwenye Ligi Kuu England, sare ni 11 na Arsenal imeshinda 33, mara 21 nyumbani na 12 ugenini, huku Newcastle ikishinda 11, saba nyumbani na nne ugenini. Lakini, Newcastle ya msimu huu imekuwa moto zaidi, huku mechi hiyo ikiwa na umuhimu mkubwa kwa Arsenal katika mbio zao za ubingwa, wakiamini chochote kinaweza kutokea kwa Man City, hivyo hawataki kujiweka mbalimbali sana kipointi.

Chelsea kinyonge sana nayo itashuka uwanjani leo, Jumamosi itakapokwenda kuwakabili Bournemouth. Miamba hiyo ya Stamford Bridge, The Blues haijashinda mechi yoyote tangu ilianza kuwa chini ya kocha Frank Lampard. Rekodi zao dhidi ya Bournemouth, wamekutana mara 11 kwenye ligi, mechi moja ilimalizika kwa sare, huku Chelsea ikishinda sita, tatu nyumbani na tatu ugenini, wakati Bournemouth imeshinda nne, moja nyumbani, tatu ugenini.

Tottenham Hotspur baada ya kuteseka katika mchezo uliopita dhidi ya Liverpool watakuwa nyumbani kukipiga na wababe wenzao wa London, Crystal Palace. Miamba hiyo imekutana mara 27 kwenye Ligi Kuu, ambapo Spurs imeshinda 16, nane ikiwa nyumbani na nane nyingine ugenini, huku Palace imeshinda nne tu, tatu nyumbani na moja ugenini. Kuna mechi saba baina yao zilimalizika kwa sare.

Shughuli nyingine pevu ya ligi hiyo itakuwa baina ya Wolves na Aston Villa, ambapo mara 15 walizokutana kwenye ligi hiyo, kila moja imeshinda mara tano, huku mechi nyingine tano zikimalizika kwa sare. Kwenye mechi hizo, Wolves imeshinda mbili nyumbani na tatu ugenini, wakati Aston Villa imeshinda moja nyumbani na nne ugenini. Patamu hapo.

Jumamosi itamalizwa kwa kipute cha kibabe huko Anfield, wakati Liverpool itakapoikaribisha Brentford. Mechi hiyo ni ngumu kwelikweli kutokana na timu hizo mbili kufukuzia nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Kwenye Ligi Kuu England, Liverpool na Brentford zimekutana mara tatu, na kila moja imeshinda mara moja, huku mechi moja ikimalizika kwa sare na uzuri wake katika mechi hizo, hakuna timu iliyoshinda ugenini. Itakuwaje sasa?

Kwa kesho, ukiweka kando kipute cha Newcastle United na Arsenal, shughuli nyingine pevu itakuwa baina ya West Ham United na Manchester United. Mzigo utakuwa London Stadium. Kwenye Ligi Kuu, zimekutana mara 53, West Ham ikishinda saba, tano nyumbani na mbili ugenini - huku mechi 13 zikimalizika kwa sare na Man United ilishinda 33, mara 22 ikiwa nyuymbani na 11 ugenini.

Kesho kutwa Jumatatu kutakuwa na mechi tatu, Fulham watacheza na Leicester City huko Craven Cottage, wakati Brighton watakipiga na Everton uwanjani Amex na Nottingham Forest wataaliza ubishi na Southampton uwanjani City Ground.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live