Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namungo, Kagera zaenda sare

Kagera Namungo Mechi ya Namungo dhidi ya Kagera

Mon, 4 Oct 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Namungo wameshindwa kupata ushindi nyumbani katika Uwanja wa Ilulu Lindi baada ya kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Kagera Sugar katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Katika mechi hiyo Kagera walionekana kuanza vizuri na kufanya mashambulizi mengi ya mara kwa mara tofauti na wenyeji wao Namungo ambao kazi kubwa waliyofanya ni kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao.

Kwenye kipindi cha pili mambo yalibadilika kwa Namungo ambao walionekana kuwa bora na kuanza kushambulia zaidi mpaka kupata bao dakika dakika 53, kupitia kwa Raliants Lusajo ambaye alitumia makosa ya wachezaji wa Kagera.

Bao hilo lilitokana na mpira wa kurushwa na kiungo, Abdulaziz Makame 'Bui' na mabeki wa Kagera waliokoa vibaya kwa kichwa kumkuta, Lusajo akiwa mwenyewe kuweka mpira kambani.

Baada ya kufungwa bao hilo Kagera walibadilisha aina yao ya uchezaji na kuanza kushambulia zaidi kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza mpaka kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Mbaraka Yusuf aliye unganisha kwa kichwa.

Mbaraka alifunga bao hilo dakika 70, kwa kichwa akiwa huru baada ya mabeki wa Namungo kushindwa kumsumbua au kuokoa krosi iliyotoka upande wa kulia mwa Kagera.

Kutokana na matokeo hayo katika msimamo wa ligi Namungo watakwenda mpaka nafasi ya tatu wakiwa na pointi nne wakizishusha, Mbeya City, Mbeya Kwanza na Simba wakati Kagera wao watakuwa nafasi ya 11 na pointi yao moja.

Kabla ya mechi hiyo Namungo walishinda mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa ligi mabao 2-0, waliocheza katika uwanja huo huo dhidi ya Geita Gold na mabao yao yalifungwa na Lusajo mwenye mawili mpaka sasa na Shiza Kichuya.

Kagera wao mchezo wa ufunguzi wa ligi walianza vibaya kwa kufungwa bao 1-0, nyumbani katika Uwanja wa Kaitaba Bukoba dhidi ya Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti