Huenda umesahau, lakini Desemba 22 timu za Simba na Yanga za Vijana U20 zilivaana katika pambano la Kariakoo Derby kwa Ligi Kuu ya Vijana na ikashuhudiwa Wekundu wakipigwa mabao 4-0, sasa unaambiwa timu hizo zinarudiana tena wikiendi hii!
Katika mchezo wa kwanza mabao ya Yanga yalifungwa na kiungo mpya Shekhan Khamis kutoka JKU, Willyson Christopher, Ahmed Fredrick na Ramadhani Hemed na keshokutwa Simba itakuwa na kazi ya kulipa kisasi kwenye mechi hiyo ya Kundi A linaloongozwa na Azam FC yenye pointi 17 baada ye mechi tisa.
Wagosi wa Kaya, Coastal Union ndio inayofuata kwenye msimamo wa kundi hilio ikiwa na pointi 13, kisha Yanga yenye pointi 11, huku Ihefu, Tanzania Prison na Simba kila moja imekusanya pointi nane. Namungo, KMC ndizo zinazoburuza mkia wa kundi hilo.
Katika mechi iliyopigwa juzi kwenye ligi hiyo, Yanga ilitoka sare ya bila kufungana na KMC, huku Simba akipata ushindi wa pili kwa msimu huu kwa kuifunga Namungo kwa mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa Simba, Mohamed Mulishona ‘Xavi’ alisema wamepata muda mwingi wa kufanya maandalizi na anaamini timu hiyo itapata ushindi.
“Mechi ya raundi ya kwanza watani wetu walikuwa bora na tukafungwa mabao yale na sababu ya kupoteza kwa mchezo ule kulitokana na maandalizi hafifu, raundi hii tumepata muda mwingi wa kufanya mazoezi na timu na ushindi wa juzi dhidi ya Namungo umeongeza morali zaidi.”