Kasi ya kutupia mabao inayoonyeshwa na mastaa wa Yanga, Fiston Mayele, Heritioer Makambo na Fiston Mayele imelishtua benchi la ufundi la Namungo na wameanza kujipanga kabla ya mchezo wao utakaopigwa wikiendi ijayo mjini Lindi.
Mayele na Moloko kila mmoja ana mabao mawili katika Ligi Kuu nyuma ya Feisal Salum mwenye matatu na wawili hao juzi walitupia wakiizamisha KMKM 2-1, huku Makambo akifunga katika mechi yao ya kwanza ya kirafiki visiwani Zanzibar dhidi ya Mlandege wakiinolea makali Namungo.
Namungo inatarajiwa kuwa wenyeji wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Uwanja wa Ilulu, Lindi na kocha wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amekiri anajua ugumu unaomkabili dhidi ya Yanga kutokana na ukweli mechi zao huwa haziwi nyepesi.
Namungo katika michezo mitano, imeshinda mmoja, sare mbili na kupoteza miwili dhidi ya vigogo Simba na Azam.
Morocco amesema Yanga ni timu nzuri, haijapoteza mchezo wowote kati ya mitano iliyochezana katika Ligi Kuu na imekuwa bora hata katika michezo ya kirafiki hivyo wanajipanga vizuri kuwakabili wasiabike.
“Yanga ina wachezaji wengi wenye viwango hivyo unaona kabisa imejipanga, mechi baina yetu huwa ngumu, tunaendelea kujiandaa, ukizingatia hatuko katika nafasi nzuri, lazima tupambane ili tushinde,” amesema Morocco.