Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nenda Google! Mastaa hawa wamefunika mtandaoni mwaka huu

Ronaldo Aongoza Kwa Kulipwa Zaidi Duniani Nenda Google! Mastaa hawa wamefunika mtandaoni mwaka huu

Fri, 5 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unamkumbuka Emmanuel Adebayor? Yule straika wa futi 6 na inchi 3 aliyekipiga kwenye timu za kibabe tu Ulaya.

Adebayor amecheza AS Monaco, Arsenal, Manchester City, Real Madrid, Tottenham Hotspur na Crystal Palace kwa kuzitaja kwa uchache.

Jina lake lilikuwa juu zaidi alipokuwa kwenye kikosi cha Arsenal kati ya 2006 hadi 2009 kabla ya kwenda Man City, alikokuwa mwaka 2009 hadi 2012, lakini katikati yake, alitolewa kwa mkopo mara mbili, Real Madrid na Tottenham kabla kuuzwa jumla Spurs.

Adebayor ana matukio mengi ya kufarahisha, lakini kali zaidi nii hiyo aliyokuwa Man City na kile alichomwambia kocha mpya wa miamba hiyo ya Etihad kwa wakati huo, Mtaliano, Roberto Mancini.

Mancini wakati anatua Man City 2009, alimwambia Adebayor kwamba anataka kumleta Mario Balotelli kikosini kwa sababu haridhishwa na kiwango cha ufungaji wa mabao cha mkali huyo wa Togo.

Na hapo ndipo Adebayor alipoamua kuwambia kocha huyo inaonekana hamfahamu vyema, hivyo aingie mtandaoni akatafute jina la Adebayor atapata majibu yake.

Adebayor alimwambia Mancini aende Google, aandike jina la mchezaji huyo ataona idadi ya mabao yake aliyofunga kwenye Ligi Kuu England na hapo ataacha maneno yake ya kumwona hana makali kikosini.

Adebayor alisema: “Mancini siku zote ana mambo yake kila kwenye klabu anayokwenda, aliniambia: "Oooh, sikutaki. Nataka Mario Balotelli aje kucheza hapa kwa sababu mimi wastani wao wa kufunga mabao sio mzuri."

“Nikamwambia sawa, pengine unamzungumzia Adebayor mwingine. Nilimwambia ajisogeze kwenye intaneti. Nikwambia kama hiyo ni kesi, basi nenda Google katafute jina langu. Nenda Google uone kile nilichofanya kwenye hii ligi.”

Haieleweki kama Mancini alikwenda Google kutafuta jina la Adebayor ili kujua makali yake – lakini mwisho wa hilo, staa huyo wa Togo alikwenda kwa mkopo Bernabeu na Balotelli akatua Etihad.

Na wakati ikizungumziwa Google, hii hapa ndiyo orodha ya mastaa wa maana kwenye soka ambao ambao wametafutwa mara nyingi kujua taarifa zao kwenye mtandao kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa hadi kufikia katikati ya Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za Footgoal, hii ndio orodha ya wanasoka ambao wamesakwa mara nyingi taarifa zao Google ndani ya mwaka huu hadi kufikia sasa.

10. Luis Suarez (Milioni 1.7 kwa mwezi)

Hachezi tena kwenye soka la Ulaya kwa sasa, lakini straika Luis Suarez bado anachezea moja ya klabu kubwa kabisa huko Brazil, Gremio na alifunga hat-trick dhidi ya Sao Luiz kwenye mechi yake ya kwanza Januari mwaka huu. Gremio ilishinda 4-1.

9. Sadio Mane (Milioni 1.8 kwa mwezi)

Licha ya kuachana na Liverpool na kwenda kujiunga na Bayern Munich, kasha akakosa fainali za Kombe la Dunia 2022 kutokana na kuwa majeruhi, jina la Sadio Mane bado liko moto kwa mashabiki, wakiendelea kumsaka mtandaoni. Hivi sasa Mane amekuwa gumzo zaidi.

8. Gerard Pique (Milioni 1.9 kwa mwezi)

Beki wa kati, Gerard Pique alishtua dunia wakati alipotangaza kustaafu soka mwaka jana. Kwenye mchezo huo, Pique ameshinda mataji makubwa zaidi ya 30 katika misimu yake 18 na aliwahi kuwa na uhusiano na Shakira. Sasa wameachana, lakini Pique anatafutwa sana huko mtandaoni.

7. Paulo Dybala (Milioni 2.2 kwa mwezi)

Hii inashtua wengi, lakini Paulo Dybala yupo vizuri kwenye orodha ya wanasoka waliotafutwa mara nyingi mtandaoni. Baada ya kujiunga na AS Roma, staa huyo alionyesha ubora mkubwa na kuwamo kwenye kikosi cha Argentina kilichoshinda ubingwa wa dunia huko Qatar mwaka jana.

6. Karim Benzema (Milioni 2.4 kwa mwezi)

Karim Benzema anazeeka na utamu wake. Ndiye mshindi wa Ballon d’Or kwa sasa, akiwa amebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga akiwa na kikosi chake cha Real Madrid. Kwa umahiri wake wa uwanjani, umemfanya Benzema jina lake kutafutwa mara nyingi kwenye mtandao wa Google.

5. Robert Lewandowski (Milioni 3.2 kwa mwezi)

Baada ya misimu minane ya mafanikio makubwa kwenye chama la Bayern Munich, straika Robert Lewandowski alitua zake Barcelona kwenye majira ya kiangazi mwaka jana. Huko Nou Camp mambo yake si haba, huku jina lake likitafutwa mara nyingi mtandaoni.

4. Kylian Mbappe (Milioni 8.5 kwa mwezi)

Bado hajatengeneza umaarufu mkubwa sana nje ya uwanja, lakini ndani ya uwanjani, mkali Kylian Mbappe ni habari nyingine. Kinara wa mabao wa Kombe la Dunia na ndiye mfungaji wa muda wote wa PSG. Jambo hilo limevutia wengi wakimfuatilia staa huyo mtandaoni kujua taarifa zake.

3. Neymar (Milioni 9.2 kwa mwezi)

Neymar hakupata nafasi ya kuonyesha ubora wake kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 kama ambavyo alitaka, lakini anapokuwa ndani ya uwanja, mara zote huduma yake ni bora. Maumivu ya enka yamemfanya kuwa nje ya uwanja muda mrefu, lakini hilo halimzuia kutamda mtandaoni.

2. Lionel Messi (Milioni 13.2 kwa mwezi)

Kwa sasa anaelekea ukomo wa zama zake matata kwenye soka. Messi amepata kila anachokihitaji kwenye mchezo wa soka. Bado anaonyesha kiwango kizuri huko PSG na anahusishwa na mpango wa kurudi Barcelona, huku jina lake likitafutwa mara nyingi kwenye mtandao wa Google.

1. Cristiano Ronaldo (Milioni 17.4 kwa mwezi)

Hakuna kinachoshangaza hapa. Cristiano Ronaldo ni mchezaji maarufu sana mtandaoni. Staa huyo huko Instagram pekee yake ana wafuasi milioni 558 na jambo linamfanya jina lake kutafutwa mara nyingi kwenye mtandao wa Google na kushinda namba moja kwa upande wa wanasoka.

Chanzo: Mwanaspoti