Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngawina ajibebesha mabomu Singida FG

Makocha Singida Ngawina ajibebesha mabomu Singida FG

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa muda wa Singida Fountain Gate, Ngawina Ngawina ametua kwenye klabu hiyo huku akijibebesha mabomu kwa kusema anataka kutumia muda mwingi mazoezini kuhakikisha wachezaji wanarejesha morali ya ushindi ili wafanye vyema katika michezo iliyosalia kwenye ligi na kuiokoa timu isishuke daraja.

Ngawina aliyepewa mikoba ya kuinoa timu hiyo, Machi 7 mwaka huu baada ya uongozi wa timu hiyo kulivunja benchi zima lililokuwa chini ya Kocha Thabo Senong kutoka Afrika Kusini akisaidiana na Nizar Khalfan na mara baada ya utambulisho wake, kocha huyo wa zamani wa Ndanda na FTA Talents amesema atapambana kurejesha morali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngawina amesema baada ya kukabidhiwa timu hiyo jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha morali inarejea kwenye kikosi hicho;

“Kwa kuwa timu hii imefungwa michezo mingi katika Ligi Kuu, ikiwa haijashinda kwa muda mrefu kabla na baada ya ligi kurejea kwenye mazoezi, natumia muda mwingi kurejesha morali ya upambanaji iliyokuwa imepotea ili tuweze kufanya vizuri michezo iliyobaki," amesema Ngawina na kuongeza;

“Naamini hadi kufikia Machi 12 tutakapokabiliana na Simba ugenini, kikosi kitakuwa katika hali nzuri kwani wachezaji wengi waliopo hapa nawafahamu, pia nitaongea nao kila mara ili kuondoa dhana ya kukata tamaa isiwepo vichwani mwao na kuipigania timu hadi dakika ya mwisho."

Tangu Novemba, Singida imecheza jumla ya michezo nane ya ligi bila kushinda ikiambulia tu sare tatu na vipigo vitano vilivyoifanya ishike nafasi ya 10 kwa sasa ikivuna pointi 21 tu katuika mechi 19 na sasa imesaliwa na michezo 11 mkononi ili kuamua hatma ya kusalia kwa msimu ujao ama iangukie kwenye janga la kushuka daraja.

Mechi ilizosaliwa nazo kwa sasa ni pamoja na hiyo ya Simba itakayopigwa Machi 12, Namungo, Yanga, Ihefu, Geita Gold, Mashujaa, Dodoma Jiji, Coastal Union, JKT Tanzania, KMC na Kagera Sugar.

Katika michezo hiyo, sita tu itakuwa nyumbani na mitano itakuwa ugenini na kumpa kazi kubwa Ngawina kupambana hili apate matokeo mazuri kutimiza azma ya kuinusuru timu hiyo iliyohamisha maskani kutoka Singida hadi jijini Mwanza na ikiwa imekimbiwa na nyota kadhaa dirisha dogo walioibukia Ihefu iliyopo pia Ligi Kuu.

Baadhi ya nyota hao tegemeo waliotimkia Ihefu na wanaendelea kuwasha moto huko ni Marouf Tchakei, Duke Abuya, Elvis Rupia, Joash Onyango, Abubakar Khomeiny na Morice Chukwu, huku Gadiel Michael akicheza soka la kulipwa Afrika Kusini, wakati Bruno Gomes akijiondoa ghafla klabuni hapo kabla ya benchi kuvunjwa.

Chanzo: Mwanaspoti