Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndanda yapata ushindi wa kwanza Championship

Ndanda Pic Ndanda yapata ushindi wa kwanza Championship

Fri, 11 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Ndanda ya mkoani Mtwara leo imepata ushindi wa kwanza kwenye Ligi ya Championship msimu huu baada ya kuichakaza Gwambina FC kwa mabao 4-2.

Ndanda imepata ushindi huo mnono ugenini leo Ijumaa katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kwenye mchezo wa Ligi hiyo ambao umepigwa kuanzia saa 10 jioni.

Mchezo huo umepigwa katika uwanja huo baada ya Bodi ya Ligi kuufungia uwanja wa Gwambina Complex unaotumiwa na Gwambina FC kutokana na eneo la kuchezea kutokukidhi viwango vilivyoainishwa kikanuni.

Ndanda ambao mchezo uliopita waliilazimisha sare ya 1-1 Pamba kwenye Uwanja huo, leo imeingia ikiwa ya moto na kupata mabao ya haraka kipindi cha kwanza huku wakitawala mchezo huo.

Vijana hao kutoka Mtwara wamepata bao la kwanza dakika ya sita na Rashid Gumbo, bao la pili limefungwa na Adam Uledi dakika ya 10 na la tatu Denis Tamba mnamo dakika ya 36 huku Gwambina wakisawazisha katika dakika ya 45 kupitia kwa Rahim Shomari ambapo kipindi cha kwanza wageni walikuwa mbele kwa mabao hayo 3-1.

Kipindi cha pili Ndanda wameendelea moto waliouanzisha kipindi cha kwanza ambapo Adam Uledi amerudi kambani na kuifungia timu yake bao la nne katika dakika ya 60 huku Gwambina wakiandika bao la pili dakika ya mwisho (90) ya mchezo ambalo limepachikwa nyavuni Rahim Shomari.

Mfungaji wa mabao yote mawili ya Gwambina kwenye mchezo huo, Rahim Shomari ameyafunga kwa mtindo mmoja akitupia kwa mikwaju ya faulo ambayo imezama kambani moja kwa moja.

Kipigo hicho ni cha tatu kwa Gwambina katika Uwanja wa nyumbani msimu huu ikipoteza dhidi ya Mbeya Kwanza, Pamba na Ndanda huku ikiambulia sare na Ken Gold.

Ndanda imeimarika katika michezo hii miwili ya ugenini jijini Mwanza ikiondoka na pointi nne baada ya sare na Pamba na ushindi mbele ya Gwambina ambapo inafikisha pointi pointi sita na kukamata nafasi ya 14 akipanda kutoka ya 15.

Baada ya kipigo hicho, Gwambina inashuka kwa nafasi moja kutoka ya 14 hadi ya 15 akibaki na pointi zake nne baada ya kucheza mechi tisa za ligi hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti