Maisha ya Kiungo kutoka nchini Nigeria, Nelson Okwa katika Ligi Kuu yameendelea kuwa magumu baada ya kushindwa kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wake ndani ya timu za Simba SC na Ihefu FC alipo hadi sasa kwa mkopo wa miezi sita.
Okwa alijiunga na Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Rivers United ya nchini kwao Nigeria na mwezi Januari akapelekwa kwa mkopo wa nusu msimu Ihefu FC ambako napo mambo yamemwendea magumu.
Simba SC alishindwa kupata namba kutokana na eneo lake analocheza la kiungo mshambuliaji kuwa na mafundi zaidi kama Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Pape Sakho, Peter Banda, Moses Phiri na Saidi Ntibazonkiza.
Hali kama hiyo amekutana nayo Ihefu FC kwa mafundi kama Raphael Daudi ‘Lothi’, Never Tigere, Joseph Mahundi, Onditi na Victor Akpan waliotoka pamoja Simba SC kwa mkopo.
Hata hivyo imebainika kuwa Ihefu FC chini ya kocha mkuu John Simkoko haina mpango wa kumuongezea mkataba Okwa baada ya kumaliza muda wake wa mkopo mwishoni mwa msimu huu lakini pia Simba SC chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ nao hivyohivyo.
Okwa alipotafutwa amesema kwa sasa hawezi kulizungumzia hilo na anasubiri msimu umalizike ndipo atajua hatima yake.