Kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma amesema kwa uzoefu wake na soka la Afrika, Simba ina kikosi kizuri ambacho kinaweza kubeba ubingwa wa ligi na hata Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ngoma aliyetua Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan amefunguka kukutana na ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho lakini kubwa zaidi amesifu usajili uliofanyika na aina ya kikosi kilivyo.
“Tuna timu nzuri, ushindani ni mkubwa na malengo yetu ni kufanya vizuri na kutwaa mataji.
Ligi ni ngumu na inaushindani mkubwa, lakini pia ndani ya timu kuna ushindani wa kutosha kutokana na aina ya wachezaji waliopo kila mmoja ana ubora na sifa zake,” alisema Ngoma na kuongeza;
“Kama wachezaji tumejipanga kufanya vizuri ili kufikia malengo, na naamini tutafanya vizuri zaidi msimu huu na kuwapa furaha mashabiki wa timu hii.
Kiungo huyo wa zamani wa MK Etancheite na AS Vita za DR Congo, Ifaenyi Ubah ya Nigeria, Raja Casablanca ya Morocco, Al Faheheel na Al Hilal za Sudan aliwahi kutakiwa na mabingwa watetezi wa ligi, Yanga lakini baadae alichagua kujiunga na Simba.
Ngoma tangu amejiunga na Simba, ameonekana kuingia taratibu kwenye mfumo katikati ya Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute na tayari ameifungia Simba mabao mawili hadi sasa. Robertinho alieleza Ngoma bado anahitaji muda zaidi ili kuwa bora na ataendelea kumpa nafasi ili hilo litimie.
“Kuna wachezaji ambao wanahitaji muda kidogo akiwemo Ngoma, tupo hapa kutengeneza timu yenye muunganiko kwani tuna michuano mingi, naamini siku chache zijazo mtawaona wakiwa kwenye ubora wao na kuisaidia Simba,” alisema.