Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngono kambini inavyotesa mastaa

Brown 780x470 Ngono kambini inavyotesa mastaa

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Moja ya kazi ngumu kwa viongozi wa klabu za soka hususan mameneja ni ishu ya kuwasimamia wachezaji ikizingatiwa kwamba ni watu wenye uwezo wa kuamua mambo kulingana na vile watakavyo.

Bahati mbaya zaidi kwao ni kwamba, wachezaji kuna wakati wanalazimika kuwa kambini pamoja ili kupokea maelekezo kutoka kwa makocha vizuri na pia kulinda nidhamu na kuelekezana mambo mbalimbali.

Hata ukibahatika kupata nafasi ya kukutana na mameneja wa klabu mbalimbali na kupiga nao stori juu ya ugumu wa kazi zao klabuni, unaweza kushangazwa na yale wanayokutana nayo katika kuhakikisha kazi zao zinakuwa na ufanisi na kuendelea kuaminiwa na viongozi wa juu wa klabu hizo.

“Hakuna kitu kigumu kama kusimamia wachezaji, hasa watu wazima, ni mtihani mgumu kwelikweli.” Hiyo ni kauli ambayo aliwahi kuisema aliyekuwa meneja wa timu ya Simba, Patrick Rweyemamu ambaye kwa sasa yupo kwenye soka la vijana.

Licha ya ugumu huo, lakini Rweyemamu anajivunia mafanikio makubwa aliyonayo kwani alikuwa kipenzi cha wachezaji kutokana na kujua namna ya kwenda nao sawa na pale ilipotokea wameenda nje ya mstari alisimamia misingi ya kazi yake na kuaminika zaidi kwa viongozi, yaani hakuwa na mbambamba!

Kama hujui ni kwamba mameneja ndio watu ambao wanasimamia kipi wachezaji wanatakiwa kufanya na kipi ni mwiko kwao pindi ambapo wanakuwa kambini, hawa ndio wenye siri za wachezaji na ndio watu ambao viongozi hula nao sahani moja ikiwa mchezaji fulani haonekani kambini kwani zipo kesi za wachezaji kutoroka kambini.

Kulingana na sheria ambazo klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara zimejiwekea haya ni mambo baadhi ambayo mchezaji akiyafanya huwa kuna adhabu nyuma yake inamfuata, anaweza kukatwa sehemu ya mshahara wake, kusimamishwa kwa kipindi fulani kama sehemu ya kuchukuliwa hatua.

NGONO KAMBINI

Hiki sio kitu ambacho kipo kwenye makaratasi ya mikataba ya wachezaji au kwenye ubao wa matangazo kambini, lakini ni kati ya mambo ambayo mameneja wamekuwa wakikumbana nayo kwa kiasi kikubwa.

Hakuna adhabu ya moja kwa moja, lakini inaelezwa kuwa viongozi wamekuwa wakikutana na kujadili ikiwa tukio la namna hiyo limetokea kisha hutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine.

Akiongelea hilo upande wa Singida FG, kipa wa kikosi hicho, Beno Kakolanya anasema, “Kwetu hakuna mchezaji ambaye amewahi kukamatwa au kuwa na tuhuma za namna hiyo, lakini inafahamika kuwa ni kosa kuingiza mwanamke awe mkeo au mchumba kambini kwa sababu kikawaida mchezaji unatakiwa kulinda mazoezi yako, unaweza kuendelea na hayo mengine katika siku za mapumziko.”

Hata hivyo, inaelezwa kuwa baadhi ya mastaa hasa wale ambao klabu zao zilikuwa zikiweka kambi hotelini, walishawahi kufanya utukutu na kushughulikiwa kimyakimya bila umma kufahamishwa, ingawa inaelezwa huchangiwa zaidi na udhaifu wa mameneja ambao huzembea na kuzidiwa ujanja na wachezaji.

Nyota mmoja wa zamani wa timu ambayo kwa sasa haipo ya Temeke United, (jina tunalo) anaeleza wakati wakiwa kwenye michuano ya Ligi Daraja la Kwanza jijini Arusha, mmoja wa makipa wao alizingua kwa kujifanya anaumwa na kukacha mechi, lakini alibambwa akiwa ameingiza mpenzi kambini.

Anasema hakukuwa na msalie, kwani alichokumbana nacho ni kutimuliwa jumla kikosini kwani alionekana ni mtu aliyevuka mipaka na kukiuka miiko ya kambi.

Hata hivyo, kwa mazingira ya kibinadamu na hali halisi ya kibailojia kila binadamu aliyetimia anakuwa na hamu ya kukutana na mtu wa jinsia tofauti na yake na hapo ndipo ugumu zaidi wa kuhakikisha kwamba wengi wao hawatoki ovyo nje ya kambi.

KWANINI IWE HIVYO?

Klabu zimekuwa zikiweka misingi na taratibu nzuri ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa kwenye mstari mnyoofu na kwenda kinyume cha hayo ni sawa na gari ambalo limepata pancha, hivyo ni ngumu kuendelea na safari.

Mchezaji akifanya anachotaka ni ngumu kocha kupata kile ambacho anataka kutoka kwake kuanzia kwenye uwanja wa mazoezi na hadi katika mechi.

Wakati akiwa kocha wa Chelsea, Frank Lampard aliweka sheria ya kutoza faini ya Pauni 20,000 (Sh63.7 milioni) iwapo mchezaji atachelewa kufika mazoezini na Pauni 500 (Sh1.5 milioni) kwa kila dakika watakayokosa kwenye mikutano ya timu.

Kwa klabu za Tanzania hasa zilizopo Ligi Kuu Bara nako kuna sharia zilizowekwa kudhibiti wachezaji kambini na wale wanaozingua wanajikuta kwenye wakati mgumu, ikiwamo kukatwa fedha za mishahara au posho ili kuwafanya wanyooke, kwani hakuna mtu anayefurahia kupunguzwa kipato alichonacho.

KUCHELEWA KIKAO

Inaelezwa klabu nyingi za Ligi Kuu Bara zimekuwa zikionyana zaidi kwa mdomo kufuatia mchezaji kuchelewa kwenye vikao vya timu, mfano mzuri ni Mtibwa Sugar iliyomkiri haina adhabu za kukata fedha, lakini kwa vigogo wa soka Simba na Yanga hakuna changamoto katika utekelezaji wa hilo.

Nyota wa zamani wa Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar na Singida United, Eliuter Mpepo ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa Zambia akiwa na timu ya Trident anasema; “Kwa timu kubwa ndio kunaweza kuwa na adhabu za kukatwa fedha kwa kuchelewa kwenye kikao mfano wakati nikiwa Angola niliwahi kukatwa pesa kwa kuchelewa kikao; kwa kila dakika wanakata elfu tatu.”

Mpepo anasema kwenye klabu alizochezea nyumbani hakuwahi kuona adhabu kama hizo kwani kila aliyechelewa au kukiuka jambo lolote aliishia tu kuonywa na walirekebishika.

Hata hivyo, kwa upande wa Simba, mchezaji anayechelewa kikao au kwenye mazoezi faini yake ni Sh50,000 hivyo kila mmoja amekuwa akijisimamia mwenyewe kwenye kikosi hicho ili asikumbane na rungu hilo la kukatwa kiasi hicho cha fedha kwenye kila kosa ambalo linahusiana na kushindwa kutimiza majukumu yake kwa wakati hasa kwa kuchelewa.

Ikitokea mchezaji hajafika kabisa mazoezini adhabu huongezeka na adhabu yake kuwa Sh100,000 huku kwa upande wa matukio ya utovu wa nidhamu hatua ambazo huwa zinachukuliwa ni kusimamishwa kwa mchezaji kwa muda usiojulikana kama ilivyotokea siku chache zilizopita kwa Clatous Chama.

Wachezaji wote wa Simba wakati wa chakula wamekuwa wakivaa sare maalumu huku kila mmoja akitakiwa kutokuwa na simu na wembe wa adhabu ni ule ule kwa mchezaji ambaye atachelewa.

KUCHELEWA KAMBINI

Kila klabu imekuwa na namna yake ya kuwachukulia hatua wachezaji ambao wamekuwa wakichelewa kuripoti kambini lakini kwa upande wa Yanga, inaelezwa wapo wachezaji ambao walikatwa Sh500,000 kila mmoja baada ya kuchelewa kuripoti kambini bila ya kuwa na ruhusa maalumu.

Adhabu ya kukatwa fedha kwenye mishahara yao inaelezwa kuwa ni moja, upande mwingine kocha naye anaweza kumshughulikia kwa jinsi atakavyo, ikiwamo kumsugulisha benchi mchezaji husika ili kumshikisha adabu, kwani kuchelewa kwake kumemfanya ashindwe kwenda sawa na programu za timu ambazo wamekuwa nazo kwa kipindi hayupo.

Stephane Aziz Ki, nyota wa kimataifa wa timu hiyo kutoka Burkina Faso anadaiwa kuwa mmoja wa waathirika ambao wamewahi kukumbana na adhabu za kuchelewa ikiwemo kusugua benchi wakati huo Yanga ikinolewa na kocha Nasreddine Nabi ambaye kwa sasa ni kocha wa FAR Rabat ya Morocco.

Kwa upande wake, beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anaeleza kwa kipindi chote ambacho ameichezea timu hiyo ya Wananchi hajawahi kukumbana na adhabu yoyote kali kutokana na kufuata taratibu.

“Ndani ya vipindi viwili tofauti ambavyo nimekaa Yanga sijawahi kukumbana na adhabu yoyote kubwa, nilikuwa nafanya kila ambacho natakiwa kufanya kwa wakati na nikiwa na dharura natoa taarifa kwa viongozi mapema,” anasema Ninja aliyesajiliwa kutoka Taifa Jang’ombe na aliyewahi kwenda kucheza soka la kulipwa Marekani kabla ya kurejea nchini na kutolewa kwa mkopo Dodoma Jiji.

KUTOKA BILA RUHUSA

Ikiwa mchezaji wa KMC ataondoka kambini bila ya ruhusa anaweza kukumbana na adhabu mbili tofauti, kukatwa sehemu ya mshahara wake hakuna kiwango maalum au kusimamishwa kwa muda ambao viongozi wataamua.

Nyota wa KMC, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ anaeleza vile ambavyo amekuwa akikabiliana na marufuku ambazo zimekuwa zikiwekwa na waajiri wake.

“Kutoroka kambini ni kesi kubwa, viongozi watakaa na wewe kujua sababu na wakijiridhisha watatoa adhabu kulingana na sababu ambazo umetoa, mara nyingi wachezaji wamekuwa wakikatwa mishahara au kusimamishwa na muda mwingine vyote vinaweza kufanyika kwa wakati mmoja,” anasema.

MAHOJIANO BILA RUHUSA

Kitendo cha mchezaji kufanya mahojiano na chombo chochote cha habari bila ya ruhusa ya klabu yake ni kati ya makosa ambayo kwa wachezaji wamekuwa wakikumbana na rungu la kukatwa sehemu ya mishahara yao.

Mara kadhaa nyota wa Simba, Yanga na hata Azam wamekuwa wakigoma kufanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari kwa hofu ya kukatwa mishahara. Muda ambao wamekuwa wakipata ruhusa hiyo bila ya hata kutakiwa kuzidisha ni baada ya mchezo kumalizika tena katika eneo maalumu ambalo huitwa Mixed Zone huwa kwa dakika chache.

Kwa upande wa Simba, Yanga na Azam inaelezwa adhabu ya kufanya mahojiano bila ya ruhusa adhabu yake unaweza kukatwa hadi Sh200,000 na hilo limewafanya wachezaji kuwa makini zaidi kuliko hata kuzingua kuchelewa kuwahi mazoezini.

Beki wa Dodoma Jiji, Joram Mgeveke amesema: “Binafsi nadhani ni utaratibu mzuri, nimekuwa nikiwaeleza waandishi ambao wamekuwa wakipenda kufanya mahojiano na mimi kwenda kwa uongozi kuomba kibali, vinginevyo tumekuwa tukiingia matatani. Na hakuna kiwango maalumu tunachotozwa.”

Chanzo: Mwanaspoti