Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Pablo, Simba yaweka rekodi ya ajabu

UPDATE SIMBA Simba yaweka rekodi ya ajabu

Fri, 28 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba haijawahi kucheza mechi tatu mfululizo bila kufunga bao. Pia haijawahi kuanza mechi bila straika, lakini Simba ya Pablo Franco jana Jumatano ilishuka Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba kukipiga na Kagera Sugar bila ya kuwa na straika yeyote na kuchapwa bao 1-0.

Pablo aliamua kuwapiga benchi mastraika wake wote akiwamo kinara wa mabao wa kikosi hicho kwa msimu huu, Meddie Kagere na nahodha John Bocco, akianza na viungo watupu eneo la mbele na kujikuta ikicheza kwa dakika 270 bila kupata bao na bila ushindi katika Ligi Kuu Bara.

Akiwa kwenye kikosi hicho cha Simba kwa miezi miwili na nusu tangu alipotua nchini Novemba 10 mwaka jana, Pablo ameonyesha hajapata kikosi cha kwanza kutokana na kubadili wachezaji karibu kwenye kila mechi na jana aliwashtua mashabiki wa miamba hiyo ya Msimbazi kwa kuwaacha nje washambuliaji wote na kujaza viungo uwanjani.

Kocha huyo aliwaanzisha Sadio Kanoute, Mzamiru Yasin, Ousmane Sakho, Bernard Morrison, Rally Bwalya na Clatous Chama, lakini wachezaji hao walipoteza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Pablo aliamua kujisahisha kwa kuwaingiza washambuliaji Kagere, Bocco, Yusuph Mhilu na viungo wengine Erasto Nyoni na Hassan Dilunga, lakini hayakusaidia kitu licha ya kuipa presha Kagera ambayo ilishakuwa mbele kwa bao lililofungwa dakika ya 71.

Bao la Hamis Kiiza ‘Diego’, aliyewahi kuichezea Simba, ambaye aliingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Ally Ramadhan lilitosha kuamua matokeo ya mchezo huo, huku shambulizi hilo lililozaa bao lilitokea kwa Chama kupokonywa mpira na Ufudu, kabla ya kugongwa pasi kama nne na kisha mpira kupelekwa kushoto, ambako ilitokea pasi ya mwisho kwa mfungaji aliyepiga mpira wa chini kwa guu la kushoto kumpita Aishi Manula, aliyekuwa ametoka langoni kumkabili.

Hata hivyo, Kiiza hajamaliza mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi. Hicho kilikuwa kipigo cha pili kwa Simba katika mechi tatu zilizopita, nyingine ikiwa ni sare, ikianza kwa kuchapwa na Mbeya City 1-0, ikatoka sare 0-0 na Mtibwa Sugar na kufanya wabaki na pointi zao 25 katika mechi 13. Pointi 10 nyuma ya mahasimu wao vinara kwenye ligi, Yanga huku zote zikiwa zimecheza michezo sawa. Yanga imekusanya pointi 35.

Related Simba, Kagera hakuna kisingizio, Chama aongeza mzuka Kizza aiangamiza Simba Uwanja wampa mzuka Pablo Banda amtabiria makubwa ChamaMechi hiyo ya jana iklikuwa ni kiporo baada ya Desemba 18 kushindwa kuchezwa kutokana na kilichoelezwa kuwa, wachezaji 16 wa Simba walikuwa wakiumwa mafua makali na kifua na mchezo kupangwa kupigwa jana.

Ushindi huo wa Kagera umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 16 baada ya mechi 13 na kuchupa kwa nafasi mbili kutoka ya 11 hadi ya tisa.

Kocha wa Kagera, Francis Baraza alisema baada ya kugundua ni ngumu kupata bao kwa jinsi Simba ilivyojaza viungo alizungumza na wachezaji wake kipindi cha pili kuingia wachezaji wenye kasi kuwakimbiza mabeki wa Simba na kufanikiwa.

WASIKIE HAWA

Nyota wa zamani wa Simba, aliyewahi kuzinoa Kagera Sugar na JKT Tanzania, Mrage Kabange alisema presha ya matokeo ndio inayowasumbua Simba kwa sasa huku akimuunga mkono kocha Pablo kuwapiga benchi mastraika wote kwa jana.

“Hawachezi vibaya lakini nafikiri wachezaji wanaathiriwa na presha kubwa ya kutaka ushindi jambo ambalo wanatakiwa kuliangalia kwani wakiendelea hivyo wanaweza kufanya vibaya zaidi.

“Kwa upande wa kocha kuwaweka nje washambuliaji wote na kuwaanzisha viungo wengi katika mchezo huo naona ni sawa, kwani mastraika wake hawajafunga karibu mechi nyingi zilizopita,” alisema Kabange huku beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kitendo cha kocha kuwaweka benchi mastraika wake katika mchezo huo ni kutokana na kuhangaika kutafuta muunganiko wa kikosi hicho.

“Bado kocha anahangaika kutafuta muunganiko wa timu na ndio maana hadi sasa hana kikosi cha kwanza kama ilivyo kwa watani zao wa jadi Yanga. Leo (jana) kajaribu kuweka viungo wengi kwa sababu aliona hali ya uwanja ni rafiki kwa timu yake kucheza mpira, lakini pia mechi mbili zilizopita alijaribu kuwaanzisha mastraika wawili katika kujaribu kupata muunganiko wao lakini haujakubali hivyo ndio maana anajaribu jaribu kila wakati kwa sababu bado hajawajua vizuri wachezaji wake ,”alisema Pawasa na kuongeza;

“Jambo ambalo wachezaji wa Simba wanatakiwa kufanya kwa sasa ni kushusha presHa, wasicheze kwa presha ya mashabiki ambao wanataka matokeo ya haraka kwa sasa, Watulie watafute mbinu mbadala kuhakikisha wanashinda mechi yoyote ili kurudi kwenye ubora wao.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz