Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchi itasimama, all the best wanetu

Yanga Sauziiiiiiiii Nchi itasimama, all the best wanetu

Wed, 17 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania yote itasimama kwa dakika 90 kuanzia saa 1:00 usiku huu, kuitazama Yanga ikikabiliana na Marumo Gallants mjini hapa. Hata Simba watakuwa kwenye runinga zao kuitazama Yanga ikisaka rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho.

Yanga ambayo ilishinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Jijini Dar es Salaam, ndiye klabu pekee ya Afrika Mashariki na Kati iliyosalia kwenye michuano ya kimataifa. Klabu zote kubwa unazozijua zilishatolewa kitambo, lakini Yanga bado wanatetea heshima ya Tanzania wakitamba na jina lao ya Wananchi.

Yanga inasaka rekodi mpya ya kuwa klabu pekee ya Tanzania kucheza kwa mara ya kwanza fainali za Shirikisho zitakazopigwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini Mei 28 na Juni 3.

Morali ya Yanga iko juu ndani na nje ya Uwanja wa Royal Bafeng wanakokwenda kukiwasha usiku huu mbele ya mashabiki ambao wataingia bure kutokana na wenyeji kutoa viingilio kuvutia mashabiki wengi ambao hata hivyo hawana mzuka na timu yao.

HESABU ZA VIDOLE

Matokeo ya Dar es salaam yanawapa presha kubwa wenyeji. Yanga inahitaji sare, suluhu, ushindi au hata kufungwa mabao 3-1 ili isonge kwa madaha kwa ajili ya fainali hiyo na wataanzia Dar es Salaam na mshindi kati ya Asec Memosas na US Algiers.

Hata hivyo, rekodi za Yanga kuwa na uwezo wa kupata ushindi au mabao ugenini ndio vinawatisha zaidi Marumo ambao kocha wao wa muda, Dylan Kerr hana rekodi ya kuifunga Yanga tangu akiwa na Simba.

BARIDI LAKINI FRESHI

Yanga ambayo viongozi wake wote wapo hapa, haijaridhika na ushindi huo na kuthibitisha hilo juzi walifanya mazoezi yao ya kwanza uwanjani na licha ya baridi kali haikuwazuia wachezaji wa timu hiyo kujituma zaidi wakiwa na hamasa kubwa uwanjani.

Kikosi hicho kilitumia uwanja wa hoteli yao ya kisasa yenye Hadhi ya nyota tano Royal Marang kujifua Uwanja ambao ulitengenezwa na timu ya Taifa ya England walipotumia hoteli hiyo kwenye Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini hapa mwaka 2010.

Hatua ya Yanga kufikia hoteli hiyo imewashtua mashabiki wa Marumo na viongozi wao waliodhani wasingeweza kumudu kutumia hoteli ya namna hiyo kutokana na gharama zake. Marumo hawako vizuri kiuchumi na hivi karibuni viongozi wao walizuiwa Libya ilikokwenda baada ya kushindwa kulipa bili.

Hali ya hewa ya jijini Rustenburg ndio changamoto pekee ambayo sio tu Yanga watakabiliana nayo, bali hata wenyeji wao Marumo kwani nao sio eneo ambalo wamekuwa wakiishi wakienda hapo kwa ajili ya mchezo huo pekee ingawa Yanga ndio watakuwa na kazi nayo.

Baridi hiyo inayofikia sentigredi 7-8 majira ya usiku haikuwazuia wachezaji kuonyesha ubora wao wakiwa tayari wamenunuliwa mavazi ambayo yatawaongezea uimara wa kukabilia na hali ya hewa hiyo.

NABI MABEKI, KAZI FOWADI

Kazi kubwa iliyofanyika juzi ni, makocha hao waliigawanya timu hiyo katika makundi matatu na Kocha Mkuu Nasreddine Nabi alikuwa akiwafua mabeki wake wote huku msaidizi wake Cedric Kaze akibaki na washambuliaji wakati, Khalil Ben Youssef ambaye kitaaluma ni kocha, pia akiwa mtaalam wa kuchambua mikanda ya timu za wapinzani akibaki na viungo wa kati.

Kila idara ilikuwa inapewa mbinu na hesabu za kutekeleza majukumu yao uwanjani hatua ambayo iliwapa faraja mabosi wa Yanga waliokuwa nje ya uwanja wakifuatilia mazoezi yao.

VIONGOZI NA MASHABIKI

Ukiondoa wajumbe wa baraza la wadhamini, ni mjumbe mmoja pekee wa kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye hayupo hapa, wengine wote wapo.

Anzia kwa mwezeshaji wa Yanga Ghalib Said Mohamed, Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said, makamu wake Arafat Haji na wajumbe wao Yanga Makaga, Munir Said, Alexander Ngai, Mbunge wa Manonga, Seif Gullamali, Ofisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine wako hapa. Jana jioni walitarajiwa vigogo wengine kuongezeka zaidi.

Uwepo wa jopo hilo umekuwa hamasa kubwa kwa timu yao na mara ya mwisho kundi kama hilo kusafiri Yanga iliichapa TP Mazembe kwao.

Marumo haina mashabiki wengi hapa mjini Rustenburg na baadhi watatoka miji mingine ambao bado ni wachache lakini Yanga itashuka na jeuri kutokana na Watanzania wanaoishi nchini hapa na wengine waliosafiri kwa wingi kuonekana kuanza kuwafunika wenyeji wao kwa mbwembwe nyingi.

MECHI YA MKWANJA

Hii ni mechi yenye vita nyingine ya fedha kwani Marumo tayari wanafahamu wako katika hali ngumu ya kubaki ligi Kuu ya hapa kwao, lakini kuna tajiri amewawekea mzigo mezani wa Sh400 milioni pamoja na ahadi zingine kama wataitoa Yanga.

Hata hivyo, taarifa hizo zimemfikia muwekezaji wa Yanga, Ghalib Said (GSM) ambaye alishaweka mezani ahadi ya Sh300 milioni na alitarajiwa kutoa sapraizi nyingine kwenye kikao na wachezaji jana usiku.

KOCHA NABI

Kocha Nabi ameliambia Mwanaspoti lililoweka kambi hapa, wanakwenda kucheza mechi ngumu pengine yenye ugumu kuliko mechi zote zilizopita dhidi ya Marumo na hata kwenye mashindano haya.

Nabi alisema wamechukua tahadhari zote kwa kuwapa mbinu zote muhimu wachezaji wao na watashuka na kikosi chenye mabadiliko machache huku akithibitisha kwa mara nyingine Yanga haitopaki basi kwa kutumia mbinu za kujilinda zaidi.

Nabi alisema amewataka wachezaji wao kuiheshimu Marumo ambao lazima watakuja na presha kubwa ya kutaka kusawazisha mabao hayo huku akiwataka wachezaji kucheza kwa nidhamu kubwa ya kujituma wakati wakimiliki mpira na wakati hawana mpira.

"Hii ndio fainali kwetu, tunakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Marumo akili yangu inaniambia hizi ni dakika 90 ngumu kuliko zote ambazo tumewahi kuzicheza tangu nifike hapa Yanga," alisema Nabi.

"Kitu kizuri tunatakiwa kuiheshimu Marumo, hii ni timu ambayo ina nguvu kubwa inapokuwa nyumbani, hawajawahi kufungwa hapa wala kuzuiwa kwenye mashindano haya ya CAF.

"Tunatakiwa kucheza kama wanajeshi tujue jinsi ya kufanya jukumu la kukaba kwa pamoja lakini tucheze kwa haraka kufika langoni kwao na kumalizia nafasi vizuri," alisema Nabi huku akisisitiza atatumia ujanja wake wote kupata matokeo. Nabi anasifika kwa mabadiliko ya kipindi cha pili ambayo yamekuwa na madhara makubwa kwa timu pinzani.

WAAMUZI:

Mutaz IBRAHIM-Kati(Libya)

Attia AMSAAED-Msaidizi 1 (Libya)

Khalil HASSANI- Msaidizi 2 (Tunisia)

KIKOSI KINAWEZA KUWA HIVI;

Diarra, Job, Kibwana, Mwamnyeto, Bacca,

Aucho, Bangala, Aziz, Moloko, Mayele na

Mzize.

Chanzo: Mwanaspoti