Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namungo kumpiga chini Kayembe

Kayembeeee Namungo kumpiga chini Kayembe

Sun, 14 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Namungo usiku wa leo inatarajiwa kuikabili Azam FC kwenye pambano la Ligi Kuu Bara linalopigwa Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 2:30 usiku, lakini mapema mabosi wa klabu hiyo walikuwa kwenye mazungumzo ya kusitisha mkataba na mshambuliaji, Alidor Kayembe.

Namungo iliyopo nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 36 baada ya mechi 27, inataka kumtema nyota huyo kutoka DR Congo kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake tangu alipojiunga nao Julai mwaka jana akitokea Red Arrows ya Zambia.

Kayembe alisaini mkataba wa miaka miwili lakini licha ya kutumikia mwaka mmoja tayari mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo ya kusitisha kandarasi iliyobaki kwa kile kinachoelezwa kushindwa kupambania namba.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo zililiambia Mwanaspoti ni kweli mazungumzo ya kuachana na nyota huyo yapo kwani licha ya kutegemewa kuleta ushindani kwa staa mwenzake, Reliants Lusajo ila imekuwa ni tofauti.

"Matarajio yalikuwa ni makubwa kwake hasa baada ya kufanya vizuri alikotoka na kuchukua ubingwa pia ingawa hapa mambo yamekuwa magumu kwani ameshindwa kucheza hata nusu ya mechi za msimu huu," kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Denis Kitambi akimzungumzia nyota huyo alisema hawezi kutoa ripoti ya mchezaji mmoja kwa sasa hadi msimu utakapoisha ndipo atakaa na viongozi kujadili hilo na maboresho kikosini.

"Tathimini ya timu tulishaifanya ila kwa sasa tunahitaji kwanza kumalizia michezo iliyobaki, kuhusu nani atabaki au ataondoka hilo litafahamika mwishoni mwa mwezi huu hivyo endelea kuvuta subra," alisema Kitambi.

Kayembe alisajiliwa na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hanour Janza aliyeachana nao Desemba 7, mwaka jana kurudi Zambia alipoteuliwa na Zesco United kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.

Chanzo: Mwanaspoti