Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Mayele na Saido tu msimu huu

Mayelle Pic Ni Mayele na Saido tu msimu huu

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pazia la Ligi Kuu Bara linafungwa rasmi leo kwa timu 16 zilizoshiriki msimu huu zitakaposhuka viwanja tofauti kuanzia saa 9:30 alasiri ili kukamilisha raundi ya mwisho ya ligi hiyo, huku macho na masikio ya mashabiki wa soka yakielekezwa jijini Mbeya na Dar es Salaam.

Simba ipo Uwanja wa Uhuru kuikaribisha Coastal Union, wakati Yanga itakuwa ugenini Uwanja wa Sokoine, kuvaana na Tanzania Prisons, huku mashabiki wakisikilizia Mfungaji Bora wa msimu huu kutokea kwenye viwanja hivyo kutokana na vita ya Saido Ntibazonkiza na Fiston Mayele.

Ndio kama ilivyowahi kutokea kwenye misimu miwili mfululizo iliyopita kwa Mfungaji Bora kufahamika mechi za mwisho kwa John Bocco kumpiku Chris Mugalu (2020-2021) na George Mpole kumzidi ujanja Mayele (2021-2022), ndivyo hali ilivyo safari hii kwa nyota hao wa Simba na Yanga.

Mayele ndiye kinara wa mabao akiwa na 16, huku Ntibazonkiza akifunga 15 na yeyote kati yao leo akitupia mabao zaidi badi atamaliza msimu kibabe.

Mayele aliyebeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akimaliza na mabao saba akiiwezesha Yanga kucheza fainali ya kwanza ya CAF na leo anatafuta kusahihisha makosa ya msimu uliopita alipozidiwa na Mpole aliyekuwa Geita aliyemaliza na 17, moja zaidi na aliyokuwa nayo.

Mabao matano aliyofunga Saido kwenye mechi iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania imemfanya afikishe mabao 15 na kumshtua Mkongoman huyo aliyeukosa mchezo uliopita wa Yanga dhidi ya Mbeya City ulioisha kwa sare ya 3-3 na leo atakuwa na kazi mbili kuvunja mwiko wa kuifunga Prisons, lakini kupambana kumaliza kama kinara mbele ya Saido ambaye anapewa nafasi kubwa ya kutwaa kiatu.

Saido anapewa nafasi hiyo kutokana na rekodi iliyopo kwa Simba mbele ya Coastal, lakini uwezo wa nyota huyo kufunga mabao na kuweka rekodi kwa sasa kuhusika na mabao 27 akifunga 15 na kuasisti 12.

Hsta hivyo, nyota wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Willy Martin ‘Gari Kubwa’ kufunguka kwamba pamoja na vita nzito lakini Mayele ana uwezo wa kupambania tuzo hiyo kutokana na rekodi aliyoweka msimu huu.

Alisema nyota huyo amekuwa rafiki sana wa nyavu bila kujali uwanja wa nyumbani au ugenini na kwamba anajua namna ya kucheza na mabeki wa timu pinzani hivyo anayo nafasi kubwa.

“Juzi sikumuona uwanjani wakati Yanga anacheza na Mbeya City, hivyo kama kesho (leo) atacheza dhidi ya Prisons anaweza kufunga mabao hivyo naona kiatu msimu huu kikienda kwa Mayele,”

“Ila kwa mipango waliyonayo Simba kitimu inambeba Ntibazonkiza hivyo yeyote atakayepanga vyema karata zake anaweza kuchukua tuzo, naona vita ni kali sana,” alisema Nahodha huyo wa Yanga, Simba, Majimaji na Ushirika.

Hadi sasa Yanga ndio bingwa mara 29 ligi kuu na leo atakabidhiwa kombe lake kwa msimu wa pili mfululizo, huku Polisi Tanzania na Ruvu Shooting wakiwa wameshuka daraja.

Chanzo: Mwanaspoti