Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nani Ramos? Huyu mwamba ana kadi nyekundu 46

Ekgqg77XgAAeO14 Nani Ramos? Huyu mwamba ana kadi nyekundu 46

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kati ya mambo yanayopewa umuhimu mkubwa katika michezo ni urafiki, maelewano, uvumilivu na nidhamu.

Lakini tunachokiona kupewa umuhimu ni ushindi tu huku mengine yakibaki kuangaliwa kama kachumbari tu, yaani sio muhimu sana.

Hii pia inajitokeza katika vyombo vya habari kwa kutoa sifa kwa wachezaji mashuhuri wanavyolinda kwa ustadi nyavu zao na kutikisa za wenzao, kupiga chenga za mwili na wanavyofyatua makombora ya kasi.

Utovu wa nidhamu na ukorofi wa kurusha mateke, kutumia lugha chafu, kutafuna au kutemea mate na kuwafanyia wachezaji wengine vitendo vilivyokosa utu, havipewi umuhimu.

Vitendo hivi vimepungua kutokana na kuwepo kwa kamera za kisasa zinazonasa vizuri kila linalotendeka uwanjani kuliko macho ya waamuzi na wasaidizi wake wa pembeni.

Leo nitazungumzia baadhi ya wakorofi wakubwa na zawadi za kadi walizopewa kwa mchezo mchafu.

Kama patatolewa zawadi ya mchezaji mtata, jeuri na mkosefu wa nidhamu halafu akitokea mmoja katika jopo la majaji ambaye hatamchagua Gerardo Alberto Bedoya Munera wa Colombia itakuwa ajabu.

Mchezaji huyu mstaafu ambaye sasa ana miaka 48 na aliwahi kuwa meneja wa timu ya Colombia ambaye anajulikana zaidi kwa jina la ‘Beast’ (Mnyama) alikuwa katili na jeuri kupita kiasi.

Siku moja alipokuwa anacheza na watoto ili kuwaonyesha mchezo mzuri alijisahau na kuwarukia kuwapiga mateke kama vile alikuwa anacheza na watu wazima.

Aliwaumiza watatu katika kipindi cha dakika 5 na akaombwa atoke nje na alipokuwa anatoka aliporomosha matusi ya ajabu.

Bodeya alianza kucheza kama mlinzi na baadaye kama kiungo, lakini siku zote alikuwa akirusha mateke na matusi mwanzo hadi mwisho wa mchezo.

Hii ilimpelekea kupata kadi nyekundu 46, kiwango kikubwa katika historia ya mchezo huu na hakijafikiwa na mchezaji yeyote wa michezo ya kimataifa. Kadi za njano alizopewa ni zaidi ya 400. Sasa kama ulikuwa unamshangaa beki Sergio Ramos kuonyeshwa kadi nyekundu mara 26, basi huyu mwamba Bodeya ndio baba lao.

Siku moja bada ya mchezo kumalizika kule kwao Colombia bila ya kuonyeshwa kadi alimwendea mwamuzi na kumwambia alimkasirisha kwa kutomtendea haki.

Mwamuzi alishangaa na kumuuliza lipi lilimkasirisha na Bodeya alimwambia alimnyima chakula anachokipenda. Nacho ni kupata angalau kadi ya njano.

Bedoya alianza kuwa mchezaji wa kulipwa kwa kujiunga na klabu ya Deportivo Pereira mwaka 1996 na kuchezea Deportivo Cali ambayo ilikuwa klabu bingwa ya Colombia mwaka 1998.

Katika mwaka 2001, bada ya kuona hatakiwi na klabu za Colombia kutokana na mchezo wake mchafu aliamua kwenda Argentina na kuichezea klabu ya Racing Club de Avellaneda.

Huko pia alitimuliwa kutokana ma mchezo wake uliosababisha mara nyingi timu hiyo kucheza na watu 11 au kupigiwa mipira ya adhabu.

Hata hivyo, alibakia Argentina na kwanza aliichezea klabu ya Colon de Santa Fe na baadaye Boca Juniors, lakini aliichezea michezo mitatu na katika miwili alipewa kadi za njano na mmoja kadi nyekundu.

Kwa vile alikuwa hataki kujirekebisha akatimuliwa na ndipo alipofunga safari ya kwenda Mexico na kupokewa na klabu ya Puebla F.C. kwa kutoa ahadi kwamba atabadilika.

Mambo yakawa yale yale kwa Bedoya na alipoona kila klabu ilikuwa haimtaki kutokana na kupenda kucheza rafu, aliamua kurudi Colombia mwaka 2005 na kuichezea Atletico Nacional na baada ya kutuwakana viongozi wa klabu alitumuliwa na kujiunga na klabu ya Millonarios mwaka 2006.

Hapo pia hakutulia na akaenda kuzichezea klabu nyingine, kwanza Envigado F.C, baadaye Chico FC katika mwaka 2010.

Licha ya rekodi hii mbaya katika klabu zote alizochezea bado ustadi wake wa mchezo ulitumika kama kigezo cha kumuita katika timu ya taifa ya Colombia mwaka 2000.

Alicheza vizuri na kufunga bao katika mashindano ya Gold Cup (Kombe la Dhahabu) katika pambano lao dhidi ya Jamaica katika dakika 81 na kufanya matokeo 1-1.

Lakini katika dakika ya 89 alifanya mambo yake ya kumrukia mchezaji kwa miguu yote miwili na kupewa kadi nyekundu.

Alikaa nje michezo miwili na Colombia ilipofanikiwa kucheza fainali dhidi ya Marekani Bodeya aliingia uwanjani na kupewa kadi nyekundu dakika moja kabla ya kumalizika muda wa nyongeza baada ya timu hizi kuwa sare ya 1-1.

Colombia ilifanikiwa kubeba kombe baada ya timu hizi kwenda kwenye matuta huku Bodeya akiwa nje ya uwanja.

Wakati wachezaji walipokuwa wamekabidhiwa kombe na kuzunguka nalo uwanjani kwa furaha Bodeya alikwenda kujiunga nao na mmoja wa wachezaji wenzake alikwenda kuichukua kadi nyekundu ya mwamuzi na kumwonyesha Bodeya.

Hee, hicho ndicho alichukuwa anakitaka. Aliwasukumia makonde wenzake na kubebwa juu kwa juu na askari polisi kwenda kituoni.

Bodeya pia alikuwamo katika kikosi cha Colombia kilichobeba Kombe la Copa America 2001 kwa kucheza michezo mitano bila ya kupewa kadi, jambo ambalo liliwashangaza watu wengi.

Tokea wakati ule akabadilika na kuwemo katika kikosi cha Colombia cha kugombea tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za 2006, lakini hakuitwa kushiriki mashindano ya 2007 Copa Amarica.

Mchezo wake wa mwisho na timu ya Colombia ulikuwa Aprili 1, 2009 pale walipofungwa 2-0 na Venezuela.

Baada ya kustaafu alikuwa kocha msaidizi wa Santa Fe na kufukuzwa siku chache tu baadye kutokana na kuwatukana wachezaji bila ya sababu.

Huyo ni kiumbe aliyekubuhu kwa rafu na lugha chafu na hadi leo rekodi za Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (FIFA) halijashuhudia mchezaji aliyemkaribia Bodeya kwa kadi nyekundu.

Chanzo: Mwanaspoti