Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndayiragije: Bahati haikuwa yetu

E594bfb58c95491893cbfcbb9b16400b Ndayiragije: Bahati haikuwa yetu

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’, Ettiene Ndayiragije amesema walipambana kwa uwezo wao ili kuhakikisha wanasonga hatua ya robo fainali ya michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) ila bahati haikuwa ya kwao.

Taifa Stars ilitolewa katika michuano hiyo inayochezwa nchini Cameroon baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Guinea juzi usiku.

Timu mbili zilizofuzu robo fainali kutoka Kundi D ni Zambia na Guinea kila mmoja akivuna pointi tano, huku Taifa Stars ikiondoka na pointi nne katika nafasi ya tatu na Namibia pointi moja.

“Tunashukuru Mungu tumemaliza salama, wachezaji wamejitahidi kupambana ila bahati haikuwa yetu, kuna mambo mengi tumeona, mwamuzi alituvunja moyo kwa kuwapa penalti wapinzani na mengine,” alisema baada ya mchezo dhidi ya Guinea.

Ndayiragije alisema licha ya kushindwa kusonga mbele kikosi chake kilionesha kuimarika kutoka mechi moja kwenda nyingine na ni timu inayokua.

Kipa wa Taifa Stars, Aishi Manula alisema walitamani kushinda na kusonga mbele ila imekuwa tofauti, wanashukuru Mungu kwa yote na ana amini wamejifunza na watafanya vizuri wakati mwingine.

“Watanzania wameona na watu wote wameona namna tulivyojitahidi kupambana ila bahati haikuwa kwetu, wenzetu nao walikuwa wakifanya kila jitihada ili kupata matokeo mazuri,” alisema Manura ambaye ametajwa kwenye kikosi cha wachezaji 11 waliofanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya fainali hizo.

Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya U20 na wale wa Simba pamoja na kocha Suleman Matola walianza safari ya kurudi nchini jana na wengine watafuata baadaye.

Wakati huo huo, serikali imesema imeridhishwa na kiwango kilichooneshwa na Taifa Stars kwenye michuano hiyo licha ya kutolewa katika hatua ya makundi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa na kusema alifuatilia michezo yote mitatu na kila mechi walionesha kubadilika.

Alisema kupitia michuano hiyo wamejifunza mengi kwani wamegundua upande wa michezo hawafanyi maandalizi ya mapema na mechi zikikaribia siku tatu wanaweka kambi jambo ambalo hawawezi kutegemea kupata mafanikio.

“Nawaambia Watanzania siri ya kushinda ni kufanya maandalizi mazuri, hata Taifa Stars walipofikia walipambana na kikubwa tunajipanga upya,” alisema Bashungwa.

Chanzo: habarileo.co.tz