Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namungo yaahidi mazuri kwa Pyramids

02e6ec9dbf7a508405857dbc78a33028.jpeg Namungo yaahidi mazuri kwa Pyramids

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Namungo leo wanashuka kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kucheza na Pyramids ya Misri katika mchezo wa pili hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Namungo iliyo kundi D wiki iliyopita ilipoteza mchezo wake wa kwanza kwa kufungwa bao1-0 na Raja Casablanca ugenini Morocco. Aidha, wapinzani wao Pyramids wametoka kushinda mabao 3-0 dhidi ya Nkana ya Zambia.

Mchezo wa leo bila kujali ubora wa timu wanayokutana nao Namungo wakijipanga na kuwaheshimu wapinzani wao wanaweza kupata matokeo mazuri. Mchezo uliopita japo walikuwa ugenini walionesha kiwango kizuri dhidi ya Raja hivyo,kile walichokifanya kule wakikionesha katika uwanja waliouzoea huenda wakapata matokeo.

Katika kundi D Namungo inachukuliwa kama timu ndogo kwasababu ndio mara ya kwanza inashiriki michuano hiyo haina uzoefu kama ilivyo kwa wapinzani wake.

Pyramids sio mara ya kwanza kuja Tanzania msimu wa mwaka 2019/2020 ilicheza na Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ambapo ilishinda mabao 2-1 na nyumbani kwao ikashinda mabao 3-0.

Msimu huo ukiwa wa kwanza kwake kushiriki michuano hiyo mikubwa ilifanya mapinduzi na kufika fainali ambako ilifungwa na SR Berkane ya Morocco bao 1-0. Katika ligi ya kwao kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwa pointi 25 katika michezo 15. Kwa upande wa Namungo inashika nafasi ya 10 kwa pointi 27 katika michezo 18 ikiwa nyuma michezo sita dhidi ya wengine.

Kocha Mkuu wa Namungo Hemed Morocco alisema kikosi chake kinajifunza kila mchezo hivyo ana imani atapata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kufanyia marekebisho.

“Kila mchezo tunajifunza, tulicheza mchezo wa kwanza ugenini na kuna mapungufu tuliyaona na tunaahidi kuyafanyia kazi. Tukijitoa kama tulivyofanya dhidi ya Raja ninaimani tutafanya vizuri dhidi ya Pyramids,”alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz