Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngao ya Jamii 2024 wababe wanakutana

Wababeeeeee Ngao ya Jamii 2024 wababe wanakutana

Thu, 8 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Azam vs Coastal Union ni mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Ngao ya Jamii utakaochezwa leo Alhamisi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.

Baada ya kuanza kwa mchezo huo, tutashuhudia Kariakoo Dabi itakayopigwa Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ikiikaribisha Simba kuanzia saa 1:00 usiku. Kumbuka Simba ndiyo mabingwa watetezi wa Ngao ya Jamii.

Mechi hizi ni za ufunguzi wa msimu wa mashindano ya soka 2024-2025 yaliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mfumo wa Ngao ya Jamii kushirikisha timu nne ulianza msimu uliopita na Simba ilikuwa bingwa baada ya kuifunga Yanga kwa penalti 3-1 kutokana na muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0. Azam ilishika nafasi ya tatu wakati Singida Fountain Gate ikiwa ya nne.

Timu zinazoshiriki Ngao ya Jamii ni zile zinazomaliza msimu zikiwa ndani ya nne bora katika msimamo wa Ligi Kuu Bara. Mfumo wa zamani uliokuwa ukishirikisha timu mbili, bingwa wa Ligi Kuu Bara na bingwa wa Kombe la FA. Lakini ikitokea bingwa wa ligi ndiye bingwa wa FA, basi mshindi wa pili wa ligi ndiye atakayecheza na bingwa.

Leo ikiwa ndiyo mechi za nusu fainali ya Ngao ya Jamii zinachezwa kabla ya Jumapili ya Agosti 11, 2024 kushuhudia fainali itakayotanguliwa na kusaka mshindi wa tatu, hapa kuna uchambuzi wa timu shiriki namna zilivyokuwa zikifanya maandalizi yao.

YANGA

Ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, walianza kambi yao Julai 8, 2024 jijini Dar es Salaam kabla ya Julai 18 kwenda Afrika Kusini.

Wakiwa Afrika Kusini, Yanga walicheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani na kupoteza kwa mabao 2-1. Jean Baleke ndiye aliyekuwa mfungaji wa bao pekee la Yanga.

Kisha ikapambana na TS Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube. Mechi hizo mbili zilikuwa ni katika mashindano maalumu ya Mpumalanga Cup.

Mchezo wa mwisho wakiwa Afrika Kusini, Yanga walicheza dhidi ya Kaizer Chiefs inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini na kushinda mabao 4-0 yakifungwa na Prince Dube, Clement Mzize na Stephane Aziz Ki aliyepachika mawili.

Vijana hao wa Kocha Miguel Gamondi, walirejea Dar wakiwa na Kombe la Toyota walilokabidhiwa baada ya kuifunga Kaizer Chiefs inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi.

Ukiangalia mechi hizo tatu walizocheza Yanga wakiwa Afrika Kusini zote ni dhidi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu kwenye nchi zao, kubwa zaidi ni ile kupambana na Augbsburg inayoshiriki ligi iliyo ndani ya tano bora barani Ulaya.

Mchezo wa nne ambao ni wa mwisho kabla ya Ngao ya Jamii, Yanga imecheza dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Zambia na mabingwa wa Kombe la Kagame 2024, Red Arrows, wakashinda 2-1 kupitia Stephane Aziz Ki na Mudathir Yahya.

Matokeo ya mechi hizo nne yanaonyesha, Yanga katika utafutaji wake wa ushindi umebalansi kwa maana ya mabao nane yaliyofungwa viungo wamehusika katika manne na washambuliaji manne. Viungo ni Aziz Ki (3) na Mudathir (1), washambuliaji wakiwa ni Baleke (1), Mzize (1) na Dube (2).

Hii inatupa picha ndani ya kikosi cha Yanga mchezaji wa nafasi yoyote kuanzia kwenye kiungo anaweza kukuadhibu kwani hata msimu uliopita ndani ya ligi lilijidhihirisha hilo ingawa viungo ndiyo walikuwa na mchango mkubwa wa mabao.

Ipo hivi; Aziz Ki (21), Maxi Nzengeli (11), Mudathir (9) na Pacome Zouzoua (7), ndiyo waliokuwa juu kwenye chati, hawa wote ni viungo, akafuatia Clement Mzize (6), Joseph Guede (6) na Kennedy Musonda (4) ambao ni washambuliaji.

Yanga wana mtihani wa kuhakikisha wanashinda dabi hii dhidi ya Simba ili kulipa kisasi cha kufungwa msimu uliopita kwenye fainali walipopoteza taji lao, safari hii wanataka kuona nao wakiwapokonya wapinzani wao.

Kisha kuendeleza rekodi bora mbele ya Simba waliyoiweka msimu uliopita kwenye ligi baada ya kushinda jumla ya mabao 7-2 katika mechi zote mbili walizokutana.

Rekodi zinaonyesha Yanga wameshinda makombe saba ya Ngao ya Jamii, wanahitaji la nane ili kuikaribia Simba yenye 10.

Wakati TFF ikipanga ratiba ya mechi za Ngao ya Jamii, Gamondi alisema: “Kwangu mimi mashindano ya Ngao ya Jamii sio muhimu sana, hapa Tanzania muhimu ni Ligi Kuu, katika Ligi unaonyesha ubora wako kwani tunacheza mechi 30, lakini katika vikombe unaweza kuwa na siku mbaya ukatolewa kwa sababu ni mechi za mtoano.

“Tunataka kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa, tunataka kujaribu kufika mbali zaidi kwenye mashindano ya CAF zaidi ya msimu uliopita.”

Hivi karibuni baada ya kuishuhudia Simba ikiifunga APR katika Simba Day, siku moja mbele Gamondi alisema amewaona wapinzani wao hao kuwa na mabadiliko ya uchezaji kutokana na kusajili wachezaji wenye viwango vizuri, hivyo anawakumbusha nyota wake kuachana na matokeo ya msimu uliopita ili waingie uwanjani kuendeleza ubabe wao.

AZAM

Wakiwa na kombe moja pekee la Ngao ya Jamii waliloshinda mwaka 2016 walipoifunga Yanga kwa penalti 4-1, safari hii wanaingia uwanjani wakisaka taji lao la pili katika michuano hiyo.

Makocha Bruno Ferry na Youssouph Dabo wana kazi ya kuiondosha Coastal Union ili kufika fainali na kupiga hesabu za kubeba ubingwa.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara 2013-2014, juzi Jumanne jioni waliondoka Dar es Salaam na kwenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo huo.

Azam kwenda kucheza New Amaan Complex unaweza kusema ni kama uwanja wameshauzoea tayari kwani mapema mwaka huu Januari walikuwa huko kushiriki Kombe la Mapinduzi, kisha Juni 2, 2024 wakacheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Yanga.

Baada ya hapo, kambi yao ya maandalizi ya msimu ujao waliiweka Zanzibar kuanzia Julai 9 hadi 13 na kucheza mechi moja dhidi ya Zimamoto wakashinda 4-0, wafungaji ni kiungo Feisal Salum (2) na mshambuliaji Jhonier Blanco (2).

Julai 15 wakaenda Morocco kuweka kambi ya wiki mbili, wakiwa huko wakacheza mechi dhidi ya US Mansour, wakapata ushindi wa mabao 3-0. Beki Cheikh Sidibe, kiungo Gibril Sillah na Blanco ambaye ni mshambuliaji ndiyo waliokuwa wafungaji.

Mchezo uliofuata ni dhidi ya Union Touarga, matokeo yakawa sare ya bao 1-1. Kiungo Nassor Saadun alikuwa mfungaji wa Azam, wakafunga kambi kwa kucheza dhidi ya Wydad Casablanca, wakafungwa 4-1, bao lao lilifungwa na Cheikh Sidibe.

Azam katika maandalizi yake imecheza mechi nne, ile ya mwisho ni dhidi ya Rayon Sports kutoka Rwanda iliyochezwa nchini humo, wakashinda 1-0 kupitia beki Lusajo Mwaikenda na kubeba Kombe la Chopslife.

Mechi tano Azam ilizocheza imefunga mabao kumi na kuruhusu matano, inaonyesha wapo vizuri katika kufumania nyavu, lakini safu ya ulinzi inahitaji maboresho kidogo ingawa mechi ambayo waliruhusu mabao mengi ilikuwa dhidi ya wababe wa Morocco, Wydad Casablanca unaweza kusema kilikuwa kipimo kikubwa zaidi ya timu zingine ilizopambana nazo.

Mabao hayo kumi, matatu yametoka kwa mshambuliaji mmoja, viungo wamefunga matano na mabeki matatu. Hii inaonyesha Azam ipo vizuri kufungua mabao kupitia nafasi zote, beki, kiungo na mshambuliaji.

SIMBA

Mechi tatu za kirafiki ilizocheza kambini wakiwa Misri, ilishinda zote dhidi ya Canal SC (3-0), Telecom Egypt (1-2) na Al Adalah (2-1).

Mchezo wa kwanza dhidi ya Canal, Kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua alifunga mawili na kiungo mkabaji Augustine Okejepha moja. Waliposhinda 2-1 dhidi ya Telecom Egypt, mshambuliaji Valentino Mashaka na kiungo mshambuliaji Ladaki Chasambi kila mmoja alifunga bao moja, kisha mshambuliaji Steven Mukwala na Kiungo mshambuliaji Joshua Mutale wakafunga mojamoja dhidi ya Al Adalah.

Mchezo wa mwisho ni katika Simba Day wakashinda 2-0 dhidi ya APR kwa mabao ya viungo Debora Fernandes na Edwin Balua.

Hapa inaonyesha Simba usajili mpya umeanza kulipa mapema kwani kati ya mabao tisa iliyofunga, wachezaji wapya wamefunga saba. Kwa jumla washambuliaji wamefunga mawili na viungo wakifunga saba.

Hawana tofauti na Yanga kwani nao washambuliaji na viungo wamehusika kwenye mabao ingawa tofauti yao ipo katika idadi ya mabao. Simba ikifunga tisa na Yanga nane.

COASTAL UNION

Kati ya timu nne zinazocheza Ngao ya Jamii, Coastal Union unaweza kusema ni wageni wa michuano hii kwani ni mara yao ya kwanza kushiriki.

Ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki, wakaamua kujipanga kisawasawa kuanzia maandalizi yao na waliweka kambi yao kisiwani Pemba ili kuzoea mandhari yanayoendana na sehemu wanayokwenda kucheza. Jumatatu wakatua zao Unguja kutokea Pemba tayari kwa mchezo dhidi ya Azam.

Kabla ya hapo, walishiriki michuano ya Kagame iliyofanyika Dar es Salaam, hawakufanya vizuri kutokana na kuishia hatua ya makundi baada ya kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza moja.

Kocha wa Coastal Union, David Ouma ameonekana kuridhishwa na maandalizi ya kikosi chake baada ya kucheza mechi hizo za Kagame sambamba na za kirafiki wakiwa Zanzibar na walimaliza maandalizi yao kwa kuifunga Uhamiaji mabao 2-0, wafungaji wakiwa Abdallah Hassan na Denis Modzaka.

Katika Kagame waliifunga Dekedaha 1-0 kupitia bao la Mwenda Ramadhan, wakafungwa 2-0 na JKU, kisha wakatoka sare ya 1-1 dhidi ya Al Wadi FC, mfungaji wao akiwa Abdallah Hamis.

Wagosi wa Kaya wamefanya maboresho si tu kwa wachezaji bali hata benchi la Ufundi kwa kumshusha Ngawina Ngawina kumsaidia Ouma.

Chanzo: Mwanaspoti