Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imempeleka mwamuzi Abel William kwenye kamati ya waamuzi akajadiliwe katika kamati hiyo baada ya kuonekana alifanya makosa ya kutafsiri sheria 17 za soka kwenye mchezo wa Ligi Kuu kati ya Namungo dhidi ya Yanga
Taarifa ya bodi ya ligi imesema, uamuzi huo umekuja baada ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kujiridhisha kuwa mchezo huo kati ya Namungo FC na Yanga SC ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, ulikumbwa na matukiona na maamuzi yaliyoacha maswali juu ya utekelezaji wa sheria 17 za mpira wa miguu.
Mwamuzi Abel William kutoka Arusha alikumbwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wadau na mashabiki wa soka kutokana na namna alivyochezsha mchezo huo, ikiwemo maamuzi ya kutoa penati kwenda upande wa Namungo ambayo iliaminika haukustahili kuwa penati, lakini pia kabla ya penati hiyo kupigwa takribani wachezaji saba walionekana wakiwa kwenye eneo la 18 wakati mpigaji wa penati akiwa bado hajapiga penati hiyo.
Maamuzi haya ya Bodi ya Ligi ni kwa mujibu wa kikao chake cha Novemba 26, 2021. Ambapo kamati ya Usimamizi na Uendshaji wa Ligi ilipitia mwenendo na matukio mbali mbali ya Ligi na Kufanyia maamuzi.