Yanga imekifanya kile ambacho baadhi ya mashabiki wa soka hawakuwa wakikitarajia baada ya juzi usiku kupata ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ugenini dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini na kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wawakilishi hao wa Tanzania na wametinga hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 baada ya awali kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam na sasa inatarajiwa kukutana na USM Alger ya Algeria katika mchezo wa fainali.
Yanga itaanzia nyumbani kwenye mechi hiyo ya fainali kwa mkondo wa kwanza Mei 28 kabla ya kwenda ugenini Juni 3 ambapo mshindi wa jumla atatwaa taji hilo ambalo msimu uliopita lilibebwa na RS Berkane ya Morocco iliyong'olewa mapema kwenye mechi za awali.
Kazi kubwa iliyofanywa na straika, Fiston Mayele aliyefunga bao kwanza akitumia pasi aliyopewa na Kennedy Musonda kisha naye kulipa asisti kwa Musonda kipindi baada ya kukimbia kwa kasi na mpira akimzidi ujanja beki wa Marumo kisha kutoa pasi kwa mfungaji aliyefunga kirahisi.
Kwa Musonda lilikuwa bao la tatu kwenye michuano hiyo ya Shirikisho akiwa pia na asisti nne wakati Mayele bao la juzi limekuwa ni la sita kwake na kuasisti mara tatu, lakini lilikuwa pambano la 12 kwa timu hiyo klatika michuano hiyo ya Shirikisho Afrika kuanzia play-off ilitolewa Ligi ya Mabingwa.
Katika mechi hizo 12, Yanga imepoteza mchezo mmoja tu ilipofungwa kwenye makundi ya US Monastir, lakini ikishinda michezo nane na michezo mitatu ikiisha kwa sare tofauti, lakini ikifunga jumla ya mabao 16 na kufungwa mabao matano tu.
Kutinga fainali kwa Yanga kumeihakikisha klabu hiyo kuzoa Dola za kimarekani 800,000 (zaidi ya Sh 1.8 Bilioni) na iwapo itatoboa kwa kubeba ubingwa, itawapa fursa ya kutwaa Kombe la Dola 2Milioni (zaidi ya Sh 4.7 Bilioni).
Kufika fainali za Yanga ni rekodi kwa klabu hiyo kwani katika historia yake ilikuwa haijafikia hatua hiyo, lakini imefikia rekodi iliyowahi kuwekwa na watani wao, Simba iliyocheza fainali ya Kombe la CAF mkwaka 1993.
Michuano hiyo ya CAF iliasisiwa mwaka 1992 kupitia ufadhili wa mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Mashoud Abiola ambaye kwa sasa ni marehemu kabla ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuliunganisha na Kombe la Washindi mwaka 2004 na kuzaliwa kwa michuano ya sasa ambayo hakuna klabu ya Afrika Mashariki iliwahi kufika hata nusu fainali achilia mbali fainali kama ilivyofanya mabingwa hao wa Tanzania.
Jeshi la Yanga chini ya kocha Nasreddine Nabi lina kazi wa kuwakabili Waalgeria watakaocheza nao fainali, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuwahi kuvaana nao hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho 2018 na kila mmoja kushinda mechi ya nyumbani. Yanga ilianza kwa kulazwa mabao 4-0 ugenini kisha kushinda nyumbani 2-1 na kuongoza kundi D walilokuwa pamoja.
NDOO HII HAPA
Yanga kwa sasa inahesabu siku tu kabla ya kuandika rekodi nyingine kali baada ya ile ya kutinga nusu fainali kisha kuivunja na kutinga fainali.
Kama Yanga itazitumia vyema mechi hizo za fainali, ikianzia nyumbani kabla ya kumalizia ugenini timu hiyo itabeba taji na kubwa timu ya kwanza Afrika Mashariki kufanya hivyo, lakini kuandika historia kwa timu za Tanzania kubeba kombe hilo.
Kwa aina ya wachezaji iliyonayo kuanzia Mayele aliyehusika na mabao tisa hadi sasa akifunga sita na kuasisti mara tatu, sambamba na Musonda aliyehusika na mabao saba, akifunga matatu na kuasisti nne mbali na nyota wengine kama Stephane Aziz KI, Mudathir Yahya, Khalid Aucho na Diarra Djigui ambao kwenye michuano ya CAF kwa msimu huu wamefanya makubwa wakiibeba Yanga.
Kitu cha muhimu kuhakikisha inapata ushindi nyumbani kabla ya kwenda kumalizia kazi ugenini na rekodi zinaonyesha Yanga imekuwa na matokeo mazuri bila kujali uwanja wa nyumbani ama ugenini kwani katika mechi 12 ilizocheza tangu play-off, imeshinda nyumbani mara manne na kutoka sare mbili, huku ugenini imeshinda pia nne na kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja.
HAWA NDIO USM ALGER
Wapinzani wa Yanga kwenye fainali ni USM Alger kutoka Algeria iliyoanzishwa mwaka 1937, ikiwa inashika nafasi ya tatu kwa timu iliyotwaa mataji mengi katika Ligi Kuu ya Algeria (Ligue 1) ikibeba nane ikiwa nyuma ya CR Belouzdad yenye tisa na vinara JK Kabylie yenye 14.
Kwa sasa inakamata nafasi ya saba kwenye ligi hiyo kwa msimu huu na hii ni mara ya pili kwa USM Alger kukutana na Yanga, kwani iliwahi kupambana nayo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018 ambapo katika mechi ya kwanza iliyochezwa Algeria, iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 na katika mechi ya hapa Tanzania, Yanga ikapata ushindi wa mabao 2-1.
Stade du 5 Juillet 1962 uliopo Algiers ambao unaingiza mashabiki 80,200 ndio umekuwa ukitumiwa na USM Alger kwa mechi zao za nyumbani za mashindano ya klabu Afrika.
Inapokuwa nyumbani, timu hiyo ya Algeria imekuwa ikitumia jezi zenye mistari ya rangi nyekundu na nyeusi na bukta nyeusi na inapocheza ugenini huvaa jezi za rangi nyeupe ambazo huwa na michirizi na vidoti vyeusi huku soksi zao zikiwa za rangi nyeusi ama nyeupe.
Sifa kubwa ya USM Alger ni ugumu wa kufungika pindi wanapokuwa katika uwanja wa nyumbani na kuthibitisha hilo, timu hiyo imecheza mechi 31 mfululizo za mashindano tofauti ikiwa nyumbani bila kupoteza ikishinda 22 na kutoka sare tisa huku ikifunga mabao 51 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Kocha anayekinoa kikosi cha USM Alger kwa sasa ni Abdelhak Benchikha mwenye umri wa miaka 59 ambaye amewahi kushinda taji la Ligi Kuu Algeria mara mbili akiwa na CR Belouizdad na taji moja la Ligi Kuu Tunisia akiwa anainoa Club Africain.
Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermrkt.com, thamani ya kikosi cha sasa cha USM Alger ni Euro 10.3 milioni na mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi ni beki wa kati Zineddine Belaid ambaye ana thamani ya Euro 800,000. Timu hii imefika fainali moja tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2015 na kufungwa na TP Mazembe iliyobeba taji hilo.
Beki wa kulia, Saadi Redouani mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, krosi na kujilinda ndiye mchezaji hatari zaidi katika kikosi cha USM Alger ingawa wako pia Aymen Mahious, Abderrahmane Meziane Bentahar na Abdelkrim Zouari.
Pia kuna Khaled Bousseliou mwenye mabao manne kwa sasa katika michuano hiyo akimfukukia Mayele na Ranga Chivaviro wa Marumo kadhalika kuna Zineddine Belaïd mwenye mabao matatu kwa sasa.
Rekodi zinaonyesha USM Alger haijapoteza mchezo wowote ikiwa uwanja wa nyumbani kwani katika michuano hiyo ya Shirikisho msimu huu, kwani katika play-off ilishinda 1-0 nyumbani baada ya suluhu ugenini dhidi ya Cape Town City ya Afrika Kusini.
Katika hatua ya makundi, USM Alger ilipangwa Kundi A ikiwa sambamba na Marumo Gallants ya Afrika Kusini, FC Lupopo ya DR Congo na Al Akhdar ya Libya iliyoing'oa Azam FC hatua za awali na timu hiyo ilimaliza nafasi ya pili nyuma na Wasauzi kwa tofauti ya pointi moja.
USM Alger ilimaliza na pointi 11, huku Marumo ikiwa na 12 na katika mechi zote tatu za hatua hiyo ilishinda, huku ikipoteza mchezo mmoja tu ugenini dhidi ya Wasauzi, kwani ilianza kwa kuifumua Al Akhdar kwa mabao 4-1, kisha ikainyoa FC Lupopo kwa mabao 3-0 na kuifunga Marumo kwa mabao 2-0 kabla ya kulipwa kisasi ziliporudiana. Mechi nyingine za ugenini ilitoka sare ya 1-1 kila moja dhidi ya Walibya na Wakongoman na kutinga robo fainali ambapo ilishinda nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya AS Far Rabat ya Morocco na kulala ugenini 3-2 na kuvuka kwaushindi wa jumla wa 4-3.
Nusu fainali ya kwanza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ilianza kwa kutoka suluhu kabla ya juzi usiku ikiwa nyumbani kutakata kwa ushindi wa mabao ....na kutinga fainali itakapokutana na Yanga katika mechi ya kwanza itakayopigwa Kwa Mkapa Mei 28 na marudiano Juni 3 na bingwa wa msimu atajulikana baada ya RS Berkane ya Morocco iliyokuwa watetezi kutemesha taji mapema.
Matokeo ya Yanga Shirikisho
PLAY-OFF
Yanga 0-0 Club Africain
Club Africain 0-1 Yanga
MAKUNDI
US Monastir 2-0 Yanga
Yanga 3-1 TP Mazembe
Real Bamako 1-1 Yanga
Yanga 2-0 Real Bamako
Yanga 2-0 US Monastir
TP Mazembe 0-1 Yanga
ROBO FAINALI
Rivers 0-2 Yanga
Yanga 0-0 Rivers
NUSU FAINALI
Yanga 2-0 Marumo
Marumo 1-2 Yanga
REKODI DHIDI YA USM ALGER
USM Alger 4-0 Yanga (Mei 06, 2018)
Yanga 2-1 USM Alger (Aug 19, 2018)