Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni akili ya Robertinho dhidi ya Yanga iliyochangamka

Robertinho Kufanya Mabadiliko Ya Kikosi Dhidi Ya Al Ahly Ni akili ya Robertinho dhidi ya Yanga iliyochangamka

Sun, 5 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dabi ya Kariakoo. Mchezo wenye hadhi na thamani kubwa zaidi nchini unachezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ni Simba dhidi ya Yanga. Huu ndio mchezo mkubwa zaidi kwenye ukanda huu wa Cecafa. Kila Simba inapocheza na Yanga mashabiki kila kona hufuatilia. Ni mchezo mkubwa. Mchezo wa viwango.

Ni mchezo pekee wa Ligi Kuu Bara unaoweza kujaza Uwanja wa Mkapa. Hakuna mwingine. Hakuna unaokaribia. Kwanini? Kwa sababu hizi ndizo timu kubwa zaidi nchini. Timu zinazopendwa zaidi.

Ni mechi ambayo huzungumzwa kwa muda mrefu kabla ya kuchezwa. Tambo za mashabiki huwa ni nyingi. Hata hivyo mwisho wa siku dakika 90 huzungumza zaidi.

Uzuri ni kwamba mechi moja ya dabi ikimalizika hutengeneza hamu ya dabi nyingine. Ni kama Simba walivyotwaa Ngao ya Jamii pale Tanga papo hapo mashabiki wa Yanga wakaanza kutamba kuwa tutakutana kwenye Ligi Kuu. Ni mchezo wa kipekee. Unagusa maisha na hisia za watu wengi. Ni mechi ambayo huleta upatanisho wa waliokosana. Iwe mashabiki au viongozi wa timu hizo humaliza tofauti zao na kuwa kitu kimoja ili kushinda dabi.

Hapa karibuni Yanga walikuwa na Kocha Nasrredine Nabi. Mbali na rekodi zake kadhaa, Yanga yake ilifanikiwa kuitesa Simba. Kwa muda wote wa miaka miwili aliokaa hapa nchini, Nabi alipoteza dabi mbili tu kati ya nyingi alizocheza na Simba.

Aliwanyanyasa kwa kadri alivyoona inafaa. Simba ilikuwa ikifurukuta sana inapata sare, ila vinginevyo ni kipigo. Hizo ndizo zama za Nabi.

Baada ya kuitesa Simba kwa muda mrefu, akaja huyu Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Huyu naye amekuwa na mbinu bora dhidi ya Yanga kila akikutana nao. Alianza kuwaonea tangu akiwa Rayon Sports ya Rwanda. Akawanyanyasa akiwa na Vipers ya Uganda. Alipotua Simba akamaliza utemi wa Nabi. Akawafunga 2-0 kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita.  Huwa inatokea anakuja kocha mmoja na kuwa na mbinu za kuikamata dabi zaidi. Robertinho ameonyesha ana mbinu nzuri za kuikamata Yanga.  Nani aliwaza kama ile Simba ya kina Kibu Denis na Onyango ingeweza kuisumbua Yanga msimu uliopita? Hakuna. Simba ilikuwa na kikosi cha kuunga unga. Yanga walikuwa wa moto. Kwenye dabi mambo yakawa tofauti.

Kwa leo tunakwenda kwenye dabi yenye sura ya tofauti kabisa. Simba ya Roberinho iko vizuri kimbinu wakati Yanga ya Miguel Gamondi imechangamka. Wachezaji wa Yanga wanacheza kama hakuna kesho. Wanajitoa kwelikweli. Wakipoteza mpira wanakaba kwa pamoja kama mbweha. Hawawapi wapinzani nafasi ya kucheza. Ndio Yanga ya Gamondi. Inashambulia kwa kasi kama nyuki ambao wanahisi kuvamiwa. Wanatafuta bao muda wote wa mchezo. Kila mchezaji anajituma. Ni Yanga iliyochangamka kwelikweli.

Robertinho atafanya nini mbele ya Yanga hii? Ni jambo la kusubiri na kuona. Simba yake iko vizuri kwenye mbinu. Tuliona namna ilivyobishana na Al Ahly hapa Dar na pale Cairo.  Kuna watu waliamini Simba itapigwa bao nyingi na Al Ahly pale Cairo. Kilichotokea, Robertinho aliifunga timu. Walishambuliwa sana lakini waliweza kuituliza presha. Wakashambulia kwa kushtukiza na kupata bao. Ikawa vita ya mbinu dhidi ya ubora. Uzuri wa Simba ya Robertinho inafunga mabao. Ubaya wa Simba yake inaruhusu sana mabao. Msimu huu katika mechi 10 za mashindano yote imeruhusu mabao katika michezo minane.

Ni wazi kuwa bado kuna shida katika namna ya kuzuia, ila kwa mbinu anaweza kuwa vizuri. Acha tuone Yanga ya Gamondi iliyochangamka itaweza kumaliza utawala wa Robertinho mbele yao?

Mwisho wa yote niseme jambo juu ya hamasa za kuelekea dabi hii. Nimekerwa na kitu kimoja. Kuna namna timu mwenyeji inaachiwa kazi ya kufanya hamasa peke yake. Pengine huu utaratibu wa mwenyeji kuchukua mapato yote umeleta hili jambo. Siyo zuri sana kwa dabi. Dabi ni mechi ya timu zote mbili. Zote zinapaswa kufanya hamasa bila kujali nani anachukua mapato. 

Ni aibu kuona leo kiingilio cha chini cha dabi bado ni Sh5,000. Yaani sawa na mechi ya Simba na Ihefu. Sawa na mechi ya Yanga na JKT Tanzania. Ni aibu.

Tunashusha thamani ya dabi kwa kupunguza msisimko kisa mwenyeji anachukua mapato yote.  Miaka ya nyuma kiingilio cha chini kwenye dabi kilikuwa Sh7,000 lakini sasa tumerudi nyuma. Ni jambo la kujitafakari upya. Kuna mahali kitu hakipo sawa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live