Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namungo yazidi kupotea kimataifa

B422165c2dd022d2c8d784c093fe369b.jpeg Namungo yazidi kupotea kimataifa

Mon, 5 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Namungo FC wamejikuta wakipoteza mchezo wa tatu mfululizo baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Nkana FC ya nchini Zambia nyumbani kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Bao pekee la Nkana lilifungwa dakika ya 68 na mshambuliaji Diamond Chikwekwe akimalizia vyema pasi ya mlinzi wa kushoto wa timu hiyo, Kakuta Chimwemwe. Kwa matokeo hayo Namungo wameshushwa hadi mkiani mwa kundi D wakiwa hawana pointi.

Mchezo huo wa kundi D ulikuwa unazikutanisha timu zilizo chini ya msimamo, wenyeji Namungo walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Nkana FC lakini shuti la Lucas Kikoti lilienda nje, dakika sita baadaye Steven Sey alikosa bao la wazi akiwa yeye na kipa.

Nkana walijibu mapigo dakika ya 21 kupitia kwa Chikwekwe shuti lake lilienda nje, Namungo wakajibu shambulizi dakika ya 26 shuti la Sey lilienda nje katika dakika hiyo hiyo Hamis Nyenye alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Stephen Chulu.

Wageni walizidi kuliandama lango la Namungo na kupata faulo ya ndani ya boksi dakika ya 29 baada ya kipa Jonathan Nahimana kudaka mpira aliorudishiwa na mlinzi wake Jafar Mohamed lakini faulo iliyopigwa na Obbedy Masumbuko ilipaa juu ya lango.

Namungo walirudi kwa kasi dakika ya 33 lakini shuti la Shiza Kichuya lilienda nje, kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ alifanya mabadiliko dakika ya 36 kwa kumtoa Nyenye na kumuingiza Fredy Tangalo ili kuongeza nguvu katikati ya uwanja lakini hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinaisha hakuna mbabe.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Namungo walikosa bao dakika ya 46 Kikoti mpira wake wa kichwa ulienda nje, Nkana walijibu shambulizi dakika ya 55 ambapo Chikwekwe alikosa bao la wazi akiwa yeye na kipa Nahimana.

Dakika ya 62 kocha Morocco alifanya mabadiliko mengine akiwatoa Kikoti, Kichuya na Jafar Mohamed na kuwaingiza Miza Krystom, Eric Kwizera na Hamis Manyanya ili kuongeza nguvu katika kikosi chake mabadiliko ambayo hayakumsaidia.

Nkana walipata bao lao katika dakika ya 68 kupitia kwa Chikwekwe aliyetumia vyema pasi ya mlinzi wa kushoto Kakuta Chimwemwe, dakika ya 71 Steve Nzigamasabo alioneshwa kadi ya njano kwa kumpiga kiwiko Chulu.

Nkana walifanya mabadiliko yao dakika ya 78, Owen Masumbuko alimpisha Harrison Chisala, dakika ya 89 Stephen Chulu alimpisha Moses Nyond dakika ya 92 na Chisala alioneshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Nzigamasabo Steve.

Chanzo: www.habarileo.co.tz