Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngadu, Mrwanda waongeza mzuka Copco FC

Fsfsfs Ngadu, Mrwanda waongeza mzuka Copco FC

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Copco FC ya Mwanza imeongeza dawa ya kuepuka kushuka Ligi ya Championship baada ya kuamua kuwachukua washambuliaji wakongwe Dany Mrwanda, Salum Ngadu na Morice Mahela kwenye dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu ili kutibu tatizo la upachikaji wa mabao linaloitesa.

Mrwanda amejiunga na timu hiyo kutoka Ken Gold alikokuwa meneja, Morice Mahela ametokea Tabora United na Salum Ngadu akiwa mchezaji huru, lakini nyota hao hawajaanza kucheza na wanatarajia kuanza kukiwasha katika mchezo ujao dhidi ya Stand United.

Timu hiyo inashika nafasi ya 15 ikiwa katika msimamo ikiwa na pointi 13 baada ya kuambulia sare nne, ushindi mara tatu na kupoteza miecho 11, huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu 27.

Nyota hao wanatarajiwa kuongeza uhai katika eneo la ushambuliaji lililokuwa linaongozwa na Abdulkarim Segeja aliyejiunga na Tanzania Prisons akiwa amefunga mabao manane msimu huu.

Akiwazungumzia wachezaji hao, Kocha wa Copco FC ambayo ni msimu wake wa pili Championship, Feisal Hau amesema anaamini ujio wao unakwenda kuongeza kitu na kutibu tatizo la ufungaji katika kikosi kwani amechanganya damu changa na wazoefu.

Amesema amepata matumaini ya kikosi kuwa bora baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Biashara United mwishoni mwa wiki iliyopita, hivyo hawezi kukata tamaa kwani atafanya vizuri na kikosi ili kuhakikisha hawashuki daraja mwishoni mwa msimu.

“Tatizo letu kubwa kuanzia raundi ya kwanza lilikuwa ni kumalizia na kipa. Tumetibu eneo la kipa na hata mbele kuna usajili tuliufanya. Tunaye Salum Ngadu tumemleta lakini ndani ya siku mbili hizi kapata homa, tuna Danny Mrwanda mchezaji mzoefu,” amesema Hau.

“Ana matatizo kidogo (Mrwanda) nafikiri kuanzia mechi ya Stand (Ijumaa) wote unaweza kuwaona uwanjani. Naamini watatusaidia mbele katika eneo la ufungaji wa mabao. Nyinyi wenyewe mmeona kuna watu wametoka, lakini kuna wengine wameingia.”

“Sisi kwenye selection (uchaguzi) ya wachezaji huwa tunajitahidi nafikiri mmeona kuna vijana wadogo damu changa, lakini wana uwezo wa kupambana kushirikiana na wakongwe kama Mrwanda na Ngadu naamini matokeo (mazuri) yatapatikana.”

Chanzo: Mwanaspoti