KOCHA wa Namungo FC , Hemmed Morocco amesema anakipanga kikosi chake kwa lengo la kumaliza mchezo mapema dhidi ya Rabita FC kwenye mchezo wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex keshokutwa.
Licha ya kutokuwa na taarifa za wapinzani wao hao, lakimi Morocco amesisitiza kuwa watatumia mbinu kuwamaliza mapema Rabita FC ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupenya raundi inayofuata.
Akizungumza Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru wakati wa mazoezi ya kikosi chake jana, Morocco alisema wako vizuri na wanaendelea na mazoezi huku wachezaji wake wote wako vizuri.
"Ni wawakilishi wa nchi kupitia Kombe la Shirikisho ni waambie tu, mipango na malengo yetu ni kumaliza mchezo mapema, tunahitaji ushindi mkubwa Ili tupate mteremko katika mchezo wa marejeano tukiwa ugenini, " alisema Morocco.
Alisema kazi anayoifanya kwa sasa ni kuboresha sehemu ya ushambuliaji, ambayo kwenye mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliotoka sare ya 1-1 dhidi ya Yanga, safu hiyo ilifanya makosa mengi.
"Sitaki changamoto hiyo irudie tena, tunahitaji kufanya kazi kwa kila mchezaji kutimiza wajibu wake kuiwakilisha nchi vyema kwenye michuano hii kwa sababu ni mara yetu ya kwanza," alisema Morocco aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni baada ya kutupiwa virago kwa Hitimana Thiery.
Namungo wamepata tiketi ya kuiwakilisha nchi baada ya kumaliza ya pili katika Kombe la FA kufuatia kufungwa na Simba, waliotwaa ubingwa huo wa Kombe la Shirikisho la Azam Federation Cup (FA), wanachukua nafasi ya Simba, ambao wanashiriki Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.