Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni kweli Simba hawaupigi mwingi?

Simba Yaapa Kuwachapa Power Dynamos.jpeg Ni kweli Simba hawaupigi mwingi?

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tayari Simba imeshiriki mashindano matatu msimu huu. Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba haijapoteza mchezo wowote katika michuano hiyo. Simba ndiyo mabingwa wa Ngao ya Jamiii.

Simba imepata alama tisa kwenye mechi tatu ilizocheza hadi sasa. Simba imefuzu kwenda hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni kweli Simba haiupigi mwingi? Hebu nipe na wewe mtazamo wako juu ya namna Simba inavyocheza.

Binafsi napatwa na wakati kusema kuwa Simba hawaupigi mwingi. Napata shida sana. Mpaka mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu Bara unakamilika, Simba ndiyo timu iliyopiga pasi nyingi kuliko timu nyingine yotote.

Kwa mujibu wa mtandao wa LIVEBALL, Simba imepiga pasi 1300, Yanga 1196, Azam 940. Hizi ndizo timu zenye pasi nyingi mpaka sasa kwenye ligi yetu. Lakini bado kuna kelele nyingi juu ya Simba kutoupiga mwingi. Bado kelele ni nyingi sana kuwa Simba haichezi vizuri.

Mimi na wewe wote tunaitazama Simba. Mimi na wewe wote tunaifuatilia. Kama una maoni yotote tafadhali niandikie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Je, ni kweli Simba hawaupigi mwingi?

Mchezo wa soka ni mchezo wa wazi. Kila mmoja anaona. Hakuna timu isiyoupiga mwingi inayoweza kushinda taji lolote kwenye mchezo huu. Hakuna.

Simba imetwaa Ngao ya Jamii mbele ya Singida Fountain Gate, Azam FC na Yanga. Haiwezi kuwa timu mbovu. Simba haijapoteza mechi yoyote ya ligi kwenye mechi tatu ilizocheza. Haiwezi kuwa timu mbovu.

Hakuna timu mbovu duniani inayoweza kushinda mechi tatu za ligi mfululizo. Haipo. Simba imefuzu kwa hatua ya makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hakuna timu mbovu inayoweza kufika hatua hii. Kumbuka imeichukua Yanga miaka 25 kufikia hatua hii msimu huu. Sio hatua nyepesi. Ingekuwa rahisi Yanga ingekuwa inafika kila msimu. Nilitazama kwa makini sana mechi ya Simba na Coastal Union, pamoja na ushindi wa Simba wa mabao 3-0, Simba ilimaliza pia mechi ikiwa na umiliki wa mpira wa asilimia 87. Baada ya mechi kelele zilikuwa nyingi sana kuwa Simba hawakuupiga mwingi. Kwani kuupiga mwingi ni nini? Labda hapa ndipo sielewi.

Mwenzenu nilidhani kuupiga mwingi ni kushinda mataji, lakini baada ya Simba kutwaa Ngao ya Jamii bado nikasikia pia kuwa hawaupigi mwingi. Baada ya kushinda mechi tatu mfululizo za ligi nilidhani kuwa ndiyo kuupiga mwingi kumbe hata huko pia sio? Tafadhali kwa yeyote anayejua maana ya kuupiga mwingi naomba anijuze kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Ni kweli Simba ya misimu minne nyuma sio hii. Bado ile ya kina Meddie Kagere, Larry Bwalya, Chriss Mugalu, Clatous Chama yule na Luís Miquissone yule bado haijarejea, lakini siamini kama Simba haiupigi mwingi. Bado boli linatembea. Bado Simba inazidi kusonga mbele.

Kufika hatua ya makundi bila kushinda mechi hata moja sio jambo mashabiki wanalopenda kuona kwa timu yao, lakini hatua kama hizi cha msingi huwa ni kusonga mbele. Kwa namna yoyote timu inapaswa kusonga mbele.

Tatizo la nchi hii watu wanapenda sana kulinganisha Simba na Yanga. Hapa kinachosumbua ni kuona Yanga wana udambwidambwi mwingi uwanjani. Ni kuona Pacôme Zouzoua anavuruga sana pale dimbani. Ni kuona Maxi Nzegeli amekuwa staa mkubwa nchini kwa sasa.

Haya mambo yanawatia sana unyonge mashabiki wa Simba. Kuna muda wanatamani Simba icheze kama Yanga. My friends, mpira hauko hivyo. Simba ina njia zake kutokana na wachezaji wake. Yanga ina njia zake kutokanana na wachezaji wake. Sioni sababu yotote ya Simba kuwa wanyonge hadi sasa. Sioni sababu yotote ya wao kuwa wapole. Bado naamini Simba wanaupiga mwingi na msimu huu wameongezeka kidogo ubora kuliko walivyokuwa uliopita. Bado nawaona kama timu inayoweza kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita. Bado nawaona kama timu inayoweza kufika hatua za juu zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika kuliko msimu uliopita. Pale Simba kuna watu, sema tu mashabiki wameanza kuwa na mcheche.

Labda Simba bado hawachezi kama Yanga. Labda bado Simba haichezi kama Azam, lakini Simba wana timu nzuri. Imeongeza wachezaji wengi wenye ubora. Yule Che Malone sio wa kitoto. Ni kitasa hasa wa kuwafikisha Simba mbali.

Yule Fabrice Ngoma ni suala la muda tu hakusajiliwa kwa bahati mbaya. Willy Onana watu wengi wameanza kelele, lakini atakuja tu kuwaziba midomo. Hata Chama aliporejea alianza kwa kuyumba, lakini sasa amerejea kwenye ubora wake.

Miquissone atarejea kwenye ubora wake. Moto wake kila mtu anaujua. Sioni sababu yoyote ya wana Simba kutembea kichwa chini. Pamoja na hayo yote, bado Simba kapiga pasi nyingi za Ligi Kuu kuliko timu nyingine yoyote.

Simba katinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba ndiyo mabingwa wa Ngao ya Jamii. Ulitaka Simba wafanye nini zaidi? Hakuna. Wanasimba acheni unyonge mna timu nzuri ni sula la muda tu makubwa yanakuja.

Hakuna timu mbovu inayoweza kwenda makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kama Simba ni mbovu mbona haifungwi? Kama Simba ni mbovu iliwezaje kutwaa taji la Ngao ya Jamii mbele ya Yanga?

Kama Simba ni mbovu imeweza vipi kushinda mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu? Kama una majibu ya maswali haya matatu tafadhali naomba unitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: