Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Newcastle yawasilisha ofa ya kumchukua Ramsdale Arsenal

Skysports Ramsdale Arsenal 5484905 Aaron Ramsdale

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Newcastle United inaandaa ofa ya Pauni 15 milioni kwenda Arsenal kwa ajili ya kuipata saini ya kipa wa timu hiyo na England, Aaron Ramsdale, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo washika mitutu hao wanadaiwa kuwa katika mpango wa kutaka kumuuza.

Mbali ya viongozi wa timu kutaka kumuuza, Ramsdale anataka kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arsenal na mbali ya Newcastle, Chelsea pia imekuwa ikitajwa huenda ikajitosa, lakini hadi sasa haijawasilisha ofa rasmi.

Mkataba wake unamalizika 2026 na Newcastle kwa sababu kipa Martin Dubravka hana muda mrefu kabla hajaondoka kutokana na umri wake mwisho wa msimu, inaachana na Loris Karius. Ofa ambayo Newcastle iliyowasilisha kumsajili Ramsdale inaonekana kuwa ndogo na huenda Arsenal ikataka nyongeza kufikia walau Pauni 20 milioni.

Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 11 za michuano yote na kuruhusu mabao 12.

CRYSTAL Palace na Fulham zinamfuatilia kwa karibu kiungo wa Fiorentina ambaye anacheza kwa mkopo Manchester United Sofyan Amrabat, 27. Mabosi wa Man United hawana mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu staa huyu na Palace pamoja na Fulham zinataka kutumia nafasi hiyo kwa ajili ya kumsajili.

NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, 29, amewaambia vigogo wa timu hiyo kwamba wanatakiwa wamuongezee mshahara ikiwa wanahitaji ili aendelee kusalia katika kikosi chao. Bruno kwa sasa anakunja Pauni 230,000 kwa wiki na anahitaji ongezeko la mshahara unaoweza kufikia Pauni 300,000 kwa wiki au zaidi. Mkataba wa sasa wa staa huyu unamalizika mwaka 2026. Hivi karibuni amehusishwa na Bayern Munich na timu za Saudi Arabia.

BAADA ya kuripotiwa kwamba wapo tayari kulipa Pauni 55 milioni kwa ajili ya kumsajili beki wa Everton Jarrad Branthwaite katika dirisha lijalo, mabosi wa Everton wamekataa na kudai kwamba wanahitaji zaidi ya Pauni 80 milioni kwa ajili ya kumuuza fundi huyo wa kimataifa wa England. Jarrad Branthwaite ni mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Everton na mkataba wake unamalizika mwaka 2027.

AC Milan inakumbana na upinzani wa kutosha kutoka kwa Arsenal katika mchakato wao wa kumsajili straika wa Bologna na Uholanzi Joshua Zirkzee, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Arsenal pia inataka kuboresha eneo lao la ushambuliaji kama ilivyokuwa kwa AC Milan kutokana na mapungufu ambayo wanayo msimu huu. Zirkzee ameonyesha kiwango bora akifunga mabao.. katika mechi 37 za michuano yote na kufunga mabao 12.

KOCHA wa Lens Franck Haise amewaambia mabosi wa timu hiyo kwamba anaihitaji huduma ya beki wa Manchester United na Ufaransa Raphael Varane, 31, ambaye anaondoka katika kikosi cha mashetani hao wekundu mwisho wa msimu huu. Hata hivyo inaonekana kuwa ngumu kwa Lens kufanikisha mchakato wa kumsajili Varane kutokana na kiasi kikubwa cha mshahara kinachohitajika na staa huyo.

REAL Madrid imeripotiwa kufikia makubaliano na kiungo wao raia wa Croatia Luka Modric ambaye atasaini mkataba mpya wa mwaka mmoja lakini itatakiwa akubali kupunguza mshahara wake wa sasa. Luka mwenye umri wa miaka 38, alikuwa akihusishwa kuondoka mwisho wa msimu huu kujiunga na moja ya timu za Saudi Arabia lakini ameamua kubaki na anaweza kustaafu akiwa na wababe hao wa Hispania.

AC Milan imeanza mazungumzo na Tottenham kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo na Brazil Emerson Royal, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Staa huyu anadaiwa kuhitaji kuondoka mwisho wa msimu huu kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Spurs na hadi sasa amecheza mechi 23 tu za Ligi Kuu England ambazo nyingi aliingia akitokea benchi.

Chanzo: Mwanaspoti