Nndo hivyo. Mambo ni matamu. Ni hivi, N’Golo Kante ameripotiwa kukubali dili la kujiunga na Arsenal akitokea Chelsea mwishoni mwa msimu huu. Kiungo huyo Mfaransa mkataba wake huko Stamford Bridge utafika ukingoni mwishoni mwa msimu huu baada ya miaka saba ya kutumikia timu hiyo inayotupia uzi wa bluu.
Chelsea imekuwa ikifanya usajili wa mastaa wengi ndani ya miaka ya hivi karibuni, lakini hakika bado haijafanya uhamisho uliobora zaidi kuliko ule ilioufanya mwaka 2016, wakati ilipoilipa Leicester City Pauni 32 milioni kunasa saini ya Kante.
Kante ni mmoja wa wachezaji waliodumu kwenye kiwango bora cha soka kwa muda mrefu, ambapo katika msimu wake wa kwanza tu Chelsea aliwasaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, kabla ya kurejea kutoka majeruhi mwaka 2021 na kuwapa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Siku za karibuni alikuwa majeruhi na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na hilo ndilo linalowafanya Chelsea kusitasita juu ya kumpa ofa ya maana ya kuhusu mkataba mpya.
Lakini, kuna klabu kibao zinahitaji saini ya Kante, wakiwamo Paris Saint-Germain na Barcelona – ambapo ikifika mwisho wa msimu kiungo huyo anayekaba kuzidi maelezo atanyakuliwa bure kabisa. Hata hivyo, kinachoripotiwa ni kwamba Kante anataka kubaki England, hasa kwenye jiji la London. Hiyo ina maana inaweza kuwa Arsenal, Tottenham au akabaki Chelsea – kama watampa atakachotaka kwenye dili jipya.
Ni ngumu kuamini, Kante 32, kama atakwenda kwenye timu nyingine za London kama Crystal Palace, Brentford, Fulham au West Ham United, huku ripoti zikidai kwamba kama Chelsea watagoma, basi Kante atakuwa wa Arsenal au Spurs.
Na kinachoelezwa ni kwamba Kante amebonyesha kitufe cha 'OK' kuhusu ishu ya kuhusishwa na Arsenal wiki chache zilizopita. Na hilo linafichua kwamba staa huyo mshindi wa Kombe la Dunia 2018, alipokuwa na Ufaransa huko Russia, alisema "Yes" juu ya mpango wa kwenda kukipiga Arsenal msimu ujao, mahali ambako kwenye dirisha la Januari mwaka huu, kiungo mwenzake wa Chelsea, Jorginho alikwenda kujiunga na miamba hiyo ya Emirates, inayofukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Wakati Kante akihusishwa na mpango wa kutua Arsenal, huko kwenye Big Six ya klabu za Ligi Kuu England, mambo hayajapoa baada ya miamba mingine nayo kutajwa kwenye mpango wa kusajili mastaa wa dunia, ambao ni ngumu kuwafikiria kama watakwenda kujiunga na timu hizo kama ilivyo kwa kiungo Kante kumfikiria atakwenda kutinga uzi wa Washika Bunduki.
Man United hesabu kali kwa Neymar
Manchester United inampigia hesabu kali supastaa wa Paris Saint-Germain, Neymar wakicheki uwezekano wa kunasa saini yake katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, kwa mujibu wa Foot Mercato.
Kocha wa Man United, Erik ten Hag anajiandaa kupitisha fagio la kuondoa mastaa kibao kwenye kikosi chao, wasiopungua 13 wakiwamo Anthony Elanga na Anthony Martial, hivyo atahitaji sura mpya kwenye safu yake ya ushambuliaji. Kwa sasa mpango namba moja kwenye eneo la straika ni kumnasa Harry Kane, lakini pia ikimsaka Victor Osimhen na Rasmus Hojlund kama watakwama kwenye chaguo lao la kwanza.
Man United inahitaji pia kujiimarisha kwenye wingi za kulia na kushoto na hapo wamekuwa wakihusishwa na Dani Olmo na Ansu Fati - licha ya kwamba Jadon Sancho ataendelea kupewa nafasi ya kubaki kwenye kikosi hicho, wakiamini atarudi kwenye kiwango bora cha soka lake.
Hata hivyo, Sancho akiendelea kubaki Old Trafford huenda akakabiliwa na vita kali kwenye kutafuta nafasi katika kikosi cha kwanza baada ya Foot Mercato kuripoti kwamba Man United wanafuatilia saini ya Neymar, wakimtaka aje kikosini mwishoni wa msimu huu.
PSG inapanga kumuuza mchezaji huyo anayelipwa Pauni 810,000 kwa wiki mwishoni mwa msimu huu na kwa mshahara wake, Man United ndiyo timu yenye uwezo wa kumlipa hasa itakapokuwa chini ya wawekezaji wa kutoka Qatari. Neymar kwenda Old Trafford itakuwa ni moja ya usajili utakaoshtua mashabiki kama ambao utatokea Kante akitua Emirates kwenda kucheza chini ya Mikel Arteta.
Mwandishi ampeleka Messi Etihad
Supastaa, Lionel Messi mkataba wake unafika mwisho huko Paris Saint-Germain na siku za karibuni staa huyo amekuwa akihusishwa na mpango wa kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Barcelona. Lakini, mwandishi wa habari za usajili, Dean Jones anaamini kwa mshahara anaolipwa Messi wa Pauni 1 milioni kwa wiki, mahali ambako anaweza kwenda Muargentina huyo ni Etihad tu kwenda kujiunga na Manchester City kama anataka kuendelea kubaki Ulaya kucheza soka la kiushindani zaidi.
Man City mara kadha imekuwa ikihusishwa na Messi na iliripotiwa ingemnasa kabla ya staa huyo kutimkia zake PSG mwaka 2021 alipoachana na Barcelona. Kocha wa Barcelona, Xavi amemtaka Messi kurudi Nou Camp, huku makamu wa rais wa klabu hiyo ya Catalan, Rafa Yuste akisisitiza kwamba watafanya kila wanaloweza kuhakikisha mchezaji wao huyo wa zamani anarudi kwenye kikosi chao.
Hata hivyo, shida inakuja sehemu moja tu, kwenye pesa za kumlipa mshahara mchezaji huyo. Barcelona haipo sawa kiuchumi na hilo linaweza kuwapa nguvu zaidi Man City wanaomilikiwa na tajiri Sheikh Mansour kunasa saini yake. Ni kitu kinachosubiriwa kwa hamu kumwona Messi akitua kwenye Ligi Kuu England kwa kipindi hiki cha umri wake ukianza kumtupa mkono. Klabu nyingine zenye uwezo wa kugharamia dili la Messi zinazomtaka staa huyo ni za huko Saudi Arabia, hasa timu ya Al-Hilal - ambayo inataka kumvuta Messi kwenye ligi yao, akachuane na mpinzani wake wa miaka yote, Cristiano Ronaldo, ambaye anakipiga kwenye kikosi cha Al Nassr.
Mbappe kutua Anfield kwa Dola 431 milioni
Kylian Mbappe amekuwa akihusishwa na Liverpool kwa miaka mingi sana na supastaa huyo wa PSG aliwahi kusema kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kwamba anaweza kuhamia kwenye timu hiyo kwa sharti moja. Lakini, ukweli usiopingika, ukiwaacha Real Madrid nje ya PSG, timu nyingine ambayo Mbappe anahusudu kwenda kucheza basi ni Liverpool yenye maskani yake Anfield.
Mbappe aliwahi kupewa kumbatio la nguvu kwelikweli na kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp wakati timu zao zilipokutana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2018 na tangu wakati huo mara zote kumekuwa na ripoti za kumhusisha mshambuliaji huyo wa Ufaransa na Anfield. Mbappe mwenyewe aliwahi kukiri kwamba aliwahi kuzungumza na Liverpool juu ya kwenda kujiunga na timu hiyo mara mbili tofauti kabla hajatua PSG wakati huo akiwa Monaco na kipindi hiki akiwa na wababe hao wa Parc des Princes.
Bado dili hilo halijakamilika, lakini shida nyingine itakayomchelewesha Mbappe kutua Anfield ni mshahara wake anaolipwa. Mkataba wake wa sasa PSG utafika tamati 2025, lakini anaweza kubadili timu ikifika 2024, ambayo ni mwakani tu hapo. Lakini, shida inakuja sehemu moja tu, PSG itahitaji ada ya uhamisho ya Pauni 352 milioni sawa na Dola 431 milioni za Kimarekani ili kumruhusu Mbappe aondoke.
Chelsea Namba 9 wakuja ni Osimhen
Siku si nyingi, Chelsea itamtaja kocha wao mpya wa kuwaongoza msimu ujao baada ya huu wa sasa kuwa wenye misukosuko mingi. Mauricio Pochettino ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kwenda kuwa kocha kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge.
Lakini, kocha mpya atatua Chelsea akitambua jambo moja kwamba timu hiyo ina tatizo la kuwa na Namba 9 wa maana baada ya straika Romelu Lukaku kuboronga na kumtoa kwa mkopo huko Inter Milan.
Ujio wa Pochettino unaweza kuwapa nguvu kwenye mbio za kumsajili Harry Kane kutoka Tottenham Hotspur, lakini wasiwasi ni kama mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy atakubali kumwachia mchezaji wake huyo akajiunge na timu wapinzani wa ndani ya ligi moja na zaidi wa kutoka London pia. Kutokana na hilo, Chelsea wanaweza kujihamishia kwa straika wa Napoli, Victor Osimhen.
Bilionea mmiliki wa Chelsea, Todd Boehly atalazimika kufungulia pochi tena ili kulipa pesa nyingi za kumnasa Osimhen kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kama ana mpango wa kuifanya timu yake kuwa shindani kwenye Ligi Kuu England msimu ujao. Huduma ya Osimhen haitapatikana kwa gharama ndogo na kwamba Napoli wanaweza kuhitaji mkwanja unaozidi Pauni 100 milioni. Osimhen kutua Stamford Bridge ni dili jingine la uhamisho litakalotetemesha kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Spurs washajua wa kumrithi Kane
Mabosi wa Tottenham Hotspur wanafahamu wazi watakuwa kwenye wakati mgumu sana wa kumzuia straika wao Harry Kane asiondoke kwenye kikosi hicho wakati dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa. Hadi kufikia wakati huo, Kane atakuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake katika kikosi hicho cha Spurs na hapo itakuwa juu ya mabosi hao kuamua, kumpiga bei au kuendelea kubaki naye ili aondoke bure mwakani.
Tayari Kane amekuwa akihusishwa na timu kibao vigogo huko Ulaya, tena wenye uwezo wa kwenda kumpa mshambuliaji huyo fursa ya kubeba mataji kitu ambacho kwenye kikosi cha Spurs hakipo. Lakini, Spurs kwenye kujiandaa na jambo hilo wameshamtambua mchezaji ambao watakwenda kunasa saini yake ili kurithi buti za Kane na staa huyo ni straika kinda wa Brighton, Evan Ferguson.
Ferguson, hivi karibuni amesaini mkataba mpya huko Brighton, lakini miamba hiyo ya Ligi Kuu England imefanya hivyo kumwongezea thamani mchezaji wao ili ikimuuza ipige mkwanja wa maana kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kutokana na mchezaji huyo kuwindwa na timu kibao. Spurs watakuwa na upinzani mkali kwenye kunasa saini ya mrithi huyo wa Kane kwenye kikosi chao.