Beki wa kati wa Ruvu Shooting, Frank Nchimbi amesema licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1, lakini amechekelea kumtibulia straika Fiston Mayele na kushindwa kufunga bao dhidi yao ikiwa ni rekodi mbovu kwa nyota huyo wa Jangwani dhidi ya timu hiyo.
Mayele aliyemaliza msimu uliopita na mabao 16 akishika nafasi ya pili ya ufungaji mabao nyuma ya George Mpole wa Geita Gold, hajawahi kuitungua Ruvu Shooting sambamba na Tanzania Prisons na katika mechi ya juzi alikwama tena, huku Nchimbi akijisifia kwa kumdhibiti mwanzo mwisho.
Ruvu ikicheza kwenye ubora wake juzi, iliangukia pua kwa kulala na kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Yanga, huku beki na nahodha huyo akifanya kazi ya maana kwa kudhibiti mashambulizi mengi. Timu hiyo inatarajia kurudi uwanjani tena kesho Ijumaa kuikabili KMC, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ukiwa wa raundi ya saba kwa timu hizo.
Nchimbi alisema walipambana kadri ya uwezo wao lakini walishindwa kufikia malengo yao ya kuchukua alama tatu, huku akikubali kazi aliyoifanya kumdhibiti Mayele. Alisema kabla ya mchezo benchi la ufundi liliwapa maelekezo ikiwamo kuwa makini na straika huyo mwenye mabao matatu ya Ligi Kuu msimu huu na mengine sita ya michuano ya Afrika yote akifunga dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini na kumfanya aingie katika kinyang’anyiro cha tuzo ya mwezi ya CAF.
“Tuliambiwa kuwa makini na Mayele ila nashukuru kazi aliiona na pia nafikiri hatausahau mtiti wangu,” alitamba Nchimbi na kuongeza;
“Nikiangalia timu yangu ni kama wote tuko imara, kimsingi ni kupambana kila mchezo bila kujali Simba na Yanga kuhakikisha tunafanya vizuri na kumaliza ligi kwenye nafasi nne za juu.”