Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nguvu ya soka imeshindwa Israeli, Palestina

Israel X Palestine Nguvu ya soka imeshindwa Israeli, Palestina

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo soka umekuwa na sifa ya kuvunja mipaka ya uadui katika jamii mbalimbali. Wakati wa vita ya kwanza ya dunia majeshi ya Uingereza na Ujerumani yaliweka silaha chini na kupiga pambano la soka la mkesha wa Krismasi (Christmas truce) ambalo limekuwa maarufu na liko kwenye historia ya mchezo huo na historia ya vita hiyo iliyopiganwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Nimepata maswali mengi ya wapenzi wa soka wakiuliza ni kwa nini timu ya taifa na klabu za Israeli zinacheza mashindano ya Ulaya yaliyo chini ya Uefa badala ya yale ya Asia yaliyo chini ya AFC.

Kuna waliouliza pia kwamba hawajawahi kusikia timu ya taifa ya Israeli ikishindana na Palestina.

Chama cha Soka cha Palestina/Israeli (PFA) kilianzishwa mwaka 1928 na kukubaliwa kuwa mwanachama wa Fifa mwaka wa 1929. Chama kiliomba kucheza Fainali za kwanza za Kombe la Dunia huko Uruguay mwaka 1930, lakini wakati wakijiandaa kusafiri, amri ikatoka kwenye serikali ya Uingereza iliyokuwa ikitawala Palestina wakati huo kwamba timu haiwezi kucheza kwenye fainali hizo zilizokuwa zimegomewa na Chama cha Soka cha Uingereza (The FA).

Mpira wa miguu na sekta nzima ya michezo imekuwa muathirika wa mgogoro wa Israeli na Palestina au tuseme Israeli na majirani zake wa Kiarabu. Kwa sababu kuundwa kwa taifa la Kiyahudi mwaka 1948 kulipingwa na Palestina na mataifa jirani kama Misri, Syria, Jordan na Lebanon. Hivyo Israeli haikupokewa vizuri hata katika Shirikisho la Vyama vya Soka vya Asia (AFC). Chama cha Soka cha Israeli (IFA) kilijiunga na AFC mwaka 1954, lakini miaka 20 baadaye yaani mwaka 1974, ilitimuliwa AFC baada ya wanachama wengi wa bara Asia kuweka shinikizo na kukataa kucheza na Israeli.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa Israeli kucheza katika mashindano ya Bara Asia. Timu ya kwanza ya taifa hilo ilikuwa na wachezaji mchanganyiko wa wayahudi na waaarabu.

Mwaka 1991 klabu za Israeli zilianza kucheza katika mashindano ya Klabu ya Ulaya (Uefa), huku ikiwa kama mwanachama mshiriki (Associate Member), hadi mwaka 1992, ilipokubaliwa kushiriki mtoano kuelekea Fainali za Kombe la Dunia na mwaka 1994 ikakubaliwa kama mwanachama kamili wa Uefa.

Upande wa Waarabu hawakuridhika na jinsi Chama cha Soka cha Palestina (PFA) kilivyoendesha mambo yake. Walidai kwamba chama kiliwapendelea Wayahudi na kiliongozwa karibu na Wayahudi peke yao. Mwaka 1934 klabu za Waarabu zikaamua kugomea timu ya taifa na Chama cha Soka, hivyo kuanzisha Chama kingine kilichoitwa General Palestinian Sports Association (GPFA). Huo ukawa mwanzo wa mgawanyiko kati ya Waarabu (Wapalestina) na Wayahudi (Waisraeli) katika uga wa soka. Mwaka 1998 Chama cha Soka Palestina kiliomba na kukubaliwa kuwa mwanachama kamili wa Shirikisho la Soka la Asia (AFC) na lile la Kimataifa (FIFA). Hii ni baada ya kupatikana kwa mamlaka ya Palestina.

Uendeshaji wa soka katika mamlaka ya Palestina umekuwa ni mgumu, kwani Israeli imekuwa na udhibiti katika mambo mengi kama kusafiri kwa timu na kuruhusu au kuzuia vifaa vinavyoingia. Mamlaka ya Palestina inalazimika kuendesha ligi mbili yaani moja kwenye ukanda wa Magharibi wa Jerusalem na nyingine kwenye ukanda wa Gaza. Timu ya taifa ya Palestina imekuwa ikilazimika kucheza michezo ya kimataifa katika viwanja vya ugenini, hii ni kufuatia vizuizi vya kusafiri vinavyowekwa na Israeli. Palestina imekuwa ni kama nchi ndani ya nchi ya Israeli, hivyo haina uhuru kamili wa kuamua mambo yake ikiwemo yanayogusa soka.

Kwa sababu ya vikwazo vya kusafiri, timu ya taifa ya Palestina imekuwa ikitegemea zaidi wachezaji walio nje (diaspora) kama Marekani, Misri na kwingineko, kwani Israeli imekuwa ikigomea visa za kuingia na kutoka kwa wachezaji wa Palestina wanaoishi ukanda wa Gaza na ukingo wa Magharibi. Michezo mingi ya klabu na hata timu ya taifa ya Palestina imekuwa ikishindwa kufanyika kutokana na mkono wa chuma wa Israeli. Mapigano ya mara kwa mara yamesababisha vifo vya wachezaji wa Kipalestina na pia kuna wachezaji wanaotumikia vifungo katika Magereza ya Israeli. Miundombinu ya kuchezea kama viwanja vimekuwa vikipigwa mabomu, hivyo kuifanya isiwe salama kwa soka.

Matukio hayo yote ni matokeo ya uhasama kati ya Palestina na Israeli. Ni vigumu kutumia soka kuwaleta karibu ndugu hawa. Soka lenyewe pia ni muathirika wa kinachotokea katika jamii hizo za Mashariki ya Kati.

Kwa nyakati tofauti zimefanyika juhudi za kimataifa za kuwaleta ndugu hawa pamoja kupitia soka, lakini hazikuzaa matunda. Soka lenyewe liko korokoroni, unahitaji mkombozi. Kupitia Fainali za Kombe la Dunia la Qatar 2022, Fifa ilifanya mpango wa mashabiki kutoka Israeli na mamlaka ya Palestina kusafiri pamoja kwenda Qatar ikiwa ni njia ya kujaribu kuzileta jamii hizi karibu.

Mashindano ya Qatar yalishuhudiwa harakati nyingi za kuwasemea Wapalestina kupitia mabango na bendera zilizoonekana viwanjani kana kwamba Palestina ilikuwa inacheza. Baadhi ya vyombo vya habari ya Bara Amerika Kusini viliipachika jina Palestina kama ‘timu ya 33’ ya Kombe la Dunia kutokana na bendera yake kuwa kila mahali.

Pamoja na sifa yake ya kuwaleta watu pamoja katika mgogoro wa Israeli na Palestina mpira umekuwa moja ya alama, sehemu na pia muathirika wa mgawanyiko wa jamiii hizo za Mashariki ya Kati. Itachukua muda kwa Israeli na majirani zake kukutana uwanjani na kushikana mikono kama ilivyokuwa kwa Wajerumani na Waingereza kwenye mahandaki ya Vita Kuu ya Dunia.

Chanzo: Mwanaspoti