Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nauona msimu huu ukikumbwa na mgogoro ratiba Ligi Kuu

Simba Mtibwa Sds Nauona msimu huu ukikumbwa na mgogoro ratiba Ligi Kuu

Thu, 7 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 2023/24 wa Ligi Kuu Bara ulianza Agosti 15 na hadi mwezi huo unaisha, mizunguko miwili tayari imechezwa.

Pia mwezi huu kunaweza kuwa na mzunguko miwili tu na Oktoba kukawa na mizunguko isiyozidi miwili, kisha Januari kutakuwa na Kombe la Mapinduzi.

Nasema ‘kunaweza kuwa’ kwa sababu kuna mechi ambazo hazijapangiwa tarehe. Hii ina maana kuanzia Agosti msimu ulipoanza hadi Januari, yawezekana ligi ikawa imechezwa robo moja tu.

Ikiwa hivyo, maana yake kuanzia Februari tutaanza safari ya kuzimalizia robo tatu zilizobaki tukitarajia msimu uishe Mei, kisha Juni mwanzoni ifanyike fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam. Hapo ndipo kwenye hofu yangu. Kumaliza robo tatu za mechi za msimu ndani ya miezi mitatu maana yake kutakuwa na kukimbizana sana kwenye ratiba.

Hapo isitokee klabu zinazoshiriki kimataifa zikafika hatua za mbali kwenye mashindano hayo. Msimu utachelewa zaidi kuisha. Matatizo haya yalianza kujionyesha mapema hata kabla ya msimu haujaanza.

Ratiba ya ligi ilitoka wiki moja kabla ya tarehe iliyopangwa kuanza kwa msimu. Ilitoka Agosti 7 na ligi ilianza Agosti 15. Bodi ya Ligi walikaa muda mrefu kutengeneza ratiba, tukadhani watakuja na ratiba bora, lakini wapi.

Ratiba ikaanza kuonyesha udhaifu tangu mwanzo wa msimu. Kagera Sugar kupangiwa mechi mbili ndani ya siku tatu katika viwanja vyenye tofauti ya umbali wa kilomita zaidi ya 1000, ni udhaifu mkubwa wa ratiba. Pata picha mechi za mwisho za ligi zilichezwa kuanzia Agosti 19 hadi 31, ligi ikasimama bila sababu yoyote ya maana zaidi ya blahblah.

Kalenda ya Fifa inasema kutakuwa na mechi kati ya Septemba 4 hadi 12. Tanzania itacheza na Algeria keshokutwa, Septemba 7. Kutoka Agosti 31 kungeweza kuwa na mechi angalau moja hapo kati kabla ya mechi ya Taifa Stars. Lakini Bodi ya Ligi wanakubali kusimamisha ligi kwa sababu ya kuipa muda wa kutosha wa kujiandaa Taifa Stars. Hapa kuna vitu viwili. Kwanza, bodi inaithamini Taifa Stars kuliko ligi? Kwa nini inapanga ratiba zenye muda finyu kwa klabu bila kujali kuzipa muda wa kujiandaa, lakini inaipa Taifa Stars?

Pili, hivi Bodi ya Ligi haijui wao siyo jukumu lao Taifa Stars? Timu ya Taifa ni biashara ya TFF na wanatakiwa waisimamie timu yao bila kuathiri wengine. Timu ya taifa ni ya TFF na ligi ni ya Bodi ya Ligi. Timu ya taifa ikifeli majibu watatoa TFF. Ligi ikifeli majibu watatoa Bodi ya Ligi.

Lakini Bodi ya Ligi iko radhi kutafuta majibu ya Taifa Stars kuliko majibu ya ligi. Maajabu sana. Ilishindwaje kuahirisha mechi ya Kitayosce na Azam FC kutokana na matatizo ya klabu hiyo changa? Hawaoni kama waliitia dosari kubwa ligi yetu?

Katika muda wote huu wa mapumziko haya ya timu za taifa au ya mashindano ya klabu, mechi si ingechezwa tu? Kulikuwa na haja gani ya kutopanga tarehe ya mechi ya Simba na Coastal Union? Timu hizi mbili zilicheza mechi za mwisho Agosti 20. Zingeweza kucheza mechi yao Kati ya Agosti 25 hadi 31, lakini Bodi ya Ligi haikuona umuhimu. Inaruhusu viporo visivyo na sababu na kulazimisha mechi zilizostahili kuahirishwa.

Mechi ya Ihefu na Kagera Sugar pamoja na ile ya Azam FC na Kitayosce zilistahili kuahirishwa. Sasa tunasubiri kuona kama kutakuwa na mechi za ligi katikati ya mapumziko ya Fifa na CAF. Ligi ambayo imeshachezwa raundi mbili tu tayari ipo kwenye hali ya sintofahamu, vipi huko mbele?

Msimu uliopita ligi iliisha Juni 9 na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ikafanyika Juni 12. Msimu huu inaweza inavuka hapo. Ligi inaweza kumalizika mwishoni mwa Juni na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ikafanyika Julai mwanzoni. Na kama itakuwa hivyo, tutakuwa tumejiharibia kabisa mipango ya maandalizi ya msimu unaofuata.

Maana yake timu zitakosa muda wa kutosha wa maandalizi ya kabla ya msimu...tutakuwa tunarudi nyuma badala ya kusonga mbele. Kushindwa kujiandaa ni kujiandaa kushindwa. Bodi ya Ligi ilishindwa kujiandaa vizuri kwa Kutoa ratiba bora, matokeo ikashindwa kutoa ratiba bora na sasa tunaelekea kuzama.

Kuanzia Februari, mvua zinaanza kunyesha na kusababisha usafiri kuwa mgumu, halafu ratiba ndiyo iko ‘taiti’, mechi moja baada ya siku tatu kwa umbali wa kilomita zaidi ya 1000 kwa jiografia ya nchi yetu...kazi ipo!

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: