Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndayiragije abadili gia angani Chan

D02cba7829aa38784d5fcdbaa9eb75e6 Ndayiragije abadili gia angani Chan

Wed, 27 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa timu ya taifa, ‘Taifa Stars’, Etienne Ndayiragije amesema amekuja na mbinu mpya itakayowasaidia kupata ushindi dhidi ya Guinea katika mchezo wa mwisho wa fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) yanaoendelea Cameroon.

Mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu utachezwa Uwanja wa Reunification, sawa na mchezo wa Zambia na Namibia kwani kila kikosi katika kundi lao kinahitaji ushindi ili kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Stars inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu na mpinzani wake ni kinara ikiwa na pointi nne sawa na Zambia ambaye anashika nafasi ya pili kwa idadi sawa ya pointi lakini zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na Namibia ikishika mkia bila pointi.

Akizungumza kwa njia ya mtandao jana, Ndayiragije alisema wanatarajia kucheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza ili kupata pointi tatu kwani ni muhimu.

“Mchezo utakuwa mgumu kwetu, tunakwenda kucheza na kinara wa kundi lakini kwa mazoezi tuliyofanya nimewapa mbinu ya kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza lengo ni kupata ushindi ili kusonga hatua inayofuata,” alisema Ndayiragije.

Alisema anashukuru wachezaji wanaendelea vyema na wamewasoma wapinzani wao kwenye michezo yao miwili iliyopita na kuona ni timu inayocheza kwa kasi na bora sehemu ya kiungo.

“Mfumo tutakaoingia nao nadhani utatusaidia kwa kuwa wote tutaingia kwa presha na tumetofautiana kwa pointi moja hivyo chochote kinaweza kutokea,” alisema Ndayiragije.

Stars walifufua matumaini baada ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo uliopita kwa bao 1-0 dhidi ya Namibia huku Guinea ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia.

Chanzo: habarileo.co.tz