Ndege iliyokuwa imebeba kikosi cha timu ya wanawake ya klabu ya Arsenal iliyokuwa ikirejea kutoka Ujerumani ilipokuwa kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wolfsburg iliwaka moto wakati ikianza kuondoka siku Jumapili jioni.
Tukio hilo limetokea katika uwanja wa ndege wa Braunschweig, Wolfsburg baada ya kiumbe ndege kuingia ndani ya injini muda mfupi kabla ya kuruka na kusababisha kishindo kikubwa.
Mlipuko ulianza kutokea kwenye ndege hiyo aina ya Boeing 737 hali iliyopelekea marubani waliokuwa ndani ya ndege hiyo kuwahamisha haraka abiria, kikiwemo kikosi cha kwanza cha Arsenal, hadi mahali pa usalama.
Ikithibitisha kutokea kwa tatizo hilo Klabu ya Arsenal imesema kuwa wamerejea nyumbani salama leo mchana.
Taarifa hiyo imesema: “Ndege yetu ilipata tatizo la kiufundi kabla ya kupaa nchini Ujerumani Jumapili jioni. Kutokana na hayo, tulibaki Wolfsburg usiku kucha Jumapili kabla ya kuruka kurudi Uingereza Jumatatu mchana.
“Tungependa kuwashukuru wafanyakazi walio ndani ya ndege na walio chini kwenye uwanja wa ndege kwa usaidizi wao.”