Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namungo yafurahia kucheza nyumbani

E980ce113144e1e9b99240f7197a9c60 Namungo yafurahia kucheza nyumbani

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KLABU ya Namungo FC imefurahia uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kurejesha mechi zote mbili za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Premer CD 1 Agosto ya Angola kuchezwa Tanzania.

Uamuzi wa kurudisha michezo hiyo ambayo kiutaratibu inachezwa nyumbani na ugenini, umefanywa na Caf kupitia kamati yake baada ya kubaini kuwa si Agosto wala Namungo iliyohusika moja kwa moja kukwamisha mchezo wa kwanza uliokuwa uchezwe Februari 14 nchini Angola.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu alisema kurejeshwa michezo hiyo nyumbani kwao ni ishara njema na inawapa faraja kubwa kufanya vizuri na kutinga hatua ya makundi.

“Unajua ni maamuzi sahihi waliyofanya baada ya kubaini hakuna upande ambao ulisababishwa mchezo wa kwanza usichezwe, kwetu kama wenyeji tunaona tuna msimu mzuri wa kutimiza malengo kwa kile tulichodhamiria,” alisema Zidadu

Alisema uamuzi huo wameupokea kwa mikono miwili na kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa Februari 21 ambapo Agosto watakuwa wenyeji lakini mechi itachezwa Tanzania.

“Bado tunaendelea kujipanga tangu tumewasili kutoka Angola kikosi bado kipo Dar es Salaam kinafanya mazoezi ya kujiandaa na kama ilivyokuwa michezo iliyopita malengo nikufanya vyema kutinga hatua ya makundi,” alisema Zidadu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Caf, michezo yote inatakiwa ichezwe angalau ndani ya saa 72 na iwe imechezwa kufikia Februari 26, mwaka huu.

Ratiba inaonesha Agosto itakuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza hivyo itawajibika kugharamia maandalizi yote ikiwamo gharama za maofisa wa mechi hiyo.

Kwa kuwa kwa utaratibu wa Caf inatarajiwa kupanga makundi ya Kombe la Shirikisho Februari 22, mshindi wa jumla kati ya Namungo na Agosto azitazingatiwa wakati wa upangaji ratiba.

Chanzo: habarileo.co.tz