Kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma amefunguka namna watakavyowachakaza Jwaneng Galaxy ya Botswana ikiwa ni mechi ya mwisho ya hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ngoma ambaye alianza kuitumikia Wekundu hao wa Msimbazi msimu huu, amekuwa na uzoefu na michuano ya kimataifa kutokana na rekodi kali alizonazo katika timu alizowahi kuchezea.
Uzoefu wa kiungo huyo ambaye amecheza mechi 13 kati ya 15 za Ligi Kuu Bara na kufikisha jumla ya dakika 1131, huenda akaisaidia Simba kuweka rekodi nyingine mpya kama Kocha Abdelhak Benchikha atampa nafasi katika mechi hiyo.
Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi Machi 2 Saa 1:00 Jioni, huku timu zote mbili zikiingia zikiwa na pointi sita.
Mkongomani huyo amecheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na kufunga mabao matatu na kwenye Shirikisho amecheza mechi 23 akifunga mabao sita na asisti nne.
Staa huyo mwenye uwezo wa kucheza kama beki wa kati pia alizungumza na Mwanaspoti na kusema, wanakwenda kucheza mechi ambayo wanatakiwa wachezaji wenyewe ndio waiamue.
Alieleza sio vizuri kwa timu kubwa kama yao kushinda mechi moja mpaka sasa lakini waliobeba matumaini na heshima ya Simba ni wachezaji.
“Mechi iko mikononi mwetu, ni sisi tuamue kufanya makubwa ili kutinga hatua inayofuata kwa ushindi mkubwa ambao utarejesha nguvu kwenye kikosi na kocha kwa jumla.
“Kuwa makini na kutumia nafasi zote tunazopata ndizo zinaweza kuamua ni matokeo gani tutapata kwani tuko uwanja wa nyumbani mahali ambapo tunapafahamu vizuri, hivyo hatutafanya makosa tena.”
Aliongeza; “Haijalishi wapinzani watakuja vipi ila lazima tuwaonyeshe nini tunachokitaka ijapokuwa hatuna rekodi nzuri nao.”
Simba na Jwaneng Galaxy, zimekutana mara tatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kila timu ikiibuka na ushindi mara moja huku zikitoka sare moja.
Wekundu hao wameshinda mechi moja kati ya tano walizocheza katika michuano hiyo na kuwafanya kufikisha jumla ya pointi sita wakiongozwa na ASEC Mimosas wenye 11 na mhezo wa Jumamosi utaamua hatma yao.