Klabu ya Geita Gold imethibitisha kuachana na kocha wake mkuu, Ettienne Ndayiragije baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara huku ikitaja matokeo mabovu na mgawanyiko ndani ya timu kuwa ni miongoni mwa sababu zilizomuondoa Mrundi huyo.
Ndayiragije alitambulishwa Agosti 22 mwaka huu akisaini mkataba wa mwaka mmoja huku akiiongoza katika mechi saba za michuano yote zikiwemo tatu za kirafiki na nne za Ligi, ambapo mechi za kirafiki alishinda moja dhidi ya kagera Sugar, Sare dhidi ya Polisi Tanzania na Kagera Sugar huku kwenye mechi za Ligi akipoteza dhidi ya Yanga (1-0), Namungo (2-0) na sare mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Mbeya City akikusanya alama mbili.
Mmoja wa Wajumbe wa Kamati Tendaji akizungumzaa kwa sharti la kutotajwa jina alisema maamuzi ya kuachana na kocha huyo yalifikiwa jana usiku baada ya kikao cha kamati tendaji kuketi usiku huku akiweka wazi kuwa mikoba amekabidhiwa Kocha Msaidizi Felix Minziro ambaye aliipandisha daraja timu hiyo kwenda Ligi Kuu.
"Sababu kubwa ni kwamba mashabiki wanahitaji matokeo lakini pia Kocha ameleta mpasuko kwenye timu ameigawa timu na imevurugika, ameugawa uongozi na kwahiyo kamati ya utendaji imefikia maamuzi hayo ili kuinusuru timu,"
Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Geita (Gerefa) Pius Kimisha ambaye alihidhuria kikao hicho aliliambia Mwanaspoti kuwa hatua hiyo imechangiwa na tabia aliyoonyesha kwa mashabiki baada ya mchezo kwa kuanza kujibizana nao na kuwatukana na kushindwa kuomba radhi, ambapo jambo hilo limewaghadhabisha watu.
Akizungumza jana baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City kumalizika kocha huyo aliwapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kuimarika kila mechi, huku akitaka waendelee kuhimizwa na siyo kukatishwa tamaa kwani ni mapema mno huku akiwa na imani kuwa timu hiyo itakuwa na mabadiliko na mbeleni itakuwa tishio.
"Hakuna mechi rahisi na sioni timu ya kuiogopa ni suala tu la kujipanga nina imani sana na timu, maneno machache ya mashabiki hayatuteteleshi kwasababu nina imani kuna siku watakuja kunipongeza na watafurahia ushindi wa timu yao," amesema Ndayiragije.
Awali baada ya mchezo huo Mwenyekiti wa timu, Leonard Bugomola alisisitiza kuwa uongozi una imani na timu na itafanya vizuri kwani inacho kikosi kilichosheheni vijana wenye vipaji vikubwa huku akibainisha kuwa wameyasikia malalamiko ya mashabiki kuona nini cha kuongeza na ni eneo lipi linalowakwamisha.