Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni kweli ligi yetu iko nafasi ya tano Afrika?

Saido Penati Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kampuni ya Utafiti za Kimataifa na Historia kwenye Soka (IFFHS), wikiendi iliyopita imeteka mitandao. Imeibua mjadala. Kwa mujibu wa utafiti wao Ligi Kuu Bara inashika nafasi ya tano Afrika.

Kinacholeta mjadala zaidi ni kwamba vigezo walivyotumia havijawekwa wazi. Kwa namna tunavyoifahamu ligi yetu na upungufu wetu wengi tumeshangaa kuona tunaipata nafasi hyo. IFFHS wamekuwa na utafiti mwingi ambao huibua mjadala.

Kwa mfano utafiti wao pia umeonyesha kuwa Ligi Kuu ya Brazil ndiyo ligi bora Kwa sasa duniani. Sio Ligi Kuu ya England (EPL), sio Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), sio Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Ngumu sana kwa mtu wa soka kuipokea hii.

Utafiti wao unaonyesha klabu bora ni CR Flamingo kutoka Brazil na nafasi ya pili ni SE Palmeiras ya Brazil pia. Sio Real Madrid, sio Bayern Munich wala sio Manchester United. Vigezo gani wametumia? Mimi na wewe hatuna majibu. Ni kwenye kutazama mafanikio ya klabu zetu na namna ligi yetu inavyoendeshwa tunaweza kushika nafasi ya tano Afrika? Wapo watakaosema ndiyo. Wapo watakaosema hapana. Lakini, utafiti siku zote huwa unapingwa na utafiti. Haupingwi na hisia. Haupingwi na mihemko.

Nini kitakuwa kimeipa thamani ligi yetu? Labda ni Azam TV. Pamoja na changamoto zetu lakini tusisahau mechi zote za ligi yetu zinaonyeshwa na Azam TV. Sio kila taifa limepata bahati hii. Azam TV wameongeza thamani kubwa sana kwenye mpira wetu. Siku za nyuma kidogo haya mambo hayakuwepo.

Mechi kubwa tu ndiyo zilikuwa zinapewa kipaumbele. Siku hizi mechi ya Ihefu dhidi ya Tanzania Prisons inaonyeshwa moja kwa moja. Siku ya mechi ya Namungo dhidi Kagera Sugar utaitazama moja kwa moja kupitia Azam TV. Sio jambo dogo. Ni hatua kubwa sana kwenye kuitangaza ligi yetu.

Kwa sababu IFFHS hawajasema vigezo walivyotumia kuiweka ligi yetu nafasi ya tano Afrika, huenda sababu ya ligi kuonekana kila kona ya dunia nayo ikawa imechangia. Ukitazama majirani zetu kama Kenya na Uganda wao bado soka lao linasuasua.

Hakuna msisimko wala hamasa ya kutosha. Nguvu kubwa bado iko kwenye ligi za Ulaya. Watu wanatazama zaidi Ligi Kuu ya England (EPL). Watu wanatazama zaidi mechi za Arsenal na Manchester United. Ni tofauti sana na hapa kwetu.

Hata kama nafasi ya tano Afrika inaonekana ni ya juu sana, lakini tusidharau ligi yetu. Kuna namna tumekua sana. Bado hatuna matokeo mazuri kwenye michuano mikubwa ya CAF, lakini haiondoi ukweli kuwa ligi yetu imepiga hatua nyingi tu za ukuaji. Nilikuwa natazama ukuaji wa ligi yetu kwenye mitandao ya kijamii.

Kuna hatua kubwa sana tumepiga huku. Katika klabu 10 bora Afrika zenye wafuasi wengi, Simba iko nafasi ya pili. Tanzania ina timu nne kwenye orodha hiyo. Hili sio jambo dogo. Kuna namna tumeiteka Afrika mitandaoni. Kuna namna watu wanaanza sasa kutufuatilia.

Hata kama bado kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatufanyi vizuri kama nchi, lakini kuna namna mpira wetu umekua kwa sasa. Huwezi kulinganisha na miaka 10 iliyopita.

Ukitazama mwenendo wetu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika nako pia bado tunasuasua, lakini kuna vitu vingi pia tumeimarika. Utafiti huu haupaswi kupuuzwa. Unapaswa kutupa hamasa ya kuendelea kujiimarisha zaidi. Unapaswa kutupa nguvu ya kurekebisha kasoro zetu. Moja kati ya vitu vizuri pia kwenye mpira wetu ni hamasa.

Pale Kenya zamani Mashemeji Derby Gor Mahia dhidi ya AFC Leopards ilikuwa inajaza watu uwanjani, lakini siku hizi hamna kitu. Ni tofauti sana na Tanzania. Hata mechi ya KMC dhidi ya Ruvu Shooting watu wanaenda uwanjani.

Watanzania wengi wanapenda zaidi soka la ndani. Pamoja na changamoto zake zote, lakini soka la ndani lina nguvu sana nchini. IFFHS hawajaweka vigezo vyote wanavyotumia kuweka ubora wa ligi na klabu zao duniani, lakini huenda hii ikawa ni moja ya sababu zinazoipeleka Tanzania nafasi ya tano Afrika.

Ukitazama Simba Day na Siku ya Wananchi unaweza kudhani ni fainali ya Kombe la Dunia. Ushawishi ni mkubwa Tanzania. Mashabiki wengi hujitokeza. Hili sio jambo dogo kwa sababu biashara kubwa ya soka iko kwenye wingi wa mashabiki.

Kuna namna Afrika na Dunia inaitambua Ligi ya Tanzania kupitia nguvu ya mashabiki wa soka tuliyo nayo. Labda tukichanganya mafanikio yote bado nafasi ya tano Afrika ni kubwa kwetu, lakini haiondoi ukweli kuwa ligi yetu inazidi kukua. Inazidi kuingiza pesa nyingi. Inazidi pia kuvutia wachezaji wengi vijana kutoka maeneo yaliyoendelea kama Afrika Magharibi. Kuna hatua tunapiga kwenda mbele.

Ni kweli ligi yetu inashika nafasi ya Tano Afrika? Kwa kutazama matokeo ya uwanjani kwenye michuano ya Afrika pekee, jibu litakuwa ni HAPANA. Kwa kutazama uwekezaji kwenye miundombinu jibu litakuwa pia ni HAPANA.

Lakini nguvu ya mitandao ya kijamii, hamasa ya mashabiki uwanjani na thamani kubwa tunayoipata kutokana na ligi yetu kuonyeshwa moja kwa moja na Azam TV, jibu ni KWELI. Tuheshimu utafiti lakini uende ukatupe nguvu ya kujipanga vizuri ili tuiboreshe vizuri.

Chanzo: Mwanaspoti