Uzee wa Saido Ntibazonkiza ni ‘uzee wa busara’. Utu uzima dawa. Ni ile maana halisi ya hakuna kijiji kinachokosa wazee.
Ligi yetu bado ina maajabu kidogo. Wachezaji wazee wanacheza vizuri na wanafunga sana kuliko vijana.
Ni kweli soka letu linakua na tumeanza kupata wachezaji wengi bora licha ya kutoondoa ukweli, umri sio kigezo cha kumzuia mchezaji asicheze.
Ligi yetu hata kama una babu yako aliwahi kuupiga, anaweza kusajiliwa Kariakoo na bado akaupiga mwingi tu.
Kabla ya mechi za mwisho za ligi yetu, kulikuwa na wachezaji watano tu walifikisha kuanzia mabao 10 msimu huu. Aziz KI, Feisal Salum, Wazir Jr, Maxi Nzengeli na Saido.
Katika orodha hiyo, kuna jina la Saido. Ndiye kinara wa mabao wa msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara na msimu huu akiwa amefikisha 10 kabla ya mchezo wa jana dhidi ya JKT Tanzania wa kumaliza msimu.
Saido ni mmoja ya wachezaji wanaiotwa ‘wazee’ kwenye ligi yetu, lakini bado kwenye orodha ya wafungaji bora jina lake halikosekani. Ligi yetu ina vijana wengi sana lakini bado wazee ndio tishio.
Nimesikia kelele za baadhi ya mashabiki wa simba wakitaka Saido aachwe msimu ujao.
Huenda wana hoja ya msingi na wanaitakia mema timu yao, lakini ukweli utabaki pale pale, nyota huyo wa kimataifa wa Burundi bado ana uwezo wa kufunga.
Pengine kiu ya mashabiki wa simba ni kupata mchezaji anayeweza kuwapa mabao 20 kwa msimu na kuona mchezaji mpya Kikosi.
Hata hivyo, moja ya kazi ngumu kwenye ligi yetu ni kupata mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao 20 au zaidi kwa msimu.
Yanga bado hawajampata mshambuliaji mwenye uwezo huo tangu aondoke Amis Joslyn Tambwe, kama ilivyo kwa Simba tangu aondoke Meddie Kagere.
Mshambuliaji bora kwenye ligi yetu ni yule anayeweza kukupa walau mabao 10 kila msimu. Kabla ya mzunguko wa mwisho, kulikuwa na wachezaji watano tu walifikisha idadi hiyo. Saido ni miongoni mwao.
Ni rahisi sana kutoona mchango wake kwa Sababu tu timu imeshindwa kufikia malengo yake lakini ukweli unabaki pale pale, pamoja na umri wake kusonga, bado ni mshambuliaji anayekupa uhakika walau wa mabao 10 ya ligi kila msimu.
Katika misimu miwili, ndiye mfungaji bora wa Simba. Hakuna aliyefunga mabao mengi zaidi yake kwa Wekundu hao wa Msimbazi.Namba hazidanganyi.
Kwa aina ya ligi yetu, bado anaweza kucheza kwa misimu mingine hata miwili na kukupa uhakika wa mabao walau 10 kwenye ligi kila msimu.
Ligi yetu ina wachezaji wengi sana wenye umri mdogo lakini hawapo kwenye tano bora ya wafungaji. Jina la Saido lipo kila msimu. Huyu sio mchezaji wa kumwacha. Ni mali kwenye ligi yetu.
Ana uwezo mkubwa sana wa kuendelea kufunga. Anakupa uhakika walau wa mabao 10 kila msimu. Ni wachezaji wachache sana wanaweza kufunga kama yeye kwenye ligi yetu. Kupata mshambuliaji mwenye uwezo wa kukupa mabao 20 sio shughuli ndogo.
Fiston Mayele alikuwa mshambuliaji mzuri sana misimu mwili iliyopita lakini hakuwahi kufikisha mabao 20 kwa msimu. Alitetema sana enzi zake lakini hakufikisha 20 licha ya kucheza kwenye Kikosi bora. Tuwaheshimu sana wachezaji wanaoweza kufikisha walau mabao 10 ya ligi kila msimu huu. Kwa Saido, bado umri ni namba tu. Anawazidi vijana wengi tu kwa upachikaji wa mabao.
Usajili ni kamari. Unaweza kusajili mchezaji mzuri huko alikotoka lakini akaja kufeli kwenye mikono yako.
Willy Somba Onana hakuwa mchezaji mbaya huko alikotoka lakini amekuwa na wakati ngumu msimu wake wa kwanza Simba.
Hali kama hii ni kawaida sana kwenye soka. Hata Aziz KI alikuwa na wakati ngumu sana msimu wa kwanza lakini msimu huu amekuwa mfalme wa Jangwani.
Ni hali ya kawaida kabisa. Simba inaweza kusajili mchezaji mwingine kwenye eneo la ushambuliaji lakini ikabaki na Saido kama chaguo la pili. Ukipata mshambuliaji bora wa kukupa mabao 15 kwa msimu na Saido akakupa 10, tayari una mtaji wa mabao 25.
Saido bado anaweza kukupa mabao 10 za uhakika kabisa. Ni aina ya wachezaji ambao hata akitokea benchi ana uwezo wa kubadili matokeo na ana uwezo mkubwa wa kufunga kupitia mipira ya kutenga. Tuna wachezaji wachache sana kwenye ligi yetu wenye uwezo huo.
Pamoja na umri wake, lakini bado namwona akifanya vizuri kwenye ligi yetu. Watu kama kina Khalid Aucho ni ‘wazee’ lakini hakuna kijana anayewafikia. Bahati mbaya kwenye soka ‘uzee’ unaanzia miaka 30. Ndiyo mchezo pekee ambao ‘uzee’ wake uko karibu.
Aucho sio juzi wala jana. Ni mchezaji wa miaka mingi. Alishapita kwenye kila vita ya uwanjani lakini bado anaupiga mwingi Jangwani. Anapokosekana unaona kabisa hakuna wa kuziba pengo lake. Umri bado sio kigezo.
Ni kweli Simba inaweza kuachana na Saido lakini natamani ingempa hata mkataba wa mwaka mmoja. Ni kweli inatajwa kutafuta mshambuliaji mpya, ni wazo zuri sana lakini bado inaweza kubaki naye kama chaguo namba mbili.
Jean Baleke ameondoka Simba tangu dirisha dogo, lakini kabla ya mechi za mwisho aliyempita kwa mabao ni Saido pekee. Inafikirisha kidogo.
Huenda Baleke angekuwa hata na mabao 15 muda huu na kuwa mfungaji bora msimu huu kama angebakia Simba. Hii ndiyo hali halisi ya soka letu.
Bado hakuna washambuliji wa uhakika. Mchezaji anaweza asicheze nusu msimu na bado hakuna wa kumpiku kwa mabao. Ukipata mshambuliaji mwenye uwezo wa kukupa mabao 10, usimchezee. Mtunze. Huyo ni mali.
Najua viongozi wa Simba wanataka kuwafurahisha mashabiki wao kwa kuleta wachezaji wengi wa Kigeni, lakini unahitajika umakini mkubwa.
Ugeni sio tatizo. Shida kubwa ipo kwenye ubora. Simba imekosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo lakini haikuwa mbaya kiivyo, haijitaji usajili mkubwa, inahitaji usajili makini.
Nadhani eneo ambalo imeshindwa kutamba sana misimu ya hivi karibuni ni kukosa jicho zuri kwenye usajili. Matokeo yake wamesajili sana na kuacha sana.
Sina dhamira ya kuipangia Simba, lakini Saido anawapa uhakika wa mabao 10 ya ligi ya kuanzia msimu. Najua soka ni mchezo wa wazi na wa maoni. Unamuonaje Saido?
Unaweza kututumia maoni yako na tutayaheshimu sana. Kama Mnyama atapata mshambuliaji wa juu kabisa ni vyema kumleta lakini Saido anaweza kubaki kama chaguo la pili na bado akaisaidia timu. Uzee wa Saido ni uzee wa busara. Ni utu uzima dawa. Ni ile maana halisi ya hakuna kijiji kinachokosa wazee.