Usiku wa deni haukawii kukucha, ndivyo unavyoweza kusema kwani hatimaye kivumbi cha mashindano ya kimataifa yaani Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kimeanza kutimua vumbi rasmi Ijumaa na kinatarajiwa kuendelea wikiendi hii.
Kwa upande wa Tanzania Bara msimu huu tunatarajiwa kushirikisha timu nne katika mashindano hayo, ambapo timu za Yanga na Simba zinatarajiwa kutuwakilisha katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC na Singida Fountain Gate zikituwakilisha kwenye Kombe la Shirikisho.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wao wana faida ya kuanzia hatua ya kwanza, hivyo ni watani zao wa jadi Yanga ambao wataanzia hatua hii ya awali ambapo karata yao ya kwanza itakuwa kuvaana na AS Ali Sabieh Djibouti Télécom (ASAS), ya Djibout ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza utapigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Hapa tunakuletea dondoo muhimu za mchezo huu kama ifuatavyo, Ugenini kama nyumbani, nyumbani ni nyumbani tu Kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita dhidi ya Zalan, Yanga msimu huu pia wamepata mteremko wa michezo yao yote miwili ya hatua ya awali kupigwa kwenye ardhi ya Tanzania kutokana na maombi ya Zalan ambao wameomba kutumia Uwanja wa Azam Complex, kama Uwanja wao wa nyumbani.
Kwa wapenzi wa ngumi hii inaweza kuwakumbusha ule usemi wa bondia maarufu, Karim Mandonga ambaye aliwahi kusema yeye akipigwa kama amepiga, na akipiga ndo amepiga. Hivyo kwa Yanga ugenini kama nyumbani, na nyumbani ni nyumbani tu.
Nani kuvunja rekodi ya Mayele? Msimu uliopita kwenye kikosi cha Yanga bao la kwanza kwenye mashindano ya kimataifa lilifungwa na aliyekuwa straika wao mkongomani, Fiston Kalala Mayele akitumia asisti matata ya Denis Nkane dakika ya 45 ya mchezo ambao ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 huku Mayele akifunga Hat-trick.
Kwa sasa Mayele hayuko ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kukamilisha uhamisho wa kujiunga na Pyramid FC ya Misri. Ukiachana na straika Mzambia, Kennedy Musonda Yanga imesajili straika mpya, Hafiz Konkon na swali kubwa ni je, nani atavunja rekodi ya Mayele? Ikumbukwe, Mayele pia msimu uliopita alimaliza akiwa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akiweka kambani mabao saba na kumzidi Ranga Chivaviro.
Rekodi zinawabeba Yanga Licha ya kwamba wamekuwa na rekodi mbovu ya zaidi ya miaka 20 kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini katika mizania Yanga wanaonekana kuwa kwenye faida kubwa ya rekodi nzuri za ushiriki wao kimataifa kulinganisha na wapinzani wao.
Mafanikio makubwa ya Yanga katika mashindano ya kimataifa ni kuibuka washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika, rekodi ambayo wamefanikiwa kuipata msimu uliopita ambapo waliukosa ubingwa wa mashindano hayo kutokana na faida ya kanuni ya bao la ugenini.
Kwa upande wa ASAS ambao licha ya kwamba hakuna taarifa nyingi kuwahusu kwenye mtandao lakini ni inaonekana hawana rekodi yoyote ya kuweza kucheza hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa japo kwa nyakati kadhaa wamefanikiwa kutawala soka la ndani na kushinda ubingwa wa Ligi Kuu.
Yanga wanasemaje? Kuelekea mchezo huo dhidi ya ASAS, Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe: “Nadhani mchezo huu utakuwa mgumu zaidi kwetu kulinganisha na michezo ya Ngao ya Jamii kwa kuwa hatuna taarifa nyingi kuwahusu wapinzani wetu.
“Tutahitaji kuwajibika zaidi kwenye mchezo huu na kusahau kuhusu Ngao ya Jamii ili kutimiza malengo ya kufuzu hatua inayofuata.”